WANDAAJI WA MICHEZO WATAKIWA KUSHIRIKIANA NA VYAMA VYA MCHEZO - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Tuesday 13 December 2022

WANDAAJI WA MICHEZO WATAKIWA KUSHIRIKIANA NA VYAMA VYA MCHEZO


Na Shamimu Nyaki

NAIBU Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Pauline Gekul ametoa wito kwa Wadau wanaoandaa mashindano mbalimbali ya michezo kuwaalika Vyama vya Mchezo husika, ili viweze kuona vipaji vinavyooneshwa katika Mashindano hayo, ili viweze kusaidia Taifa.

Mhe. Gekul, ametoa wito huo Desemba 10, 2022 Wilayani Moshi Mjini, wakati akifunga mashindano ya michezo yaliyoandaliwa na Umoja wa Wanawake wa Chama Cha Mapinduzi Wilayani hapo, ambapo amesisitiza Maafisa Utamaduni na Michezo kutoa ushirikiano wa kutosha kwa Wadau wanaofanya shughuli za Utamaduni, Sanaa na Michezo katika maeneo yao.

"Jukumu la kukuza michezo sio la Serikali pekee, nawapongeza UWT kwa kuandaa Mashindano haya ambayo yametoa nafasi kwa vijana kuonesha uwezo wao katika Sanaa na Michezo, Naendelea kusisitiza Mamlaka za Serikali za Mitaa kutenga maeneo ya michezo, kuyalinda yasivamiwe, lakini pia bajeti ya michezo itumike katika michezo," amesisitiza Mhe. Gekul.

Amesisitiza Jamii kufanya mazoezi kila Jumamosi ya mwisho wa mwezi kama maelekezo ya Serikali chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan yanavyoelekeza ili kujikinga na magonjwa yasioambukiza pamoja na kuimarisha afya.

Aidha, ameitakia Jamii kuzingatia maadili, Mila na Desturi za Tanzania zilizo njema na kujiepusha na vitendo vya Ukatili wa kijinsia, huku akieleza kuwa upatikanaji wa Vazi la Taifa, Kamati iliyoundwa na Waziri Mhe. Mohamed Mchengerwa inaendelea na kazi hiyo.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa UWT Wilayani hapo Mhe.Theresia Komba amesema lengo la Mashindano hayo ni kuimarisha afya, kujenga uhusiano miongoni mwa jamii, kuinua vipaji pamoja na kujikinga na magonjwa yasiyoambukiza.

Mashindano hayo yamehusisha mpira wa miguu wanawake, Netiboli, kivuta kamba pamoja na michezo ya jadi ikiwemo kukimbia na magunia, kufukuza kuku, huku  yakipambwa na burudani kutoka kwa Wasanii wa wilaya hiyo.

No comments:

Post a Comment