DPP AKABIDHI MALI ZA BILIONI 4.4 ZILIZOTAIFISHWA KWA SERIKALI - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Tuesday, 4 October 2022

DPP AKABIDHI MALI ZA BILIONI 4.4 ZILIZOTAIFISHWA KWA SERIKALI

Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Emmanuel Tutuba (wapili kushoto) na Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP), Bw. Sylvester Mwakitalu (wapili kushoto), wakisaini hati za makabidhiano ya mali 8188 zilizotaifishwa na Serikali katika hafla iliyofanyika jijini Dodoma.

Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Emmanuel Tutuba na Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP), Bw. Sylvester Mwakitalu, wakibadilishana hati za makabidhiano ya mali 8188 zilizotaifishwa na Serikali baada ya kuzisaini katika hafla iliyofanyika jijini Dodoma.

Ofisi ya Mkurungenzi wa Mashtaka nchini imekabidhi mali mbalimbali 8188 zenye thamani ya shilingi bilioni 4.4 zilizotaifishwa na Serikali kwa Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango.

Makabidhiano ya mali hizo yamefanyika jijini Dodoma kati ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Emmanuel Tutuba na Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP), Bw. Sylvester Mwakitalu.

Akizungumza katika hafla hiyo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Emmanuel Tutuba alisema kuwa makabidhiano hayo ni kwa mujibu wa Sheria ya Muenendo wa Makosa ya Jinai ambayo inaelekeza utaratibu wa mali zilizotaifishwa ziweze kukabidhiwa kwa Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango ambaye ni Msimamizi wa mali zote za Serikali.

Alisema baada ya makabidhiano hayo wizara hufanya uchambuzi wa mali hizo kuaona zile zinazofaa kwa matumizi ya Serikali na kuzigawa katika taasisi mbalimbali, na kama hazifai kwa matumizi ya Serikali zitafanyiwa utaratibu mwingine ikiwemo kuzipiga mnada.

“Ni wahakikishie kuwa mali hizi zote tulizopokea tutahakikisha tunazigawa kwa matumizi yanayuostahili kwa taasisi mbalimbali za Serikali na ambazo zitaonekana hazifai kwa matumizi ya Serikali tutazitafutia utaratibu maalum wa kuziondosha ikiwemo kuzipiga mnada ili hata fedha zitakazopatikana ziingie katika mfuko mkuu wa Serikali kama utaratibu wa kawaida,” alifafanua Bw. Tutuba.

Aidha, alitoa wito kwa Wananchi wasijiingize katika vitendo vya kihalifu kwa kuwa vitahatarisha maisha yao na pia mali zao na kuwataka kuendelea kuzingatia sheria, taratibu, kanuni na miongozo mbalimbali ya nchi katika shughuli zao ili wapate vipato halali.

Bw. Tutuba aliongeza kuwa Serikali haipendi kutaifisha mali za watu ila mtu atakapojiingiza katika vitendo vya kihalifu basi Sheria itafuata mkondo wake.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP), Bw. Sylvester Mwakitalu alisema mali hizo zimekusanywa katika maeneo mbalimbali nchini  kutoka kwa wahalifu ambao walizitumia kufanya uhalifu au walizipata kupitia uhalifu huo.

Alisema kwa mujibu wa sheria za nchi mhalifu haruhusiwi kunufaika na mali alizozipata kihalifu kwa kuwa mali hizo wakiendelea kubaki nazo zitatumika kufadhili uhalifu mwingine au kuhamasisha watu wengine kufanya uhalifu.

Naye Mkurugenzi wa Idara ya Usimamizi wa Mali za Serikali, Bw. Chotto Sendo alizitaja mali zilizokabidhiwa kuwa ni nyumba 19, viwanja tisa, mashamba  mawili, magari 31, mitambo – matrekta 23, pikipiki tisa, vifaa vya kielekroniki 38, mbao 5,843, mafuta ya ndege/taa lita 109, mashine ya kukoboa mpunga moja na maditi bati 2,104.

No comments:

Post a Comment