NMB YASHINDA TENA TUZO YA KUONGOZA KUWAFADHILI WAJASIRIAMALI - AFRIKA - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Monday, 18 September 2023

NMB YASHINDA TENA TUZO YA KUONGOZA KUWAFADHILI WAJASIRIAMALI - AFRIKA

Mkuu wa Idara ya Biashara wa Benki ya NMB – Bw. Alex Mgeni (katikati) katika picha ya pamoja na Afisa Mtendaji Mkuu wa Shirika la IFC aliemaliza muda wake Bw. Matthew Gamser  pamoja na Afisa Mtendaji Mkuu wa Shirika la IFC Bw. Qamar Saleem, baada ya kupokea tuzo ya Mwezeshaji Bora wa Kifedha kwa Biashara Ndogo na za Kati (SMEs) katika bara la Afrika, kwa niaba ya Benki ya NMB.

Mkuu wa Idara ya Biashara wa Benki ya NMB – Bw. Alex Mgeni (pili kulia) akipokea tuzo ya Mwezeshaji Bora wa Kifedha kwa Biashara Ndogo na za Kati (SMEs) katika bara la Afrika kwa Mwaka 2023 kutoka kwa  Waziri  wa Muungano wa Biashara Ndogo na za Kati wa Serikali ya India - Bw. Narayan Rane, katika hafla ya tuzo za Kimataifa za Mitaji kwa Biashara Ndogo na za Kati (Global SME Awards) iliyofanyika Jijini Mumbai, India mwishoni mwa wiki. Kulia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la IFC Bw. Qamar Saleem na Kushoto ni Mkurugenzi wa Benki Kuu ya India - Bw. India Alok Kumar Choudhary.

BENKI ya NMB imetunukiwa tena tuzo na jukwaa la kufadhili ujasiriamali duniani (SME Finance Forum) kutokana na huduma zake wezeshi na ufadhili wake wa kuwaendeleza wafanyabiashara wadogo na wa kati nchini wakati wa mkutano wa jukwaa hilo uliofanyika September 14 katika jiji la Mumbai nchini India.

Ushindi iliyoupata Benki hiyo kwenye tuzo za mwaka huu za ufadhili wa ujasiriamali duniani (Global Finance Awards 2023 - GSMEFF 2023), ni wa Mfadhili wa Ujasiriamali wa Mwaka upande wa Afrika uliyoipa tuzo ya fedha (Silver Award).

Kama ilivyokuwa kwa tuzo zingine, tuzo za GSMEFF 2023 zinatambua dhamira na mafanikio ya taasisi za kifedha na kampuni zinazojihusisha na teknolojia za huduma za kifedha (fintech) katika kuwahudumia wateja wao ambao ni wajasiriamali wadogo na wa kati.

Pamoja na mambo mengine, tuzo hii imetambua mchango wa NMB katika kuwawezesha wajasiriamali kukuza biashara zao kwa: Kuwapa mikopo yenye riba nafuu kwa wakati, kuwapa elimu ya fedha kuhusu jinsi gani watazidi kukuza biashara zao kupitia majukwaa yao ya Business Clubs, Business Executive Network na mengine. Pia, kuwawezesha kupokea malipo kidijitali kupitia NMB Lipa Mkononi na njia zingine za kidijitali, kuwawezesha kukopa kidijitali bila kuwa na dhamana yoyote kupitia huduma ya Mshiko Fasta na kuendelea kufurahia huduma za kibenki kwa urahisi kupitia NMB Mkononi na Wakala popote pale wanapokuwa

Heshima hii ni ushahidi mwingine wa juhudi za dhati za benki hiyo za kuziba pengo la kuwafadhili wajasiriamali na uwekezaji inaoufanya katika uvumbuzi wa kidijitali nchini. NMB inazingatia maendeleo ya wafanyabiashara hao kutokana na mchango wao mkubwa katika ujenzi wa Taifa kwa kutengeneza ajira, kuchochea ukuaji wa uchumi na kuimarisha mapato ya wananchi.

Tuzo hizi na heshima iliyopata NMB ni ushahidi wa mwendelezo wa ubora wa huduma na dhamira ya dhati ya ubunifu wake. 

Katika pongezi zake kwa washindi, Afisa Mtendaji Mkuu wa jukwaa la kufadhili ujasiriamali duniani (SME Finance Forum), Bw. Matthew Gamser, alisema ushindani wa mwaka huu ulikuwa mkubwa kutokana na washiriki kuwa wengi wakitoka katika nchi nyingi ikilinganishwa na miaka ya nyuma.

SME Finance Forum, inayoratibiwa na Shirika la Fedha la Kimataifa (IFC) la Benki ya Dunia, ilianzishwa mwaka 2012 na nchi 20 tajiri duniani (G20) chini ya mwamvuli wa Ushirikiano wa Kimataifa wa Ujumuishaji wa Kifedha (GPFI). 

Majukumu yake makubwa ni pamoja na kusimamia wanachama wake kubadilishana maarifa, kuchochea ubunifu na kukuza ukuaji wa wajasiriamali.


No comments:

Post a Comment