MSIMU wa mwaka huu wa korosho unaanza rasmi tarehe 14 Oktoba 2022 ukilenga uzalishaji wa tani 400,000 za zao hilo lengo ambalo Benki ya NMB imesema iko tayari na ina uwezo kifedha kuhakikisha linafanikiwa.
Katika kutimiza azma hiyo, jana benki hiyo ilibainisha utayari wake wa kufanya hivyo na kubainisha mikakati iliyonayo kulisaidia taifa kupata matokeo chanya kwenye msimu huu wa 2022/23.
Mbali ya mikopo na huduma zake nyingine, NMB inapanga kutumia kampeni maalumu ya kuhamasisha matumizi ya benki kuufanya msimu huu mpya kuwa wa mafanikio makubwa zaidi kiuzalishaji na kibiashara ikilinganishwa na msimu iliyopita.
Mkuu wa Idara ya Kilimo Biashara wa benki hiyo, Bw. Isaac Masusu, amezindua kampeni ya “Bonge la Mpango - Mchongo wa Kusini” na mchakato mzima unawalenga wakulima wa korosho na vyama vya ushirika (AMCOS) kwenye Kongamano na Viongozi wa Vyama vya Ushirika Mkoani Mtwara ililoliandaa kwa ajili ya kubadilishana mawazo jinsi ya kuufanikisha msimu huu na wadau wa zao hilo.
Bw Masusu alisema pia kongamano hilo limefanyika kwa kutambua ambavyo kilimo cha korosho kimekuwa nguzo muhimu kwa ustawi wa Kanda ya Kusini hususani mikoa ya Lindi na Mtwara lakini pia kwa taifa na hata Benki ya NMB.
Aidha, alisema kuwa wakulima watakaotumia NMB kufanya malipo ya mauzo yao wataziwezesha AMCOS zao kushinda zawadi zilizotengwa kwa ajili ya kampeni hiyo ambayo zawadi zake ni pikipikitano watakazozipata washindi kwenye droo zitakazofanyika kila baada ya wiki mbili.
Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Kanali Ahmed Abbas Ahmed, alisema kampeni hiyo itasaidia sana kubadilisha maisha ya watu wengi na kutoa mchango mkubwa kwenye uchumi wa korosho wa Mkoa wa Mtwara inaendana na juhudi za serikali za kurasimisha miamala na kuongeza matumizi ya mifumo ya kibenki, vitu ambavyo ni muhimu kwenye utekelezaji wa agenda ya taifa ya kuendeleza huduma jumuishi za kifedha nchini.
Droo yake ya kwanza itafanyika October 28 mwaka huu. Mbali na kuwahamasisha wakulima kuitumia zaidi benki ya NMB kufanya miamala, sababu nyingine za kampeni hiyo ni kuhamasisha amana na kuwasaidia watu kuweka akiba.
No comments:
Post a Comment