Na Mwandishi Wetu
WIZARA ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi imeboresha huduma zake kutoka analogia kwenda kidigitali unaowezesha taarifa za wamiliki wa ardhi kuwa kwenye mfumo wa kielektroniki na kuharakisha taratibu za utoaji hati.
Hayo yamebainishwa na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Bi. Lucy Kabyemera tarehe 6 Julai 2023 wakati akizungumza na vyombo vya habari kwenye Banda la Wizara ya Ardhi linatoa huduma mbalimbali ikiwemo utoaji Hatimiliki za Ardhi za hapo kwa hapo katika Maonesho ya 47 ya Biashara Sabasaba yanayoendelea jijini Dar es Salaam.
Wizara ya Ardhi inatumia fursa ya Maonesho ya Sabasaba ya mwaka huu 2023 kutoa Hati Milki za Ardhi kwa wateja waliokamilisha taratibu za kupatiwa hati wanaotembelea Banda la Wizara pamoja na huduma nyingine zinazohusu sekta ya ardhi.
Kwa mujibu wa Bi.Kabyemera, lengo la Wizara yake kubadili mifumo yake ni kuharakisha huduma za sekta ya ardhi kupitia mfumo unganishi wa taarifa za ardhi ambao kwa kiasi kikubwa unawezeshwa na mfumo wa ILMIS wenye uwezo wa kuweka kumbukumba na taarifa za ardhi kwenye mfumo wa kidijitali.
Akitolea mfano wa ufanisi wa mfumo huo kupitia Maonesho ya Biashara ya 47 hapa nchini, Naibu Katibu Mkuu huyo alieleza kuwa, kupitia mfumo huo wa kieletroniki baadhi ya wananchi waliokamilisha taratibu za umilikishwaji ardhi wanapatiwa hati mara moja mara wanapofika katika Banda la Wizara.
Aidha, Bi. Kabyemera aliviambia vyombo vya habari kuwa, jukumu kubwa la Wizara yake ni kuhakikisha kuwa kuna usalama wa milki hapa chini ikiwemo kupanga kupima na kumilikisha ardhi pamoja na ramani za mipango miji akiutaja mfumo tajwa kuwa unaifadhi kumbumbu zote na hivyo kurahisisha utoaji huduma za ardhi kuwa za haraka na za uhakika.
‘’ Kwa sasa wizara yetu mbali na mambo mengine ina kazi ya uendelezaji miji, Nyumba, Viwanja na Mashamba ikiwemo sehemu ya uendelezaji Makazi’’. Alisema Bi. Kabyemera
Akiangazia suala la Serikali kutoa kodi ya ongezeko la thamani katika sekta ya Nyumba hapa Nchini. Bi. Kabyemera alibainisha kuwa watanzania wengi hawana uwezo wa kumudu gharama kubwa za Nyumba hivyo kutolewa kwa kwa kodi ya oingezeko la thamani kutawawezesha wanachi wengi kumudu gharama za nyumba.
Aidha Bi. Kabyemera alitaja nyumba zenye sifa ya kusamehewa kodi hiyo kuwa ni nyumba za gharama nafuu ambazo hazidi shilingi Milioni 50 za kitanzania lengo likiwa kuwezesha watanzania wengi kumiliki nyumba za gharama nafuu.
Naye Bw. Manase Ndazi aliyefanikiwa kujipatia hati yake kupitia ushiriki wa Wizara ya Ardhi alisema, amefurahi kupata hati yake kwani itamwezesha kukuwa kiuchumi kwani moja ya faida za hati ni kuwezesha mwanachi kama dhamana ya kupata mkopo kwa ajili ya kuendeleza biashara yake.
‘’Nikiwa ndani ya kiwanja chenye hati najiamini na Wizara inatambua kwamba nina hati na hati ndo kila kitu na siwezi kuwa nawasiwazsi na matumizi ya kiwanja changu’’. Alihitimisha Bw. Ndazi.
Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi inashiriki Maonesho ya Biashara ya Kimataifa ya 47 na inaendelea kutoa huduma za hati, kutatua changamoto kwa wananchi zilizopo, kutoa elimu kwa umma pamoja na kushirikiana na sekta binafsi kutoa huduma za ardhi kupitia maonesho hayo.
No comments:
Post a Comment