TBA YATAKIWA KUWASILISHA MPANGO WA MATENGENEZO NYUMBA ZA SERIKALI - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Wednesday, 2 March 2022

TBA YATAKIWA KUWASILISHA MPANGO WA MATENGENEZO NYUMBA ZA SERIKALI

 

Muonekano wa Jengo  jipya la Bodi ya Usajili wa Wahandisi (ERB) , lililopo eneo la Medeli Jijini Dodoma. Jengo hilo linatarajiwa kutumika kwa ajili ya ofisi za makao makuu ya  Bodi pamoja na kituo cha kuendeleza kada ya Uhandisi nchini.

Muonekano wa Jengo la ofisi za Makao Makuu ya  Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) lililopo Jijini Dodoma.

Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi, (Sekta ya Ujenzi) Balozi Aisha Amour, akikagua moja ya jengo la Bodi ya Usajili Makandarasi (CRB), Jijini Dodoma ikiwa ni ziara yake ya siku moja ya kutembelea na kukagua majengo ya ofisi za taasisi zilizo chini ya Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi (Sekta ya Ujenzi).

Na Mwandishi Wetu

KATIBU Mkuu Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi (Sekta ya Ujenzi), Balozi Aisha Amour ameutaka uongozi wa Wakala wa Majengo Tanzania (TBA), kuwasilisha mpango wa matengenezo wa nyumba na majengo ya Serikali, ili kuhakikisha yanadumu kwa muda mrefu. 

Alitoa agizo hilo juzi wakati wa ziara ya kukagua ofisi za taasisi zilizopo chini ya Sekta ya Ujenzi ikiwa ni lengo la kuhakikisha wanahamia jijini Dodoma kabla ya mwaka wa fedha 2021/22 kukamilika.

Akiwa katika ukaguzi huo, Balozi Aisha aliwataka TBA kuhakikisha mpango kazi unaambatana na mkataba wa makubaliano kati yao na mpangaji wa nyumba na majengo ya Serikali, kwamba kumekuwa na tabia ya wapangaji kutumia nyumba na majengo hayo kinyume na makubaliano.

"Tunatakiwa kuhakikisha kuwa jambo hili tunaliweka wazi kabla ya mpangaji kuingia kwenye nyumba ili akiondoka aiache nyumba kwenye hali nzuri jambo ambalo litaokoa fedha za Serikali zinazotumika katika ukarabati wa mara kwa mara wa nyumba na majengo hayo" alisema Balozi Aisha.

Pamoja na mambo mengine, aliagiza mameneja wa mikoa wapewe jukumu la kukagua mali za serikali zinazomilikiwa na TBA ikiwamo viwanja na kuhakikisha vinakuwa katika hali nzuri wakati wote.

Aidha, aliitaka TBA kuhakikisha wanakamilisha kwa wakati ujenzi wa jengo la Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) lililopo jijini Dodoma.

Balozi Aisha alisema: "Hakikisheni mnatumia siku 144 mlizoomba kuongeazewa kukamilisha jengo hilo kwa ubora na viwango vinavyotakiwa ikiwa ni pamoja na kuwasilisha mpango kazi utakaobainisha mpangilio wa kazi katika siku hizo".

Pia, aliiagiza TBA kuhakikisha wanatumia utaalamu wao ipasavyo katika kuangalia njia mbadala ya kukabiliana na changamoto ya mfumo wa maji katika nyumba na majengo ya Serikali jijini Dodoma, kutokana na kuharibika mara kwa mara.

Wakiongea kwa nyakati tofauti wakuu hao wa taasisi walimhakikishia Balozi Aisha kuwa watahakikisha manejimenti na watumishi wote wa serikali wanahamia Dodoma kwa muda uliopangwa.

Ziara hiyo ya siku moja ilihusisha ukaguzi wa majengo ya ofisi katika taasisi za wizara ambazo ni Wakala wa Barabara (TANROADS), Wakala wa Majengo Tanzania (TBA), Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA), Bodi ya Usajili wa Wahandisi (ERB), Bodi ya Usajili wa  Makandarasi (CRB), Bodi ya Usajili wa Wasanifu Majengo na Wakadiriaji Majenzi (AQRB) Vikosi vya Ujenzi, pamoja na Baraza la Taifa la Ujenzi (NCC).

No comments:

Post a Comment