TAFITI ZIFANYIKE KUWEZESHA MPANGO WA AFYA MOJA KUFANIKIWA - MAJALIWA - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Tuesday, 5 November 2024

TAFITI ZIFANYIKE KUWEZESHA MPANGO WA AFYA MOJA KUFANIKIWA - MAJALIWA




WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa ameziagiza idara na taasisi za utafiti na elimu ya juu ziendelee kufanya tafiti za kisayansi ili kutafuta suluhisho za changamoto zenye mwingiliano wa afya ya binadamu, afya ya wanyama, na afya ya mazingira. 

Ameongeza kuwa idara na taasisi za Serikali zinapaswa kutumia matokeo ya tafiti hizo katika utekelezaji wa mipango mbalimbali ya kitaifa.

Ametoa maagizo  hayo Novemba 04, 2024 alipofungua Mkutano wa Kitaifa wa Afya Moja katika kituo cha Mikutano cha Kimataifa  Arusha (AICC) Jijini Arusha.

Aidha, Mheshimiwa Majaliwa ametoa wito kwa Taasisi zinazohusika na masuala ya afya ya jamii, wanyama na mazingira zitenge fedha na kuweka katika mipango ya taasisi hizo afua za kuthibiti magonjwa ya kizonotiki, usugu wa vimelea dhidi ya dawa, magonjwa yasiyoambukiza, mabadiliko ya tabia nchi, na usalama wa chakula.

“Wizara za kisekta, na Mamlaka za Serikali za Mitaa, andaeni mipango kazi na taratibu za usimamizi kwa ajili ya utekezaji wa mbinu ya Afya Moja kwa kuzingatia miongozo iliyopo ambayo imeweka bayana majukumu ya wadau wote”

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amezitaka taasisi hizo kufanya vikao vya mara kwa mara, tathmini ya utekelezaji wa pamoja wa afua mbalimbali ili zijulikane mapema na kupatiwa ufumbuzi.

"Idara na taasisi za utafiti na elimu ya juu ziendelee kufanya tafiti za kisayansi ili kutafuta suluhisho za changamoto zenye mwingiliano wa afya ya binadamu, afya ya wanyama, na afya ya mazingira."

Kadhalika, Mheshimiwa Majaliwa amesisitiza ushirikiano wa kisekta na jamii katika kupunguza na kudhibiti athari zitokanazo na majanga milipuko ya magonjwa, usugu wa vimelea vya magonjwa dhidi ya dawa, usalama wa chakula, magonjwa yasiyoambukiza, na matishio mengine ya afya ya jamii.

Kwa upande wake Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu, Ummy Nderiananga amesema, Ofisi ya Waziri Mkuu inaendelea kusimamia Dhana ya Afya Moja ili iendelee kupewa kipaumbele na wadau mbalimbali kwani suala hilo linagusa sekta nyingi.

Naye, Waziri wa Mifugo na Uvuvi Abdala Ulega amesema Serikali kupitia wizara ya Kilimo imetenga shilingi bilioni 28, kwa lengo na dhamira ya kufanya kampeni ya chanjo kwa mifugo yote Nchini.

Awali, Naibu waziri wa Nchi OR- TAMISEMI Festo Ndugange, alisema utekelezaji wa mpango wa afya moja ni suala la muhimu katika kudumisha na kuimarisha afya ya jamii, hivyo wizara hiyo itaendelea kuahirikiana na wizara nyingine katika kukinga na kupambana na changamoto za magonjwa ambukizi kutoka kwa wanyama kwenda kwa binadamu.

No comments:

Post a Comment