Na Mwandishi Maalum, Las Vegas, Marekani
RAIS wa Jumuiya ya Uwindaji ya Kimataifa, (SCI), Sven Lindqueast ameitaja Tanzania kuwa ni nchi yenye nusu ya simba wote Duniani katika Mkutano wa 50 wa Mwaka wa Uwindaji wa Kitalii unaoendelea kufanyika nchini hapa.
Rais huyo Bw. Sven Lindquest amesema kwa hatua hiyo ameipongeza kwa juhudi za utunzaji na kupelekea wingi wa wanyama hao.
Kwa upande wake Serikali kupitia Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Damas Ndumbaro ametaja sababu zilizopelekea nchi ya Tanzania kutajwa kuwa nchi yenye Simba wengi Duniani licha ya kuruhusu uwindaji wa kitalii.
Akizungumza leo katika Jijini la Las Vegas nchini Marekani, Dkt.Ndumbaro amesema nusu ya simba wote wapo Tanzania kutokana na uimara wa serikali ya Tanzania katika shughuli za uhifadhi
Amesema kuimarika kwa shughuli za uhifadhi hususani kwa Wanyamapori walao nyasi ni moja ya sababu ya Tanzania kuwa na Simba wengi hivyo imepelekea Simba nao kuongezeka kutokana na uhakika wa chakula cha kutosha
Amefafanua kuwa Simba hula wanyamapori walao nyasi na wanyamapori hao walao nyasi wamekuwa wengi kutokana na uwepo wa nyasi za kutosha kutokana na usimamizi bora wa maeneo ya Hifadhi
"Kubadilishwa mfumo kutoka wa kirai kwenda katika mfumo wa kijeshi kwa Watumishi wote wanaosimamia maeneo ya Hifadhi ni moja ya sababu ya simba kuongezeka kwa Simba nchini Tanzania," alisema Dkt. Ndumbaro.
Waziri Ndumbaro amesisitiza kuwa Tanzania imefanikiwa kuwa simba wengi kutokana na serikali kuwa mstari wa mbele katika kuimarisha shughuli za uhifadhi nchini kwa kuitengea Wizara ya Maliasili na Utalii bajeti ya kutosha inayotumika katika kuendesha operesheni mbalimbali za kukabiliana na ujangili.
Amesema hadi sasa Serikali imeweza kufanikiwa kukomesha tatizo hilo la ujangili kwa zaidi ya asilimia 90 na kusisitiza kuwa ifikapo 2025 itarajia kumaliza kabisa tatizo la ujangili kwa kufikia asilimia 100%.
" Uthubutu wa Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan wa kuwa bega kwa bega na Wizara imekuwa chachu kwa Tanzania kuzidi kuongoza kwa kuwa na simba wengi Duniani," amesisitiza Dkt. Ndumbaro.
Pia, Dkt. Ndumbaro ameitaja sababu nyingine kuwa ni utolewaji wa elimu kwa Jamii, amesema kwa sasa Jamii imetambua umuhimu wa wanyamapori hivyo wananchi wamekuwa wakitoa ushirikiano kwa Serikali kwa kutoa taarifa vitendo vya ujangili vinapotokea.
"Kama nchi tumejiwekea utaratibu wa kuhakikisha wananchi wote wanaoishi katika maeneo ya Hifadhi wananufaika kwa kusogezewa huduma za kijamii, hivyo Jamii imekuwa inaona faida ya moja kwa moja ya uwepo wa wanyamapori," alisisitiza Dkt. Ndumbaro.
Katika hatua nyingine, Dkt. Ndumbaro amesema uwepo wa sheria kali ya kutokuruhusu shughuli za kibinadamu kuendeshwa ndani ya maeneo ya Hifadhi kumepelekea maeneo ya Hifadhi kubaki katika uasili wake hivyo simba wamezidi kuongezeka kutokana uwepo mazingira salama ya wanyamapori wengine.
Aidha, Dkt. Damas Ndumbaro amesema licha ya Tanzania kuwa na vitalu vya uwindaji wa kitalii zaidi ya 100 lakini imekuwa ikiendesha Uwindaji huo kwa kuzingatia matumizi endelevu ndio maana imezidi kuongoza Duniani kwa kuwa na simba wengi.
Kufuatia hali hiyo, Dkt. Ndumbaro amekanusha madai ya baadhi ya nchi zinazopinga Uwindaji wa Kitalii kwa kisingizio kuwa utalii huo umekuwa ukipunguza idadi ya wanyamapori ambapo amesisitiza kuwa Uwindaji wa Kitalii ni muhimu kwa kuwa umekuwa ukisaidia kupunguza idadi ya wanyamapori waliozidi ili kupunguza athari kwa binadamu.
Amesema kwa sasa nchini Tanzania kumekuw athari kwa binadamu kutokana na ongezeko la Wanyamapori kama vile tembo pamoja na mamba.
No comments:
Post a Comment