Wanafunzi wa Shule Huria ya Brothers Academy wakijiandaa kwa ibada ya shukrani.
Na Mwandishi Wetu
“KAMA si shule huria, vijana wengi wakiwamo hawa wanaohitimu sasa, wangepotea na kuishia mitaani, lakini shule hizi zimesaidia vijana wengi waliokuwa wamenasa na sasa wana matumaini na wengine wamejiendeleza na wanalitumikia taifa kwa nafasi na nyadhifa mbalimbali.”
Amesema Mkurugenzi wa Shule Huria ya Brothers Academy, Robert Rwezaula, muda mfupi baada ya kufanyika ibada maalumu shuleni hapo, Ukonga –Banana, Dar es Salaam kumshukuru Mungu kwa kuwawezesha wanafunzi wa shule hiyo kufaulu mitihani yao ya kitaifa hali inayowawezesha kuendelea na masomo ya kidato cha tatu na tano.
Rwezaula alisema: “Hata ninapoona idadi kubwa ya vijana wakiwamo wasichana walioamua kurudi kutafuta fursa ya pili ya elimu na sasa wanahitimu, ninafurahi sana na ndio maana ninawaomba wazazi, waendelee kuwasaidia vijana kutafuta elimu zaidi hadi katika vyuo na vyuo vikuu.”
Katika ibada hiyo, Mchungaji wa Kanisa la Waadventisti Wasabato (SDA) Mtaa wa Karakata, Jimbo la Kusini Mashariki, Julius Oisso, ameungana na wanafunzi wanaosoma shuleni hapo kuishukuru na kuipongeza shule hiyo kwa kufufua matumaini ya vijana wengi yaliyokuwa yamepotea kielimu.
Amewapongeza wanafunzi kwa kutokatishwa tamaa na changamoto za awali na kwamba, ndio maana kupitia Brothers Academy, Mungu amejibu maombi yao.
“Wema wa Mungu umeonekana hapa Bbrothers Academy kupitia matokeo mazuri ya vijana katika mitihani yao ya QT; ametumia kituo hiki kuinua mianzi iliyopondeka na kuwasha taa zilizozimika,” alisema Mchungaji Oisso.
Wanafunzi Donatha Steven, John Kelvin, Joyce John na Haji Didas, walisema moja ya vichocheo vya kufaulu kwao vizuri katika ngazi mbalimbali shuleni hapo, ni namna walimu wanavyojituma kufuatilia, kubaini changamato na kumsaidia mwanafunzi moja mmoja kwa kadiri ya shida zake kielimu.
“Walimu hawana ubaguzi; wanafuatilia vipindi na uwezo wa kila mmoja,” alisema Joyce huku John aliyefaulu mtihani wa kujitegemea na sasa anajiandaa kwa mtihani wa taifa wa kidato cha sita akisema: “Juhudi za walimu zinatufikisha mtoni, sasa kunywa maji (kufaulu) ni matakwa na jitihada za kila mmoja kujua ametoka wapi na hapa alipo anatafuta nini.”
Kutokana na ufaulu huo mkubwa wa wanafunzi, Rwezaula amebainisha siri ya mafanikio hayo kuwa ni hasa walimu na wanafunzi kumtanguliza Mungu, upendo, nidhamu, ushirikiano pamoja na wanafunzi kujengwa katika kutambua lengu kuu la wao kuwapo shuleni hapo.
“Vijana wanapofika hapa kwanza wanajengwa kutambua changamoto zilizowakwamisha kuendelea na mfumo wa kawaida wa elimu na sasa watambue na kuzingatia sababu na lengo lao kuu kuwa hapa,” alisema Rwezaula.
No comments:
Post a Comment