Na Mwandishi Wetu
WIZARA ya Utamaduni, Sanaa na Michezo imeibuka kidedea katika mchezo wa Karata kwa wanaume kwa mchezaji wao Sudi Juma kutwaa ubingwa wa Mashindano ya Shirikisho la Michezo ya Wizara, Idara za Serikali, Wakala na Mikoa (SHIMIWI) 2022 katika mchezo huo.
Akizungumzia ushindi wake mara baada ya kutangazwa matokeo ya mchezo huo Oktoba 11, 2022, bingwa huyo Sudi ameishukuru Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa kujali na kusimamia michezo ndani ya Wizara na kitaifa na amesema usindi huo ni wa watumishi wote wa Wizara hiyo na kwamba amepata ushindi huo kwa mara ya kwanza tangu aanze kushiriki mashindano ya SHIMIWI.
Nafasi ya pili katika mchezo huo imekwenda kwa Stephano Mjema kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii ambaye ametetea nafasi yake ambayo ameishika kwa miaka miwili mfululizo 2021 na 2022 huku nafasi ya tatu imekwenda kwa Anyamisye Chengula kutoka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU).
Kwa upande wa wanawake, bingwa wa mchezo huo ni Nyamzala Lupeja kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afriki Mashariki, nafasi ya pili imekwenda kwa Wandema Msumbuka kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi wakati nafasi ya tatu imekwenda kwa Sophia Mpema kutoka Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).
Wakati huo huo, katika mchezo wa netiboli, mabingwa watetezi ambao ni timu ya Ofisi ya Rais Ikulu wamefuzu kibabe kwenda hatua ya nusu fainali baada ya kuwafunga bila huruma Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa magoli 85-13 katika mchezo wa robo fainali uliorindima kwenye uwanja wa Bandari jijnini Tanga.
Katika mchezo mwingine Hazina wamewafunga Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi (Sekta ya Uchukuzi) kwa magoli 42-35; Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi wamewachapa Ofisi ya Bunge kwa magoli 55-29 huku Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) wamewapigisha kwata timu ya Wizara ya Ulinzi na Jeshi laKujenga Taifa kwa kuwafunga magoli 43-24.
Katika.mchezo wa soka, timu ya Wizara ya Ulinzi na Jeshi laKujenga Taifa imekuwa ya kwanza kufuzu hatua ya nusu fainali baada ya kuifunga Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa magoli 4-0 katika mchezo uliochezwa uwanja wa shule ya sekondari Galanos jijini humo.
Nayo timu ya Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi (Sekta ya Ujenzi) wamewafunga Wizara ya kilimo kwa jumla ya penati 8-7 katika mchezo uliofanyika uwanja wa TANROADS mizan jijini humo.
No comments:
Post a Comment