SEKTA YA UJENZI YAPIKWA KUSHUGHULIKIA MAAFA - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Monday 12 December 2022

SEKTA YA UJENZI YAPIKWA KUSHUGHULIKIA MAAFA

Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi (Sekta ya Ujenzi), Eng. Godfrey Kasekenya, akifafanua jambo kwa washiriki wa mafunzo ya kushughulikia maafa kwa wahandisi na mafundi sanifu wa Sekta hiyo na Taasisi zake mkoani Mwanza.

Mkurugenzi Msaidizi kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu, Luteni Kanali Masalamado akizungumza katika ufunguzi wa mafunzo ya kushughulikia maafa kwa wahandisi na mafundi sanifu wa Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi (Sekta ya Ujenzi) na Taasisi zake yanayofanyika mkoani Mwanza.

NAIBU Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi (Sekta ya Ujenzi), Eng. Godfrey Kasekenya, ameziagiza taasisi zilizo chini ya Wizara yake kuweka juhudi na kuwa tayari kupambana na maafa kwa kutumia rasilimali walizonazo katika maeneo yao ya kazi.

Eng. Kasekenya amezungumza hayo wakati akifungua mafunzo ya siku tano kwa wahandisi na mafundi sanifu yalioanza leo mkoani Mwanza ambapo amesisitiza kila mtumishi kutimiza wajibu wake kwa kuzingatia masuala ya upunguzaji vihatarishi vya maafa katika utekekelezaji wa majukumu yao.

 

“Sisi kama Serikali tutaendelea kuwajengea uwezo watumishi wa utayari wa kushugulikia majanga na kuwa na mipango madhubuti ya kujiandaa na kupunguza vihatarishi kwa maafa kadri inavyowezekana ili kujenga jamii iliyo na ustahamilivu wa maafa’’ amesisitiza Kasekenya.

 

Kasekenya amewataka mafundi wasanifu na wahandisi kutumia fursa ya uwepo wao wa siku tano katika mafunzo hayo kuhakikisha wanajijengea uwezo na utayari wa kushugulikia maafa.

 

“Nimatumaini yangu kuwa mafunzo haya yatawasaidia kutambua vihatarishi vya maafa, ufanyaji tathimini za maafa na taratibu zipi zitakazotumika katika uokoaji”, amesema Kasekenya.

 

Amebainisha kuwa maafa yamekuwa yakisababisha matokeo hasi katika maendeleo ya kijamii na kiuchumi kutokana na kupotea kwa mafanikio yaliyopatikana kwa muda mrefu na hivyo kuzorotesha hatua za maendeleo ambazo zilikuwa zimeshafikiwa katika eneo husika.

 

“Sekta ya ujenzi imekuwa ikiathirika na majanga ya asili yatokanayo na mvua zisizokuwa za kawaida ambazo husababisha uharibifu wa miundombinu ya barabara na hivyo huathari shughuli za kiuchumi na kupelekea kusimama kwa uzalishaji”, amefafanua Kasekenya.

 

Ameeleza kuwa Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi, Sekta ya Ujenzi itaendelea kushirikiana vyema na kwa ukaribu zaidi na wadau mbali mbali katika kuimarisha mfumo wa uratibu na usimamizi wa maafa nchini.

 

Naye Mkurugenzi wa Idara ya Usalama na Mazingira kutoka Sekta ya Ujenzi Eng. Kashinde Mussa, amesema kuwa mafunzo hayo ni shirikishi ambayo yatakuwa na fursa za kutembelea miundombinu ya vivuko, barabara na majengo kwa ajili ya kufanya mafunzo kwa vitendo. 


 

Mhandisi kutoka Kitengo cha Ujenzi wa Viwanja vya Ndege, Peter Sikalumba amesema miundombinu wanyaojenga imekuwa ikikumbwa na changamoto mbalimbali haswa za majanga yanayotokana na matukio ya asili kama vile moto, mvua na vimbunga hivyo kupitia mafunzo haya watakuwa wamepata namna bora ya kukabiliana na majanga hayo.

 

Mafunzo hayo yanatolewa na Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) kwa kushirikiana na Taasisi za Mamlaka ya Hali ya Hewa, Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, Mamlaka ya Usimamizi wa Usalama na Afya Kazini (OSHA) na Timu ya kukabiliana na Maafa ya Mkoa wa Dar es Salaam.

No comments:

Post a Comment