VIONGOZI EPUKENI MGONGANO WA MASLAHI MIRADI YA BARABARA...! - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Tuesday, 1 March 2022

VIONGOZI EPUKENI MGONGANO WA MASLAHI MIRADI YA BARABARA...!

 

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Joseph Mkirikiti akizungumza kwenye ufunguzi wa kikao cha Bodi ya Barabara jana mjini Sumbawanga ambapo amewataka wahandisi wa barabara kusimamia ujenzi wa barabara kwa ubora na viwango vilivyokusudiwa.

WABUNGE wa mkoa wa Rukwa wameshauri viongozi kujiepusha na mgongano wa maslahi kwa kutofanya kazi za ukandarasi wa miradi ya barabara ndani ya mkoa huo ili watendaji wapate nafasi ya kusimamia mradi hiyo kikamilifu

 Mbunge wa Sumbawanga mjini Aeshi Hilary alitoa wito kwa viongozi wenzake wakiwemo wabunge na viongozi wengine kujiepusha kuomba kazi za ujenzi wa barabara ndani ya mkoa wa Rukwa ili kuepusha mgongano wa maslahi hatua itakayosaidia usimamizi mzuri wa miradi hiyo.

Hayo yamebainishwa leo (28.02.2022) wakati wa kikao cha Bodi ya Barabara cha Mkoa wa Rukwa kilichofanyika katika ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa mjini Sumbawanga ambapo wametaka Wakala za TANROAD na TARURA kusimamia sheria.

“Nashauri sisi wabunge na viongozi wengine tukaombe kazi za barabara kwenye mikoa mingine ili turuhusu watendaji kuwa na usimamizi mzuri wa miradi hii” alisema Aeshi.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi Mkuu wa Rukwa Rainer Lukala alishauri uongozi wa mkoa huo kuwashirikisha wakandarasi kwenye vikao hivyo ili watoe michango yao kuboresha utekelezaji wa miradi.

Kuhusu suala la viongozi kuwa na kandarasi za miradi ya barabara , Lukala alisema muhimu ni kwa Mamlaka za usimamizi kuteua wakandarasi wenye sifa na uwezo wa kutekeleza kazi za barabara na tija ipatikane.

“Mimi pia ni mkandarasi hivyo tukisema leo tupitishe azimio kuwa viongozi tusifanye kazi za ukandarasi basi itakuwa vigumu kuendelea na majukumu mengine ya kichama au serikali. Nashauri suala hili lichunguzwe na wakandarasi wenye sifa wapewe.” alisema Lukala.

Akizungumza kwenye kikao hicho Mbunge wa Kalambo Josephat Kandege alisema hivi sasa kumekuwa na uvunjifu wa sheria ambapo Mifugo mingi inapitishwa kwenye barabara na kuzifanya zisidumu  na kuleta kero kwa wananchi.

“Tunashuhudia Mifugo ikipitishwa kwenye barabara zetu bila udhibiti toka kwenye Mamlaka zinazosimamia barabara. Hili haikubaliki. Nendeni mkasimamie sheria ili barabara zidumu” alisema Kandege.

Naye Mbunge wa Nkasi Kaskazini Aida Khenani alitaka mkoa uweke mpango mahususi wa kuweka taa za barabarani ikiwemo kwenye wilaya za Nkasi na Kalambo ili kuvutia miji na pia kukuza uchumi.

Aidha, Khenani alishauri mkoa kupitia Tarnroad na Tarura kuweka mikakati wa kuwa na wakandarasi wenye uwezo ili kazi za ujenzi wa miundombinu hiyio zilete tija.

Mhandisi wa TANROAD Mkoa wa Rukwa Mhandisi Mgeni Mwanga alisema katika mwaka huu wa fedha 2021/22 watakamilisha uwekaji taa za barabarani urefu wa kiliometa 1.5 kwenye mji wa Sumbawanga na fedha zaidi zikipatikana wataendelea kwenye wilaya za Nkasi na Kalambo.

No comments:

Post a Comment