Na Mwandishi Wetu, Pwani
HOSPITALI ya Rufaa Mkoa wa Tumbi, wilayani Kibaha mkoani Pwani, inatarajia kuanza kutoa huduma ya kusafisha damu kwa wagonjwa wa figo kuanzia katikati ya mwezi Desemba mwaka huu.
Kuanza kwa huduma hiyo ni matokeo ya maboresho yaliyofanywa hospitalini hapo na serikali ya awamu ya sita, ikiwemo ya kuiekeza Bohari ya Dawa (MSD) kufunga vifaa tiba vya kisasa katika idara mbalimbali, ikiwemo idara ya magonjwa ya figo ambako kumefungwa mashine 10 za kusafisha damu.
Daktari Bingwa wa Huduma za Ndani katika Hospitali ya Rufaa mkoa wa Tumbi Dk. Adam Gembe, ambaye pia anasimamia Kitengo cha huduma ya kusafisha damu amesema kwa sasa wamepata vifaa tiba vya kisasa kutoka Bohari ya Dawa na miongoni mwa vifaa hivyo kuna mashine 10 za kusafisha damu.
“Tunaishukuru MSD, kwa kutuletea mashine za kuchuja damu lakini tunaiomba kuendelea kuboresha huduma ya upatikanaji wa vitendanishi na vifaa tiba, vitakavyotusaidia kutoa huduma bila kukwama na kwa wakati,” alisema.
Kwa upande wake Afisa Huduma kwa Wateja MSD Kanda ya Dar es Salaam Diana Kimario alitoa rai kwa hospitali kujenga tamaduni za kuwasilisha maombi ya dawa na vifaa tiba mapema kabla kuisha, ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma stahiki kwa wakati.
No comments:
Post a Comment