BENKI ya NMB imetangaza kuanza kuuzwa rasmi kwa hati fungani ya miaka mitatu inayomlenga mwekezaji yeyote aliye tayari kuwekeza katika taasisi hiyo kwa ajili ya kupata riba nzuri.
Kiwango cha chini cha uwekezaji kwenye hati fungani hii ni TZS 500,000 na itaweza kununuliwa kutoka kwenye tawi lolote la Benki ya NMB au kwa madalali wa hisa waliosajiliwa na Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA).
Hati fungani hii ya NMB Jasiri inategemea kukusanya kiasi cha Shilingi bilioni 25 kupitia mauzo ya dhamana hii, lakini ikiwa na kipengele cha kuongeza TZS bilioni 15 zaidi. Mapato ya Hati fungani hii ya NMB Jasiri yatatumika kusaidia utoaji wa mikopo kwa biashara na makampuni yanayomilikiwa au kusimamiwa na wanawake pamoja na biashara ambazo bidhaa na ama huduma zake zinamnufaisha mwanamke.
Hii ni hati fungani ya kipekee na ya kwanza kutolewa kwenye ukanda wa Afrika Mashariki mahsusi kwa ajili ya kuwawezesha wanawake kijamii na kiuchumi na inaendelea kuonyesha tu jinsi Benki ya NMB inavyoendelea kuunga mkono juhudi za kufikia Malengo Endelevu ya Umoja wa Mataifa (SDGs), hasa lengo endelevu namba 5 (SDG 5) linalohusu Usawa wa Kijinsia na lile la namba 10 (SDG 10) lililojikita katika kupunguza tofauti za kijinsia.
Wawekezaji kwenye hati fungani hii watapata riba ya asilimia 8.5 kwa mwaka itakayolipwa kila robo mwaka wakati wa kipindi chote cha miaka mitatu mpaka mwezi Machi mwaka 2025. Riba itakayolipwa itakatwa kodi ya zuio.
Aina hii ya hati fungani pia hutoa fursa kwa wawekezaji wadogo kuwekeza katika dhamana za (viwango vidogo) kiasi kidogo, kupanua wigo wa uwekezaji na kushiriki katika soko la hati fungani hivyo kuongeza ushirikishwaji kifedha na ufikiaji huduma unaostahili kwa kutumia mtandao wa benki yetu unaopatikana kirahisi.
Uuzaji wa Hati Fungani ya NMB Jasiri utaanza leo Februari 7, 2022, hadi Machi 21, 2022. Maombi yote ya kuinunua Hati fungani hii yatapita kwenye matawi yote 226 ya NMB au kwa madalali waliosajiliwa na Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA).
Karibuni tuwekeze!
No comments:
Post a Comment