SERIKALI INAENDELEA KUIMARISHA SEKTA YA UTAMADUNI NCHINI - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Saturday, 8 January 2022

SERIKALI INAENDELEA KUIMARISHA SEKTA YA UTAMADUNI NCHINI

Mkurugenzi wa Maendeleo ya Utamaduni kutoka Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo Dkt. Emmanuel Temu akicheza ngoma ya Mjungu inayochezwa na kabila la Wapare alipofanya ziara ya kikazi mkoani Kilimanjaro kwa kutembelea vikundi vinavyojishughulisha na masuala mbalimbali ya kiutamaduni ili kuhamasisha wananchi kuendeleza mila na desturi njema kwa kizazi cha sasa na vizazi vijavyo.

Mkurugenzi wa Maendeleo ya Utamaduni kutoka Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo Dkt. Emmanuel Temu akiongea na wanakikundi cha wanakikundi cha utamaduni cha Furahisha kutoka kijiji cha Mwaniko wiayani Mwanga mkoa wa Kilimanjaro alipofanya ziara ya kikazi kutembelea vikundi vinavyojishughulisha na masuala mbalimbali ya kiutamaduni ili kuhamasisha wananchi kuendeleza mila na desturi njema kwa kizazi cha sasa na vizazi vijavyo.


Kikundi cha ngoma za asili cha Rosi kutoka Marangu wakicheza ngoma ya Rosi.

Na Eleuteri Mangi, WUSM - Moshi

SERIKALI ya Awamu ya Sita chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan ipo mstari wa mbele kusimamia, kuendeleza na kuimarisha masuala ya utamaduni nchini hatua inayosaidia kudumisha mila na desturi za Mtanzania kwa kizazi cha sasa na kijacho.

Hayo yamedhihirishwa na Mkurugenzi wa Maendeleo ya Utamadini kutoka Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt. Emmanuel Temu alipofanya ziara ya kikazi mkoani Kilimanjaro kwa kutembelea vikundi vinavyojishughulisha na masuala mbalimbali ya kiutamaduni katika makabila ya wapare, wachaga, wamasai pamoja na wagweno wanavyoendeleza utamaduni wao kupitia ngoma za asili, vyakula vyao pamoja na lugha zao. 

“Huu ni muda mwafaka wa kuwafundisha vijana wetu utamaduni wetu kwa kuunda vikundi vya ngoma za asili kama sehemu ya kutunza amali za utamaduni kupitia vyakula, historia za makabila yetu, mavazi, vifaa vya kiutamaduni pamoja na mila na desturi ambazo ni njema kwa vijana wetu” amesema Dkt. Temu.

Dkt. Temu ameongeza kuwa Septemba 8, 2021 Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan akiwa kwenye tamasha la Utamaduni lililofanyika eneo la Kisesa mkoani Mwanza alihimiza mikoa yote nchini kuwa na matamasha ya utamaduni katika maeneo yao ili kuwarithisha watoto na vijana utamaduni wao.

Hatua hiyo ya kiongozi wa nchi inaonesha Serikali inatoa msukumo wa wananchi wahamasike kulinda, kutunza, kuhifadhi, kuthamini na kuendeleza utamaduni wa mtanzania.  

Akiwa wilayani Mwanga mkoani humo Dkt. Temu amekutana na Mkuu wa Wilaya hiyo Bw. Abdallah Mwaipaya ambaye ameahidi kuendelea kushirikiana na Wizara na kuwahamasisha wananchi na vikundi mbalimbali vya utamaduni katika wilaya hiyo ili kuendeleza mila na desturi njema kwa kizazi cha sasa na vizazi vijavyo.

Akinukuu maneno ya Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere Bw. Mwaipaya alibainisha kuwa Baba wa Taifa aliwahi kusema “Utamaduni ni kiini ama roho ya Taifa lolote. Taifa lisilo na utamaduni ni sawa na mkusanyiko wa watu wasio na roho.”

Kwa upande wake Mkuu wa wilaya ya Siha Bw. Thomas Apson amesema ziara hiyo imewatia moyo na wapo tayari kutoa ushirikiano kila wakati kwa kuwa hilo ni jambo jema na kila mtu anaguswa kwa namna yake ili kuimarisha, kuboresha na kuendeleza utamaduni wetu kwa watoto na vijana wajue mila na desturi zao. 

Vikundi ambavyo vimetembelewa katika ziara hiyo ni kikundi cha Lambo Daima kutoka kijiji cha Lambo, kikundi cha Teule  kutoka kijiji cha Kisanjuni, kikundi cha Furahisha kutoka kijiji cha Mwaniko ambavyo vyote vipo wilaya ya Mwanga pamoja na kikundi cha Rosi kutoka Marangu wilaya ya Moshi Vijijini.

Vikundi vingine ambayo vimetembelewa ni Gonjaza Asili Star kutoka Suji, Lukungu Sanaa Group kutoka Vudee Nyika kata ya Bangalala pamoja na kikundi cha Wazee Nasuro kutoka kijiji cha Nasuro kata ya Mwembe vyote kutoka wilayani Same.

Katika wilaya ya Hai ambapo ujumbe huo umekutana na mghani mashairi Bw. Seifu Mkambala wakati katika wilaya ya Siha kikundi cha Osiligilai kutoka kijiji cha Ndinyika Karansi kimepata fursa ya kutembelewa na kuonesha namna wanavyoendeleza utamaduni wa kabila la Wamaasai katika eneo lao ambapo asilimia kubwa ya wanakikundi hicho ni vijana jambo linalotia moyo kuwa utamaduni huo unaendelezwa tofauti na vikundi vingine ambavyo idadi ya washiriki wengi ni watu wazima pamoja na wazee. 


No comments:

Post a Comment