Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akizungumza na wananchi wa Iramba, baada ya kuweka jiwe la msingi la mradi wa kituo cha Afya cha Mtoa, kilichopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Iramba Mkoani Singida. (Picha na ofisi ya Waziri Mkuu)
Na Dotto Mwaibale, Iramba
WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa, amesema Serikali haizuii kuchangia maendeleo
ya shule bali inakataza michango ya ovyo ovyo kwa wanafunzi isiyo na tija.
Akizungumza jana na wananchi wa Kata ya Mtoa wilayani Iramba baada ya
kuweka jiwe la msingi ujenzi wa kituo cha afya Mtoa katika mwendelezo wa ziara
yake mkoani Singida, alisema serikali inaruhusu michango inayokubalika.
"Hatuzuii kuchangia maendeleo ya shule tuanchokataza ni ile michango
kwa mfano Mwalimu anamwagiza mwanafunzi alete Sh.500 ambayo haijapitishwa na
kamati za shule au na wazazi," alisema.
Majaliwa alisema Serikali imeondoa ada kwa wanafunzi kuanzia shule ya
msingi hadi kidato cha sita ili kuruhusu wanafunzi wengi wapate fursa ya kupata
elimu.
"Nawagiza wazazi pelekeni watoto shule sasa hakuna kisingizio cha
kukosa ada, michango inaweza ikawepo kwa ajili ya 'kusapoti' maendeleo ya eneo
husika lakini kwa makubaliano," alisema.
Akizungumzia kuhusu maji, aliziagiza Kamati za Maji kusimamia na kulinda
vyanzo vya maji na mazingira visiharibiwe.
Waziri Mkuu alisema vyanzo vya maji vimekuwa vikiharibiwa kwa baadhi ya
wananchi kuingiza mifugo.
Majaliwa alisema Serikali inatumia gharama kubwa katika kutekeleza miradi
ya maji kwasababu vyanzo vya maji vimekuwa vikiharibiwa kwa kuchungua mifugo.
Alisema katika mwaka huu wa fedha Serikali itatoa Sh. 5.1 bilioni kwa ajili
ya utekelezaji wa miradi ya maji katika jimbo la Iramba Magharibi na Sh.550
milioni zimeletwa kwa ajili ya kufanya utafiti wa wapi maji yatapatikana.
Naye Naibu Waziri Ofisi ya Rais,Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa
(TAMISEMI), Festo Dugange alisema serikali imepanga kununua magari 195 ya
kubebea wagonjwa katika mwaka huu wa
fedha wa 2022/2023 ambayo yatagawanywa kwenye wilaya ili kukabiliana na
changamoto wanayopata wagonjwa.
Alisema kati ya magari hayo
Halmashauri ya Wilaya ya Iramba itapewa magari mawili.
Alisema katika sekta ya afya, Serikali imetoa fedha nyingi katika Wilaya ya
Iramba ambazo ni pamoja na Sh.2.8 bilioni kwa ajili ya ujenzi wa vituo sita vya
afya na Sh.550 milioni kuboresha Hospitali ya Wilaya ya Kiomboi.
Alisema Serikali pia imetoa Sh.300 milioni kwa ajili ya ujenzi wa zahanati
sita katika jimbo la Iramba Magharibi na watumishi wapya 25 wa afya
walioajiriwa hivi karibuni wameletwa katika Wilaya ya Iramba.
Katika sekta ya elimu, alisema serikali imetoa Sh.3.6 bilioni katika Halmashauri ya Wilaya ya
Iramba ambazo zimetumika kujenga madarasa katika shule za sekondari na msingi
ambapo pia zimetolewa Sh.940 milioni kwa ajili ya ujenzi wa shule mbili mpya za
sekondari.
Aisha, katika sekta ya barabara katika mwaka wa fedha uliopita Serikali ilitoa Sh.7.3 bilioni kwa ajili hiyo na mwaka huu zimetengwa Sh.5.6 bilioni kwa ajili kujenga kilometa 2.5 za lami mjini Kiomboi.
No comments:
Post a Comment