Na Mwandishi Wetu
KAMPENI ya uhamasishaji wa kuweka akiba ya Benki ya NMB iliyopewa jina la ‘Bonge la Mpango’ Msimu wa Tatu ilifikia kilele jana na kuwafanya wateja wenye bahati kushinda zawadi nono zenye thamani ya shilingi milioni 69.5 wakati wa droo kubwa ya kampeni hiyo iliyofanyika kwenye banda la benki hiyo katika Viwanja vya Sabasaba jijini Dar es Salaam.
Zawadi zilizoshindwa ni pamoja na bajaji za mizigo tano zenye thamani ya shilingi millioni 25, pikipiki 11 zenye thamani ya shilingi millioni 33, friji (jokofu) la kisasa la milango miwili, Smart Tv, mashine ya kufulia nguo, Laptop, simu ya Samsung Z Flip pamoja na simu ya iphone 14 ProMax.
Akizungumza wakati wa kuchezesha droo hiyo, Mkuu wa Mtandao wa Matawi na Mauzo ya Rejareja wa Benki ya NMB, Donatus Richard alisema kampeni ya benki hiyo ilikuwa na lengo kuu la kuhamasisha uwekaji wa akiba na ililenga kukuza utamaduni wa kuweka akiba kwa wateja wake.
“Tulikuja na kampeni hii ambayo kwa namna moja au nyingine imeweza kusaidia idadi kubwa ya wateja wetu kuwa na tabia ya kujiwekea akiba ili wasipate wakati mgumu wanapokumbana na masuala yenye udharura,” alisema Richard.
Richard alisema katika droo za awali za kampeni hiyo, benki yake ilitoa zawadi za shilingi milioni 110 kwa wateja wake 178 wakati wa kampeni hiyo iliyozinduliwa mnamo tarehe 29 Machi, 2023.
“Ili kurudisha faida tunayoipata kama benki kwa wateja wetu, tulizindua promosheni hii Tarehe 29 Machi na tumeshuhudia zawadi za pesa taslimu, vifaa mbalimbali vya kielektroniki zikiwemo friji, TV, pikipiki huku zawadi za pesa zikiwekwa katika akaunti za washindi, lengo likiwa kuhamasisha wateja kuendelea kuwa na akiba katika akaunti zao,” alisema Richard.
Aliongeza kuwa benki yake inatambua kuwa uwekaji wa akiba kwa watanzania ni jambo gumu kidogo kwani wengi wao hushindwa kutunza pesa iliziweze kuwasaidia baadae na badala yake hulazimika kukopa mikopo tena kwa riba kubwa.
Richard alisema kuwa kutokana na hilo, benki yake imejidhatiti kuendelea kuhamasisha matumizi ya akaunti za NMB kwa wateja wake kama njia ya kuhifadhia fedha na kujiwekea akiba.
Katika hafla hiyo, Mwakilishi wa Bodi ya Bahati Nasibu Tanzania Ibrahim Sakina aliipongeza benki hiyo kwa kuzindua kampeni ambayo siyo tu inahamasisha uwekaji akiba, bali pia inaongeza matumizi ya fedha kupitia mifumo rasmi.
“Sisi kama bodi, tunaipongeza benki ya NMB kwa kuanzisha kampeni hii. Katika droo ya leo, kumekuwepo na uwazi wa hali ya juu na washindi wote wamepatikana kihalali,” alisema.
Washindi wa zawadi za promosheni ya ‘Bonge la Mpango’ Msimu wa Tatu ya Benki ya NMB wanatarajiwa kukabidhiwa zawadi zao Ijumaa wiki hii.
No comments:
Post a Comment