Na Fredy Mgunda, Iringa
WAZIRI wa maji Juma Aweso amewapongeza uongozi wa wilaya ya Iringa kwa kusimamia vizuri ujenzi wa bwawa la kuhifadhia maji ya mvua katika bodi ya maji bonde la Rufiji kwa kuwa litafanikisha kuleta maendeleo kwa wananchi na kutatua changamoto ya maji kwa wananchi wa kata ya Masaka.
Akiwa katika ziara ya kiazi mkoa wa Iringa waziri Aweso alisema kuwa ameridhishwa na ujenzi wa mradi wa bwawa la kuhifadhia maji ya mvua katika Kijiji cha Sadan kwa kuwa mmoja ya miradi mingi mikubwa ambayo itakuja kuwa na matokeo ya moja kwa moja kwa wananchi wanaolizunguka bwawa hilo.
Aweso alisema kuwa serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan imeigiza wizara ya maji kuhakikisha inachimba mabwawa ya kila wilaya ili kutatua changamoto hiyo na kuongeza njia za kukuza uchumi wa maeneo husika.
Alisema kuwa kukamilika kwa bwawa hilo kutaisaidia kuleta maendeleo ya miradi mingine ya maji kutokana na usimamizi mzuri ambao unafanywa na uongozi wa wilaya na mkoa kwa ujumla kwenye maendeleo ya miradi ya kijamii.
Alisema mradi huo wa ujenzi wa bwawa la kuhifadhia maji ya mvua utagharimu kiasi kikubwa cha fedha ambacho ni 900,982,000/= ambazo Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan amezileta kutatua changamoto hizo kwa wananchi wa kata ya Masaka.
Akijibu maombi ya mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Iringa Stephen Mhapa na diwani wa Masaka Methew Nganyagwa alisema kuwa wanayafanyia kazi maombi yao na tayari suala la kuchimba bwawa la kuhifadhia maji ya mvua katika Kijiji cha Magubike lipo kwenye mpango wa fedha za mwaka huu na ombi la matank ya maji wataletewa mapema iwezekavyo.
Awali akisoma taarifa ya mradi kwa waziri,msimamizi wa mradi huo Eng Geofrey Simkonda alisema kuwa mradi wa ujenzi wa bwawa la kuhifadhia maji ya mvua ni mkakati wa uendelezaji,utumiaji,uhifadhi na usimamizi wa vyanzo vya maji katika bonde la Rufiji.
Alisema kuwa lengo la ujenzi wa mradi huo wa ujenzi wa bwawa la kuhifadhia maji ya mvua ni kuvunia maji na kurahisiha upatikanaji wa maji kwa wananchi hususani wenye uhaba wa rasilimali za maji kwa ajili ya matumizi mbalimbali ya kibinadamu.
Eng Simkonda alisema kuwa wananchi wa wilaya ya Iringa, Kata ya Masaka inayojumuisha Vijiji vya Makota, Sadan na Kaning'ombe watanufaika na mradi huo.
Alisema kuwa bwawa la kuhifadhia maji ya mvua la Masaka lina kimo cha mita 14,urefu mita 260 na litakuwa na ujazo wa mita 439,803 na ujenzi unatarajiwa kukamilika mwezi wa tisa mwaka 2022 hadi sasa mradi umefikia asilimia 50.
Kwa upande wake mkuu wa wilaya ya Iringa Mohamed Hassan Moyo alisema kuwa anamshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha nyingi kwa ajili ya mradi huo ambao kwa kiasi kikubwa utatua kero za wananchi pamoja na kuleta maendeleo kwa wananchi.
Alisema kuwa kukamilika kwa ujenzi wa bwawa la kuhifadhia maji ya mvua katika Kijiji cha Sadan kutachochea maendeleo ya wananchi kiuchumi kwa shughuli ambazo zitakuwa zinafanywa katika eneo hilo.
Naye diwani wa kata ya Masaka Methew Nganyagwa alisema kuwa mradi huo utawanufaisha zaidi ya wananchi 7000 kwa shughuli mbalimbali za wananchi ambazo watakuwa wanazifanya kwenye mradi huo wa bwawa.
Nganyagwa alisema kukamilika kwa bwawa hilo licha ya kuondisha changamoto ya miaka mingi ya ukosefu wa maji Safi na salama, pia kutafungua na kuchochea fursa ya ukuaji wa kiuchumi kupitia fursa ya Kilimo cha umwagiliaji, Uhakika wa maji kwa ajili ya mifugo pamoja na shughuli za uvuvi na biashara ya samaki katika Vijiji vinavyozunguka kata hiyo.
Nganyagwa akizungumza kwa niaba ya Wananchi wa kata ya Masaka alisema Rais Samia Suluhu Hassan ameonesha kwa vitendo dhamira ya kumtua mama ndoo kichwani kwa kuwakumbuka wakina mama na wananchi masikini waliopo vijijini kwa kuwasogezea miradi mbalimbali hivyo ahadi ya wananchi ni kuendelea kumuunga mkono na kumuombea ili kufanikisha malengo ya maendeleo kupitia Serikali yake ya awamu ya sita.
No comments:
Post a Comment