Dk. Mwinyi ametoa pongezi hizo leo katika hafla ya Ufunguzi wa Mradi wa Hoteli ya Kitalii ya Nyota Tano ya Marijani Resort & SPA iliopo Pwani Mchangani, Mkoa wa Kaskazini Unguja.
Amesema moja ya njia ya kujenga mahusiano mema kati ya Wawekezaji na wananchi ni kujenga utamaduni wa kurejesha sehemu ya faida wanayopata kwa jamii ili kusaidia utekelezaji wa miradi mbali mbali ya kijamii.
Alieleza kuwa kuna baadhi ya maeneo ambapo Wawekezaji wamekuwa hawana mashirikiano na wadau mbali mbali wa utalii kama vile wavuvi ,hivyo alisisitiza umuhimu wa kushirikiana ili pande zote ziweze kunufaika. Dk. Mwinyi alitumia fursa hiyo kumpongeza Mwekezaji wa Mradi huo kwa namna anavyoshirikiana na wananchi wa Pwani Mchangani katika kuendeleza kilimo cha zao la Mwani.
Aidha, alisema kuwepo kwa mfululizo wa matukio ya Uwekaji wa mawe ya msingi pamoja na ufunguzi wa miradi mbali mbali ya Hoteli hapa nchini ni mafanikio ya juhudi za Serikali za kuvutia Wawekezaji hapa nchini, ikiwa ni kielelezo cha kuvutiwa na sera na mipango iliopo.
Alisema juhudi za pamoja kati Serikali na wadau wa Utalii pamoja na kuwepo kwa mani na utulivu nchini, ni mambo yanayoendelea kuvutia Wawekezaji. Alisema hatua hiyo imechochea Wawekezaji wengi kujenga azma ya kuja nchi kuwekeza katika Visiwa kumi vidogo vidogo katika miradi ya hadhi ya juu, hivyo akasisitiza umuhimu wa kuendeleza ushirikiano na kudumisha amani iliopo.
Alimpongeza Mwekezaji na wanahisa wenzake kutoka Mauritius ambao ni Kampuni za Avenes Limited, Harwood Limited na Amcop Investment Limited kwa uamuzi wao wa kuwekeza hapa nchini katika mradi mkubwa wenye hadhi unaogharimu Dola za Kimarekani Milioni 10.5, na akatumia fursa hiyo kuwahakikishia mitaji na amana zao kuwa salama.
Alisema katika kuimarisha Uwekezaji, Serikali inatekelezaji mikakati mbali mbali ya kuimarisha mazingira ya Uekezaji nchini, kwa kuimarisha miundombinu muhimu kwa maendeleo ya sekta ya Utalii.
Alisema hatua za kuimarisha viwanda vya ndege na bandari ina lengo la kuimarisha sekta ya usafirishaji na akabainisha hatua iliyochukuliwa na serikali katika kukiimarisha kiwanda cha Ndege cha Pemba inalengo la kukifanya kisiwa hicho kuwa eneo maalum la Kimkakati na Uwekezaji.
Alitoa wito kwa Wawekezaji katika sekta zote kuja kuwekeza Zanzibar, akisema kwamba kuna fursa nyingi na mazingira ya kuvutia.
Aidha, Dk. Mwinyi aligusia suala la usalama wa watalii na kusema ni miongoni mwa vipaumbele vya Serikali, hivyo akawahimiza Wakuu wa Mikoa na Wilaya kuendelea kufanyakazi kwa karibu na Wawekezaji walio katika maeneo yao ili kubaini na kuzitafutia ufumbuzi changamoto mbali mbali zinazowakabili.
Aliitaka Mikoa hiyo kuwa na mipango thabiti ya kupambana na vitendo vyote vinavyoweza kurudisha nyuma juhudi za kukuza utalii, kuharibu utamaduni pamoja na kuipa nchi sifa mbaya.
Aidha, akatumia fursa hiyo kuwahimiza wafanyakazi wote wanaotoa huduma kwa wawekezaji na wageni kuhakikisha wanatoa huduma zinazokidhi viwango na matarajio ya watalii kwa misingi ya uzalendo na uadilifu, kwa kutambua kuwa mafanikio yaliopo ndio msingi wa kukuza pato la taifa na kuimarisha ajira.
Vile vile akazitaka taasisi zinazoshughulikia masuala ya Ujasiriamali kuongeza kasi katika kubuni mipango itakayoweza kutumika ipasavyo katika sekta ya utalii ili kuimarisha soko la ndani la bidhaa zinazozalishwa nchini.
“Bado hatujawaunganisha vizuri wajasiriamali wetu wa sekta ya utalii, kwenye eneo hili kuna fursa nyingi za wajasiariamali wetu…”, alisema.
Aliwapongeza wamiliki wa Hoteli hiyo kwa kuonyesha nia ya kununua bidhaa zote zinazopatikana hapa nchini, huku akiwakumbusha Wawekezaji kutekeleza wajibu wao kwa mujibu wa makubaliano yaliomo katika mikataba, ikiwemp kutii sheria za nchi katika ulipaji wa kodi na tozo mbali mbali, ajira pamoja na maslahi ya wafanyakazi wao.
Naye,Waziri wa Nchi (OR) Kazi, Uchumi na Uwekezaji, Mudrik Ramadhan Soraga alisema mradi huo una manufaa makubwa kwa wananchi wa maeneo hayo na wananchi wa Zanzibar kwa ujumla na kupongeza juhudi na miongozo ya Rais Dk. Mwinyi kuwa imekuwa chachu katika kuvutia Wawekezaji.
Alisema Wizara hiyo inaendelea kufanya juhudi kuhakikisha kunakuwepo mazingira bora ya uwekezaji, hususan katika suala la utoaji wa maamuzi ili kuyatolea maamuzi ya haraka mambo mbali mbali.
Aidha, Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Unguja, Ayoub Mohamed Mahamoud alisema katika kufanikisha dhamira ya kupunguza ajali na kuimarisha usalama wa watali, Mkoa huo unaendelea na programu maalum ya kuzungumza na madereva wa aina mbali mbali , ikiwemo wanaoendesha gari za watalii, baada ya kubaini kuwepo matukio ya ajali za mara kwa mara zinazojitokeza Mkoani humo.
Alieleza kuwa Mradi wa Marijan Resort & SPA unatoa funzo kwa kiasi gani Wawekezaji hao wanaweza kuendesha shughuli zao za kitalii kwa mashirikiano makubwa na wakulima wa mwani, ambao ni sehemu kubwa ya wananchi wa maeneo hayo.
Mapema, Mwenyekiti wa Kampuni ya ZK Venture Ltd, Wawekezaji wa Mradi wa Marijani Resort & SPA Amin Manji alisema ujio wa mradi huo unatokana na ari na juhudi za Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali mwinyi za kuvutia Wawekezaji kote Duniani kuja kuekeza Zanzibar.
Alisema Mradi wa Marijani Resort & SPA ni mradi wa hoteli ya Nyota tano, uliofanikishwa ujenzi wake kupitia Kampuni mbali mbali za Kizalendo, ukiwa na jumla ya vyumba 82 na maeneo mbali mbali ya utoaji huduma pamoja na kuwa na uwezo wa kuchukua wageni 104.
Katika hatua nyengine, Mwananchi na mkulima wa Mwani kutoka Shehiya ya Pwani Mchangani, Mwanakheri Mussa Mohamed alimshukuru Mwekezaji wa mradi huo kwa kuonyesha imani ya dhati kwa wananchi wa maeneo hayo na kusema ni mfano mzuri wa kuigwa na wawekezaji wengine.
Alimpongeza Mwekezaji huyo kwa kutoa fursa kwa wakulima wa Mwani kuendelea na shughuli za kilimo hicho katika maeneo yao ya asili (mbele ya hoteli) pamoja na kuwapatia eneo maalum kwa ajili ya kuanikia mwani huo.
Alitumia fursa hiyo kuiomba Serikali kuangalia namna ya kuwainua wakulima wa kilimo hicho cha mwani, kwa kigezo cha kutozwa kiwango kidogo cha bei, ikilinganishwa na kazi ngumu ya kilimo hicho, sambamba na kuiomba Serikali kuwaondolea kero ya ukosefu wa maji safi na salama wananchi wa eneo hilo.
No comments:
Post a Comment