Na Frida Manga
SHIRIKA la Kimataifa la Kutetea Uhai Kanda ya Afrika Mashariki “Human Life International (HLI) limewashilisha kwa Sipika wa Bunge la Jumuiya ya Afrika Mashariki (EALA) Martin Ngoga, hoja za kupinga kupitishwa Muswada wa Ujinsia na Afya ya Kizazi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki 2021.
Hoja hizo zimewasilishwa kwa Katibu Muhutasi wa Sipika wa EALA jijini Arusha, Priscilla Amoding na Mkurugenzi wa (HLI) Kanda ya Afrika Mashariki kwa Nchi zinazozungumza Lugha ya Kingereza Emil Hagamu, Mkurugenzi wa (HLI) Uganda Padri Jonathan Opio, Mshirikishi wa Kamati ya Utetezi wa Uhai kutoka Jukwaa la Wanataaluma Wakristo kutoka Kenya Agustine Richard Kakeeto na Mratibu wa Vijana kutoka jukwaa la Pro-Life na Pro- Family kutoka Kenya, Tobias Nauruki.
Akizungumza mara baada ya kupokea hoja hizo Katibu Muhutasi Priscilla Amoding alisema yapo Mashirika mengine ambayo yamewasilisha hoja za kupinga mswada huo kwa Spika kuonyesha unakiuka heshima, haki ya kuishi, utu na mila na desturi njema za Watu wa Afrika Mashariki.
Kwa mujibu wa Amoding hoja zote zimepokelewa na zitawasilishwa kwa Kamati ya Malengo ya Jumla (Committee on General Purpose) ya Bunge la Jumuiya ya Afrika Mashariki ambayo ndiyo inaratibu masuala hayo, nazo zitajadiliwa wakati Wabunge watakapoanza kujadili Muswada huo.
Akizungumza mara baada ya kupokelewa kwa hoja hizo, Mkurugenzi wa HLI kutoka Uganda Padri Jonathan Opio ameeleza furaha yake kwa hatua iliyofikiwa ya kuwasilisha hoja ya kupinga kupitishwa kwa Muswaada huo ambao ni hatari kwa maisha ya watu wa Afrika.
Padri Opio alisema hatua hiyo ni ya kupongezwa kwa upande wao kwani wamefanikiwa kuonyesha juhudi zao katika kutunza, kulinda tamaduni na kulinda Uhai wa mwanadamu ambao ni zawadi ya Mungu, hivyo amewaalika watu wote na hasa Viongozi wa Dini kuendelea kushirikiana na kuwa tayari kupaza sauti kupinga juu ya Muswaada huo na sheria zozote ambazo zinakiuka haki za binadamu.
Kwa upande wake Mshirikishi wa Kamati ya Utetezi wa Uhai kutoka Jukwaa la Wanataaluma Wakristo kutoka Kenya Agustine Richard Kakeeto alisema jumla ya Taasisi 46 kutoka Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki zimeungana kuupinga Muswaada huo na jumla ya Saini 1124 za watu binafsi zimetiwa za kupinga Muswaada huo.
Kakeeto alisema wamemueleza Sipika wa Bunge la EALA juu ya madhara yatakayotokea kama Muswada huo utapitishwa kuwa sheria. Baadhi ya madhara mazito yanatokana na Muswada huo kunapingana haki ya kuishi, heshima na utu wa binadamu, kuvurugwa utashi, imani na mila na desturi za Watu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, huku akiwataka Wabunge wa EALA kutokukubali kushawishiwa na ajenda zinazotoka nje ambazo hazina teija na zinaharibu thamani ya Utu wa Watu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Mratibu wa Vijana kutoka Pro-life na Pro- Family Nchini Kenya Tobias Nauruki alisema Mataifa ya Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki yanahitaji Viongozi wazuri wa baadae ambao ni Vijana ambao wamejengwa katika misingi bora ya malezi, imani na thamani za kibinadamu. Hivyo wahahitaji kujengewa mazingira bora katika kukua kwao.
Miongoni mwa Vipengele ambavyo ni viovu katika Muswaada huo ni Kipengele kinachotaka ama Kinacholazimisha Nchi za Afrika Mashariki kufanya matumizi ya Vithibiti Mimba kuwa sehemu ya maisha yao bila kujali umri, Wala hali ya Ndoa na hasa kulazimisha matumizi yake kwa Watoto.
Hali kadhalika kipengele kinachotaka Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki kutunga Sheria za Kutoa Mimba amabyo kama itapishwa kuwa sheria, Wananchi wa Jumuia ya Afrika Mashariki watakuwa wameanza mradi wa kuangamiza kizazi cha baadaye. Pia kipengele kinacholazimisha Masomo ya Ngono ambayo yanaharibu ukuwaji wa Watoto na kuleta mmomonyoko wa maadili. Kipengele kingine kibaya ni kile cha Kuingilia Kati Uumbaji wa Binadamu kwa kuhamasisha matumizi ya Tekenolojia saidizi ili kupata uzao.
HLI, inaamini Wazazi ni Walezi na Walimu wa kwanza kwa watoto hivyo, kipengele kinachoondoa Mamlaka ya Wazazi katika Malezi ya Watoto ni kukiuka misingi ya Malezi bora na maadili
Mkurugenzi wa HLI Kanda ya Afrika kwa Nchi zinzozungumza Lugha ya Kingereza, Emil Hagamu anasema (HLI) anataka Muswada huo utupwe mbali na uandikwe mwingine wenye kukidhi mahitaji halisi ya Watu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki katika masuala ya ujinsia, utu na heshima yao pia unaoakisi maisha halisi ya kiuchumi, kijamii na kimaadili ya watu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki pia utambue tunu za Kiimani na za Watu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.
No comments:
Post a Comment