SERIKALI, USAID AFYA YANGU- RMNCAH WABORESHA HUDUMA ZA LISHE MKOANI MARA - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Monday, 18 September 2023

SERIKALI, USAID AFYA YANGU- RMNCAH WABORESHA HUDUMA ZA LISHE MKOANI MARA

Zaidi ya watoto elfu moja wamepatiwa matibabu ya ugonjwa wa utapiamlo mkoani Mara katika kipindi cha mwaka 2022/23 ambapo kati yao, zaidi ya watoto 600 tayari wamepona ugonjwa huo.

Mganga Mkuu wa Mkoa Mara, Dkt. Zabrone Masatu ameyasema hayo wakati akielezea jitihada zinazofanywa na Serikali kwa kushirikiana na wadau katika kutoa elimu kwa jamii na kuboresha huduma za afya katika vituo vya afya na hospitali mkoani humo.

Dkt. Masatu amesema Serikali kupitia mradi wa USAID Afya Yangu- RMNCAH wamefanikiwa kutoa matibabu ya utapiamlo kwa watoto 1,090 ambapo kati yao watoto 608 tayari wamepona kabisa ugonjwa huo unaotokana na lishe duni hususani kwa watoto.

Amesema baadhi ya watoto wenye utapiamlo wamekuwa wakichelewa kupata matibabu kutokana na wazazi kuamini imani za kishirikina na hivyo kuwapeleka kwa waganga wa tiba asili wakidhani wamelogwa na hivyo kuchelewa kupata tiba sahihi ya chakula lishe.

Dkt. Masatu amesema kutokana na imani hiyo, zaidi ya watoto 20 waliobainika kuwa na ugonjwa wa utapiamlo wamekatisha matibabu ambapo jitihada za kuwafuatilia zinaendelea kupitia kwa watoa huduma za afya ngazi ya jamii ambao wamepewa mafunzo na wamekuwa wakiwabaini pia watoto wenye utapiamlo.

“Tumekuwa tukifanya kazi na mradi wa USAID Afya Yangu- RMNCAH ili kuhakikisha tunaboresha afya ya watoto ambapo tumewajengea uwezo watumishi wetu na wahudumu wa afya ngazi ya jamii ambao wanatusaidia kuwatambua watoto wenye utapiamlo na kuwaunganisha na tiba” amesema Dkt. Masatu;

“Pia kupitia mradi wa USAID Afya Yangu- RMNCAH tumepata vibao 52 kwa ajili ya kutusaidia kupima viashiria vya utapiamlo kwa watoto katika vituo vyetu vya afya, tunashukuru Serikali kupitia mradi huu kila Halmashauri katika Mkoa wetu sasa ina Afisa Lishe anayesaidia kwenye utoaji huduma na kuwaelimisha wananchi kuandaa chakula lishe” ameongeza Dkt. Masatu.

Naye Afisa Lishe wa Halmashauri ya Bunda Mji katika Wilaya ya Bunda mkoani Mara, Lucy Mwaluwyo amesema wakati mradi wa USAID Afya Yangu- RMNCAH unaanza, kwa mwezi zaidi ya watoto 16 walikuwa wakitibiwa katika hospitali ya Bunda DDH na Manyamanyama tofauti na sasa ambapo idadi hiyo imepungua kwa wastani wa watoto sita hadi nane kwa mwezi.

Mwaluwyo amesema tayari amefanya kikao na waganga wa kienyeji na kuwaelimisha ili wanapoona mtoto mwenye dalili za utapiamlo ambazo ni pamoja na mtoto kunyong’onyea na mwili kuishiwa nguvu wawashauri wazazi kuwapeleka hospitalini.

Mmoja wa wakazi wa Kijiji cha Guta wilayani Bunda, Regina Samson amesema baada ya mwanae kuugua utapiamlo, hakujua ni ugonjwa gani hivyo ndugu walimshauri ampeleke kwa mganga wa kienyeji ambapo hata hivyo baada ya kumfikisha huko mtoto hakupona na hali yake ilizidi kuwa mbaya.

Baada ya Regina kuona hali ya mwanae inazidi kubadilika alimpeleka katika Hospitali ya Bunda DDH ambapo alibainika kuwa na ugonjwa wa utapiamlo na kuanzishiwa tiba ya chakula lishe iliyomsaidia mwanae kupona kabisa baada ya muda wa wiki tatu.

Hata hivyo hatua ya Regina kumtoa mwanae kwa mganga wa kienyeji na kumpeleka hospitalini ilipokelewa tofauti na mama mkwe wake aliyeamua kumtorosha mjukuu wake hospitalini ili kumrudisha kwa mganga wa kienyeji lakini kutokana na jitihada za watoa huduma za afya walimfuatilia na kumresha kwenye matibabu huku mvutano huo ukisababisha ndoa yake inayotajwa kuwa ya ‘nyumba ntobhu’ kuvunjika na hivyo kurejea nyumbani.

Mkasa mwingine kama huo umemsibu Remi Mayenga mkazi wa Kijiji cha Nyatwali wilayani Bunda aliyebaini mtoto wa kaka yake mwenye umri wa miaka miwili mkazi wa Bariadi mkoani Simiyu amepelekwa kwa mganga wa kienyeji baada ya afya yake kudhoofika ambapo baada ya kumchukua na kumfikisha hospitalini alibainika kuwa na utapiamlo.

“Nilimpeleka katika Hospitali ya Bunda DDH akapatiwa matibabu kwa muda wa wiki tatu na sasa amepona. Wahudumu walitufundisha jinsi ya kutengeneza uji wa lishe kwa kutumia mtama, mchele, mbegu za maboga, michembe, karanga, soya na ufuta. Sasa anaendelea vizuri, nawashauri wananchi wenzangu kwamba si kila kitu ni kukimbilia kwenye mitishamba ama kwa waganga wa kienyeji” amesema Regina.

Mganga Mkuu mkoani Mara, Dkt. Zabrone Masatu amebainisha kuwa kabla ya mradi wa USAID Afya Yangu- RMNCAH kuanza, matibabu ya utapiamlo yalipatikana katika Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Mara iliyopo wilayani Msoma na ile ya Shirati iliyopo wilayani Rorya lakini baada ya mradi huo, matibabu yanapatikana katika vituo vinne vya afya na hospitali 11 hatua ambayo imeondoa hatari kwa watoto chini ya miaka mitano kupoteza maisha kutokana na ugonjwa huo.

Dkt. Masatu amesema kupitia mradi huo wa USAID Afya Yangu- RMNCAH, pia wanajamii wamefundishwa namna ya kuandaa vyakula vyenye lishe ambavyo vinapatikana katika mazingira yanayowazunguka ikiwemo dagaa, mtama, karanga, mhogo na mahindi hatua hatua iliyosaidia idadi ya watoto wanaougua utapia mlo kupungua.
Na George Binagi, Mara
Mtoto akinywa uji wa lishe.
Mkazi wa Kijiji cha Nyatwali Wilaya ya Bunda mkoani Mara, Remi Manabu akieleza jinsi tiba ya chakula lishe ilivyomsaidia mtoto wa kaka yake.
Bibi Mang'era Mang'era (62) mkazi wa Kijiji cha Guta Wilaya ya Bunda mkoani Mara akieleza namna tiba ya chakula lishe inayotolewa na hospitali ya Bunda DDH ilivyomsaidia mjukuu wake kupona ugonjwa wa utapiamlo.
Bibi Mang'era Mang'era (62) mkazi wa Kijiji cha Guta Wilaya ya Bunda mkoani Mara akiwa na mjukuu wake aliyepata tiba ya chakula lishe katika Hospitali ya Bunda DDH. Bibi Mang'era ndiye mama mzazi wa Regina Samson/ mama mzazi wa mtoto.
Bibi Mang'era Mang'era (62) mkazi wa Kijiji cha Guta Wilaya ya Bunda mkoani Mara akiwa na mjukuu wake aliyepata tiba ya chakula lishe.
Afisa Lishe Halmashauri ya Bunda Mji katika Wilaya ya Bunda mkoani Mara, Lucy Mwaluwyo akieleza jitihada zilizofanywa na Serikali kwa kushirikiana na wadau kupitia mradi wa USAID Afya Yangu- RMNCAH kuimarisha huduma ya tibalishe kwa ajili ya watoto wenye utapiamlo katika hospitali ya Bunda DDH na Manyamanyama.

No comments:

Post a Comment