TANZANIA YAHAMASISHA WAWEKEZAJI SEKTA YA TEHAMA ILI KUKUZA UCHUMI - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Thursday, 20 October 2022

TANZANIA YAHAMASISHA WAWEKEZAJI SEKTA YA TEHAMA ILI KUKUZA UCHUMI

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax amakizungumza wakati wa mkutano kati yake na Rais wa Kampuni ya Kimataifa ya ASSECO ya Poland inayojishughulisha na masuala ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano, Dkt. Adam Goral. Wakati wa Mkutano huo Kampuni ya ASSECO ilieleza nia yake  ya kuja nchini kuwekeza.

WAZIRI wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax amesema Serikali ya Tanzania itaendelea kutumia fursa mbalimbali zilizopo nchini ikiwemo Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) ili kunufaika kiuchumi kupitia sekta hiyo. 

Waziri Dkt. Tax amesema hayo alipokutana kwa mazungumzo na Rais wa Kampuni ya Kimataifa ya ASSECO  ya Poland Bw. Adam Goral, inayojishughulisha na masuala ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano yenye nia ya kuwekeza nchini.

Akizungumza na Rais huyo, Mhe. Dkt. Tax amemweleza nia ya Serikali ya Tanzania ya kutaka kujiimarisha kwenye masuala ya Teknolojia ya Habari  na Mawasiliano (TEHAMA) ili kupitia teknolojia hiyo nchi iweze kunufaika kiuchumi.

Mhe. Waziri amesema kuwa,  katika ulimwengu wa sasa mifumo mingi ya utendaji imebadilika ambapo kazi nyingi  hukamilishwa kwa kutumia vifaa vya kisasa kama simu, kompyuta na mtandao. Hivyo unahitajika uwekezaji wenye tija hususan kwenye eneo la usalama wa taarifa  za watumiaji.

Ameongeza kuwa matumizi ya tehama nchini yameendelea kukua  siku hadi siku ambapo taasisi mbalimbali zikiwemo za Serikali, za Fedha, Shule, Hospitali na nyingine hutegemea teknolojia ya uhakika na salama ili kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi na tija. 

Amesema mbali na mchango mkubwa wa tehama katika ukuaji wa uchumi nchini pia imeendelea kuchangia uzalishaji wa ajira kwa watanzania hususan vijana.

"Tanzania inayo nia ya dhati ya  kuwa miongoni mwa nchi zinazoongoza na kunufaika kiuchumi kupitia matumizi  ya tehama. Hata hivyo jambo muhimu katika teknolojia hii ni usalama wa taarifa katika matumizi ya teknolojia hiyo. Hivyo, tungependa wawekezaji kulipa kipaumbele suala hili pale wanapokuja kuwekeza”, alisema Dkt. Tax.

Aidha, Mhe. Dkt tax ameahidi kuiunganisha taasisi hiyo na mamlaka husika nchini, ikiwemo Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kuhusu nia yao ya kutaka kuwekeza nchini ili mazungumzo yaanze.

Kwa upande wake Rais wa Kampuni hiyo Bw. Goral amemshukuru Mhe. Waziri kwa kutembelea Kampuni hiyo na kusema kampuni yake inatengeneza software zake yenyewe na kuongoza kwa teknolojia kwa upande wa Ulaya mashariki ina nia ya dhati ya kuwekeza  nchini na ipo tayari kushirikiana na Serikali katika kuboresha mifumo mbalimbali ya tehama.

“Kampuni yetu ina nia ya dhati ya kuwekeza Tanzania na usalama wa matumizi ya mtandao ni kipaumbele chetu. Tayari tunayoo Program maalum ilianza mwaka 2020 inayoshughulikia usalama wa mitandao. Tupo tayari kubadilishana uzoefu na ujuzi na Tanzania” alisema Bw. Goral

Awali akitoa mada kwenye mkutano huo kuhusu hali ya matumizi ya teknolojia ya habari nchini,  Mtaalam wa Tehama kutoka Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Brigedia Generali Mbaraka Mkeremy amesema  Tanzania imepiga hatua katika matumizi ya tehama ambapo kwa mujibu wa taarifa kutoka Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari hadi sasa watanzania wanaomiliki simu ni milioni 28 na muamala ya simu imeingiza mapato ya zaidi Shilingi Trilion 20 kwa mwaka 2021 pekee.

Kampuni ya Asseco  iliyoanzishwa mwaka 1991 hutoa mafunzo na ushauri kuhusu masuala ya tehama na kutengeneza software zake yenyewe. Tayari imewekeza katika Mabara sita na nchi 60 ulimwenguni zikiwemo Ethiopia, Nigeria, Togo na Botswana kwa upande wa Bara la Afrika.

Mhe. Dkt. Tax alikuwa nchini Poland kwa ziara ya kikazi ya siku tatu ambapo pamoja na mambo mengine alitumia ziara hiyo kukutana na wadau mbalimbali wakiwemo wawekezaji na wafanyabiashara kwa lengo la kuhamasisha uwekezaji nchini.

No comments:

Post a Comment