TANESCO SINGIDA YASAKA MAONI YA WANANCHI KUHUSU NISHATI YA UMEME - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Tuesday, 26 July 2022

TANESCO SINGIDA YASAKA MAONI YA WANANCHI KUHUSU NISHATI YA UMEME

Meneja wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) Mkoa wa Singida, Mhandisi Florence Mwakasege akizungumza na Wananchi wa Kata ya Iguguno wilayani Mkalama  leo Julai 26, 2022  wakati akisikiliza mahitaji na ushauri wao kuhusu sekta ya nishati.

Afisa Mtendaji Kata ya Iguguno,  Josia Pangazi akizungumza kwenye mkutano huo. Kutoka kulia ni Meneja wa Tanesco Wilaya ya Mkalama, Mhandisi, Benedict Ryeimamu, Meneja wa Tanesco Mkoa wa Singida, Mhandisi, Florence Mwakasege na Mwenyekiti wa Kijiji cha Iguguno Kiula Solomon.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Iguguno, Kiula Solomon akizungumza kwenye mkutano huo.

Afisa Uhusiano na Huduma kwa Wateja wa Tanesco Mkoa wa Singida, Rehema Mwaipopo akizungumzia huduma mpya ya maombi ya kuunganishiwa umeme kwa njia ya mtandao  iitwayo NIKONEKT  ambayo inafanyika kwa kutumia simu ambapo muombaji anaomba akiwa nyumbani bila ya kufika ofisi za shirika hilo.

Mwenyekiti wa Kitongoji cha Iguguno Mashariki, Nicolaus Ernest akizungumza kwenye mkutano huo.

Mwananchi wa kata hiyo, Elisante Stephano akizungumzia changamoto ya gharama za kufungiwa umeme kuwa kubwa.

Wananchi wakiwa kwenye mkutano huo.

Mwananchi wa eneo hilo Modesta Masasi akiomba eneo wanaloishi kupelekewa umeme.

Mkutano ukiendelea.

Mkutano ukiendelea.
Wakina mama wakiwa kwenye mkutano huo.

Mama Amina Hamisi akichangia jambo kwenye mkutano huo.

Bibi Maria Makala ambaye alijaza fomu za kuomba kuingiziwa umeme kwa gharama ya Sh.27,000 lakini akuwekewa akilalamika baada ya ongezeko la zaidi ya Sh.300,000 la sasa la kufungiwa umeme kwenye nyumba yake.

Mzee Ernest Mkumbo mkazi wa Kitongoji cha Mwando akizungumzia eneo lake alilotenga kwa ajili ya makaburi kupitishwa nguzo za umeme lakini hadi leo hii bado hajalipwa fidia.

Na Dotto Mwaibale, Singida

SHIRIKA la Umeme Tanzania (TANESCO) Mkoa wa Singida limeanzisha utaratibu wa kusikiliza mahitaji na kupokea ushauri wa wananchi na kupokea maoni yao kuhusu sekta ya nishati ya umeme katika wilaya zote ili ziweze kufanyiwa kazi kwa kuwafuata katika maeneo yao.

Meneja wa Shirika hilo Mkoa wa Singida, Mhandisi Florence Mwakasege akizungumza leo Julai 26, 2022 na Wananchi wa Kata ya Iguguno wilayani Mkalama wakati akisikiliza mahitaji na ushauri wao kuhusu sekta ya nishati ya umeme alisema utaratibu huo ambao kwa mara ya kwanza umeanza kufanywa katika kata hiyo akiwa na mwezi mmoja na wiki mbili tu tangu afike mkoani hapa akitokea mkoani Ruvuma kuwa utakuwa endelevu.

“Utaratbu huu utafanyika katika kata na wilaya zote mkoani hapa na ninyi wana Iguguno mmekuwa wakwanza kusikilizwa hivyo tumekuja kuwasikiliza ili tutatue changamoto zenu na kupokea ushauri na maoni yenu  tuweze kuboresha huduma za shirika letu ziwe nzuri na kila mwananchi aweze kunufaika nazo,” alisema Mwakasege.

Alisema lengo kubwa la mkutano huo ni kuwasikiliza na kupokea ushauri wao na kama kutakuwa na maeneo yenye ukakasi waweze kuyachukua na kuyafanyia kazi ili kila mmoja aweze kutumia huduma hiyo kwa usalama ambayo licha ya kuwa nzuri lakini ikitumika vibaya ni inakuwa ni hatari.

Alisema wao kama wasimamizi wasipowaeleza madhara hayo itakuwa vigumu kuyajua ndio maana wameanzisha utaratibu huo wa kukutana nao ili kufahamishana mambo mbalimbali na kupokea maoni waliyonayo.

Mwakasege alitumia nafasi hiyo kuwashukuru viongozi wa kata hiyo kwa kuratibu mkutano huo pamoja na wananchi ambao walijitokeza kwa wingi na kueleza mahitaji yao mbalimbali.

Katika mkutano huo ambao ulifanyika katika viwanja vya ofisi ya mtendaji wa kata hiyo miongoni mwa mambo yaliyojitokeza kutoka kwa wananchi ni kuomba kupelekewa umeme katika maeneo ambayo hayana huduma hiyo , kupunguziwa gharama za kufungiwa umeme kutoka Sh.27,000 hadi zaidi ya Sh.300,000 ambayo wengi wao hawezi kuimudu.

Katika hatua nyingine wananchi hao walilipongeza shirika hilo Mkoa wa Singida kwa kuanzisha utaratibu wa kwenda kusikiliza mahitaji na ushauri wao na kwa kipekee wakimpongeza Meneja Mwakasege kwa kuanzisha utaratibu huo na kueleza shirika hilo jimejipanga kufanya kazi kwa spidi anayoitaka Rais Samia Suluhu Hassan ya kufanya kazi kwa bidii ili kuwatumikia wananchi.

Wananchi hao walimuambia Meneja wa shirika hilo Mkoa wa Singida, Mhandisi Mwakasege kuwa kutokana na mji wao kuwa mkubwa wapo tayari kutoa eneo la kujenga ofisi ya Tanesco ili waachane na kupanga na wanachotakiwa kukifanya ni kuandika barua ya maombi ya kuomba eneo hilo na kuipeleka ofisi ya kijiji.

Aidha katika mkutano huo Afisa Uhusiano na Huduma kwa Wateja wa Tanesco Mkoa wa Singida, Rehema Mwaipopo alielezea huduma mpya ya maombi ya kuunganishiwa umeme kwa njia ya mtandao  iitwayo NIKONEKT ambayo inafanyika kwa kutumia simu ambapo muombaji anaomba akiwa nyumbani bila ya kufika ofisi za shirika hilo.

No comments:

Post a Comment