Na Fredy Mgunda, Iringa
KAMISHINA Msaidizi wa Hifadhi ya Taifa (RUNAPA), Godwell Ole Meng’ataki amesema kuimarishwa
kwa ushirikiano baina ya Sekta ya Utalii na vyombo vya habari nchini kutachochea
ongezeko zaidi la watalii wa ndani na
nje ya nchi hatua itakayosaidi kukuza pato la Taifa na uboreshwaji wa huduma kwa
wananchi.
Akizungumza wakati wa ziara ya waandishi wa
habari wa mkoani Iringa (Iringa Journalists Ruaha the Royal Tour) ambapo
waandishi wapatao 40 waliotembelea hifadhi ya Taifa Ruaha, Kamishina Msaidizi Meng’ataki
alisema kuwa mategemeo yake kuwa ziara ya namna hiyo italeta tija katika sekta
ya utalii kwa kuufahamisha umma kuhusu umuhimu wa kutembelea vivutio vilivyopo
katika hifadhi mbalimbali nchini na manufaa yake ikiwemo yale ya kiuchumi kwa
taifa.
Alisema kuwa ziara hiyo ya wanahabari iwe
chachu ya kuimarisha ushirikiano baina wahifadhi na wanahabari kwa lengo la
kuibua mkakati wa pamoja katika kutangaza vivutio vilivyopo katika hifadhi za
nchini Tanzania hususani vinavyopatikana katika hifadhi ya Taifa ya Ruaha
ambayo ni hifadhi ya pili kwa ukubwa katika ukanda wa afrika.
Katika mazungumzo yake na Wataalii hao ambao ni
wanahabari wa mkoani humo Kamishina msaidizi wa hifadhi ya taifa (RUNAPA), Godwell Ole
Meng’ataki alibainisha kuwa wageni wanaotembelea hifadhi ya Ruaha upata fursa
ya kujionea baadhi ya vivutio vya Kipekee ikiwemo Simba wanaishi kifamilia, wanyama
wengine wa aina mbalimbali, utalii wa Ndege zaidi ya aina 574, na Zaidi ya aina 1650 za
mimea inayopatikana
katika hifadhi hiyo pekee.
Kamishina Meng’ataki alisema katika hifadhi ya
Ruaha kuna aina mbalimbali za utalii ukiwemo utalii wa kutembea kwa miguu,
utalii wa usiku, utalii wa boti na utalii wa uvuvi wa samaki huku akisisitiza kuwa
aina hizo za utalii wa kipekee zikitangazwa kikamilifu zitachochea ongezeko la
watalii katika hifadhi hiyo.
Alisema kuwa hifadhi ya Taifa Ruaha ni hifadhi
yenye ualisia wake tofauti na hifadhi nyingine jambo ambalo linavutia watalii
wengi kuitembelea.
Kiongozi huyo wa RUNAPA alizungumzia matokeo ya
Filamu ya Royal Tour iliyoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan ambayo aliitaja kuwa na mchango mkubwa katika
kuutangazia Ulimwengu juu ya vivutio vilivyopo nchini huku akimpongeza Rais kwa
kujitoa kwake katika kuchochea ukuaji wa sekta ya utalii wenye Tija.
Meng’ataki alisema kitendo kilichofanywa na Rais
kinapaswa kuungwa mkono na kila mtanzania kama walivyofanya wanahabari wa mkoani
Iringa walioungana na kufanya safari ya Utalii waliyoipa jina la Iringa Journalists
Ruaha The Royal Tour ikiwa ni hatua ya wazi ya kutambua mchango wa sekta ya
utalii nchini.
Kwa upande afisa Uhifadhi katika hifadhi hiyo, Amina Rashidi alisema kuwa hifadhi ya Taifa ya Ruaha (RUNAPA) kwa mwezi Julai mwaka 2022 ilipata watalii 2,232,ikiwa ni ongezeko la watalii 532 kutoka 1,700 walioitembelea kwa mwaka mzima wa 2021.
Amina alisema kuwa ongezeko hilo la watalii
limetokana na Royal Tour iliyosaidia kutangaza utalii nchini.
“Royal Tour imesaidia kutangaza hifadhi zetu, baada ya korona watalii wameanza kurudi kwa sababu watalii wa nje hawakuwepo, tulikuwa tunapata watalii wa ndani lakini sasa tunapata watalii wengi wa ndani na nje,” alisema Amina.
Alisema hifadhi imeanza kupokea watalii kwa
wingi, viwanja vya ndege vyote vinafanya kazi na mageti yana pilikapilika za
wageni wa ndani na nje.
Naye mwenyekiti wa waandishi wa habari mkoa wa Iringa Frank
Leonard alisema kuwa Waandishi wa habari Iringa wanatambua mchango wa utalii
katika maendeleo ya taifa
Leonard alisema kuwa lengo la waandishi
wa habari Iringa kutembelea hifadhi ya taifa ya Ruaha ni kuhakikisha
wanahamasisha sekta ya utalii hasa watalii wa ndani ili wahamasikie kutembelea
vivutio vya utalii vilivyopo hapa nchi.
Alisema kuwa waandishi wa
habari wanaushawishi mkubwa wa kuhakikisha wanawashawishi wananchi wengine
kwenda kutalii katika hafadhi ya Taifa ya Ruaha na hifadhi nyingine kupitia
vyombo vya habari ambavyo wanavifanyia kazi.
Leonard alimazia kwa kusema kuwa mkakati uliopo kwa waandishi wa habari wa mkoa wa Iringa ni Kahakikisha wanatembelea vivutio vyote vya utalii vya nyanda za juuu kusini ili kupata elimu na kuvijua vivutio hivyo kwa lengo la kuanza kuvitangaza vivutio na hifadhi zote za taifa.
No comments:
Post a Comment