MAWAZIRI EAC KUONGEZA KASI YA UTEKELEZAJI WA MIPANGO NA MAKUBALIANO - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Friday, 8 November 2024

MAWAZIRI EAC KUONGEZA KASI YA UTEKELEZAJI WA MIPANGO NA MAKUBALIANO

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, IKULU Zanzibar Mhe. Ali Suleiman Ameir akifuatilia Mkutano wa 34 wa Baraza la Kisekta la Mawaziri wa Jumuiya ya Afrika Mashariki linaloshughulikia masuala ya Afrika Mashariki na Mipango uliofanyika katika Makao Makuu ya Jumuiya jijini Arusha tarehe 8 Novemba 2024.

Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki anayesimamia masuala ya Afrika Mashariki Balozi Stephen P. Mbundi akiongoza Mkutano wa 34 wa Baraza la Kisekta la Mawaziri wa Jumuiya ya Afrika Mashariki linaloshughulikia masuala ya Afrika Mashariki na Mipango, Novemba 8, 2024.

MAWAZIRI wanaosimamia masuala ya Afrika Mashariki na Mipango katika Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki wamekubaliana kuongeza kasi ya utekelezaji wa mipango, maagizo na makubaliano mbalimbali yaliyofikiwa katika Jumuiya.

Hayo yamejiri katika Mkutano wa 34 wa Baraza la Kisekta la Mawaziri wa Jumuiya ya Afrika Mashariki linaloshughulikia masuala ya Afrika Mashariki na Mipango uliofanyika leo tarehe 08 Novemba 2024 katika Makao Makuu ya Jumuiya jijini Arusha. 

 

Miongoni mwa masuala hayo ni pamoja na utekelezaji wa Itifaki ya Soko la Pamoja la Jumuiya ya Afrika Mashariki ambayo inahusisha vipengele mbalimbali ikiwemo uondoaji wa tozo na ada katika shughuli mbalimbali za kiuchumi ikiwemo usafirishaji, biashara na ajira. 

 

Suala jingine ni la uondoaji wa vikwazo visivyo vya kiforodha katika biashara, ambapo licha ya kuripotiwa kuwa jumla ya vikwazo 274 vimeondolewa tangu mwaka 2007 wamekubaliana kuendelea kubaini vikwazo ambavyo havijafanyiwa kazi kikamilifu sambamba na uharakishwaji wake katika kuvitatua ili kuwarahishia wananchi katika Jumuiya kuendesha shughuli zao za kiuchumi kwa ufanisi na tija zaidi. 

 

Agenda nyingine zilizojadiliwa katika mkutano huo ni; Taarifa ya Utekelezaji wa Utatu wa Pamoja wa COMESA-EAC-SADC, Maandalizi ya Mkakati wa Saba (7) wa Maendeleo wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (2026/2027- 2030/31) na Hadidu za Rejea za Dira ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ya Mwaka 2050, taarifa ya maandalizi ya maadhimisho ya miaka 25 ya kuanzishwa kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki na Mapitio ya Utekelezaji wa Mkakati wa Sita (6) wa Maendeleo wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (2021/2022- 2025/26).

 

Mkutano huo wa 34 wa Baraza la Kisekta la Mawaziri wa Jumuiya ya Afrika Mashariki uliofanyika kwa njia mseto (video na ana kwa ana) na kuhudhuriwa na Nchi Wanachama wote wa Jumuiya, ulitanguliwa na Mkutano wa ngazi ya Wataalamu uliofanyika tarehe 4-6 Novemba, 2024 na kufuatiwa na Makatibu Wakuu uliofanyika tarehe 7 Novemba 2024. 

 

Ujumbe wa Tanzania katika mkutano huo umeongozwa na Mhe. Ali Suleiman Ameir, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, IKULU Zanzibar.

No comments:

Post a Comment