WAZIRI MWAMBE AHIMIZA WATANZANIA KUUNGA MKONO CRDB…! - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Monday, 19 April 2021

WAZIRI MWAMBE AHIMIZA WATANZANIA KUUNGA MKONO CRDB…!

Waziri wa Uwekezaji, Geoffrey Mwambe akizungumza katika Semina ya Uwekezaji iliyoandaliwa na Benki ya CRDB kwa wanahisa wake na wadau wengune mbalimbali iliyofanyika pia kwa kupitia mtandao na kuhudhuriwa na washiriki zaidi ya 3,000, Semina hiyo ilifanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere, jijini Dar es salaam.Picha zote na Othman Michuzi.
 
  • Asema ni benki ya kizalendo yenye nia ya dhati ya kuwakomboa wananchi kiuchumi
  • Aitaka Benki ya CRDB kuanzisha dirisha la Viwanda kuchochea Uwekezaji

Dar es Salaam, 17 Machi 2020 - Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Uwekezaji  Geoffrey Mwambe amewataka Watanzania kuiunga mkono Benki ya CRDB kwa kwa kupata huduma katika benki ili kuendelea kuiimarisha kwani benki hiyo inaonyesha uzalendo wa hali ya juu katika kuwainua wananchi kiuchumi. Waziri Mwambe amezungumza hayo wakati wa Semina ya Uwekezaji na Fedha iliyoandaliwa na Benki ya CRDB na kufanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere na kuhudhuriwa na watu zaidi ya 3,000 ambapo wengi wao walihidhuria kupitia mtandao.

“Benki hii imekuwa ikiwathamini sana Watanzania kwa kuandaa kuanzisha huduma na programu wezeshi kiuchumi kwa wananchi. Hivyo tunapaswa kuiunga mkono ili iendelee kuwepo na kuwahudumia Watanzania. Fungueni akaunti katika Benki hii na mtumie huduma za kisasa za kidijitali ambazo zinatolewa hapa,” alisistiza Waziri Mwambe.

 
Waziri Mwambe alisema kwa kuwa Benki ya CRDB imekuwa mstari wa mbele katika kusaidia agenda za maendeleo ya nchi anaialika Benki hiyo kushiriki katika mkakati wa kupanua wigo wa uwekezaji nchini kwa kuanzisha dirisha maalum la viwanda ili kuchochea kuimarika viwanda vidogo na vikubwa kwa kuwawezesha wawekezaji kupata mitaji ya uhakika.

“Kwa kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Benki hii Abdulmajid Nsekela ndio Mweneyeki wa Umoja wa Mabenki Tanzania (TBA) nimuombe ashawishi na mabenki mengine kutekeleza hili ili. Nitaandaa mkutano na umoja huu iliyuweze kulijadili hili kwa upana,” aliongezea Waziri Mwambe.

Aidha, Waziri Mwambe alisema alibainisha kuwa ili sekta binafsi iweze kuwa na mchango mkubwa katika maendeleo ya taifa kunatakiwa kutengenezwa mazingira mazuri ya kuwawezesha watu na makampuni kupata fedha za kuwekeza. Alisema Serikali kwa upande wake inaendelea kuboresha mazingira ya biashara kwa kuondoa urasimu na kupunguza utitiri wa kodi na tozo ili kupunguza gharama za uwekezaji nchini ikiwa ni utekelezaji wa agizo la Rais wa Awamu ya Sita, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan.

“Mkurugenzi Mtendaji naomba nikuhakikishie mkiweza kuwawezesha wawekezaji hawa kuwekeza katika viwanda faida ni kubwa mno katika uchumi wa taifa letu. Tutaweza kuimarisha uchumi kwa kiasi kikubwa, ajira zitakuwa za kutosha, mzunguuko wa fedha utaongezeka, na hata faida mtakayopata itakuwa zaidi ya hii shilingi bilioni 165 ambayo mmeipata mwaka jana,” alisema Waziri Mwambe.

Katika hotuba yake Waziri Mwambe aliainisha kuwa mpango wa Serikali nikuachana na kusafirisha malighafi nje ya nchi kwa kutengeneza bidhaa hapa nchini kupitia viwanda vya ndani na kuzitafitia soko nje ya nchi. “Mfano kwa upande wa zao la pamba tumeweka mkakati ndani ya miaka mitatu hatutaki kuona tuna uza pamba ghafi nje,” amesema Waziri Mwambe.

Waziri Mwambe ameipongeza Benki ya CRDB kwa kuandaa Semina hiyo ya Uwekezaji na Fedha  huku akiwataka wananchi kujenga utamaduni wa kujiwekea akiba na kuwekeza katika masoko ya mitaji ili kujijenga kiuchumi.

“Niwahamasishe kwa kuanza kuwekeza ndani ya Benki yetu ya CRDB. Tukiwa tunaweka akiba na kutazama riba, tukumbuke pia kuna gawio, ambalo linafaida kubwa. Sasa hivi Benki hii tunaimiliki kwa 80%, tuwekeze tufike 100%,” aliongezea huku akisisitoza juu umuhimu wa kufikisha elimu hiyo hadi vijijini ili kuwafikia wananchi wengi zaidi.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela alisema malengo ya Semina hiyo ni kuona Watanzania wengi zaidi wanashiriki katika fursa za uwekezaji hapa nchini pamoja na kupata uelewa wa huduma za benki hiyo zitakazowasidia kuwa wawekezaji wazuri.

Akielezea kuhusu program mbalimbali za elimu ya fedha na uwekezaji kwa umma, Nsekela amesema Benki ya CRDB  ikiwa benki ya kizalendo inajivunia kwa kuwa mstari wa mbele katika kufikisha elimu ya fedha na uwekezaji kwa Watanzania. Nsekela pia alimhakikishia Waziri Mwambe kuwa Benki hiyo itaendelea kutoa elimu hiyo kwa wananchi ili kujenga uwajibikaji wa kifedha katika jamii na kuongeza ujumuishi wa kifedha.

“Watanzania wengi wamekuwa nje ya mfumo rasmi wa kifedha kwasababu hawana elimu ya kutosha hivyo kupelekea wengi kuogopa. Lakini kupitia elimu hii tunaamini wengi sasa wataweza kujiunga na taasisi za kifedha lakini pia kichangamkia fursa za uwekezaji zilizopo katika sekta hii pamoja na masoko ya mitaji,” alisema Nsekela.

Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Benki ya CRDB, Dkt. Ally Laay alimshukuru Waziri Mwambe kwa kuikaribisha benki hiyo kushirikiana na Serikali katika kutekeleza mikakati ya kuchochea uwekezaji nchini, ambapo alimhakikishia kuwa benki hiyo itakwenda kuandaa sera ambayo itakwenda kuelekeza na kusimamia uwezeshaji katika sekta ya viwanda na kuwa pendekezo la kuanzisha dirisha la viwanda limepokelewa kwa ajili ya utekelezaji.

Mada mbalimbali ziliwasilishwa katika Semina hiyo ya Uwekezaji na fedha ikiwamo; Biashara ya Hisa Kidijitali iliyowasilishwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE),  Moremi Marwa, Mada ya Uwekezaji wa Pamoja iliyowasilishwa na Mkurugenzi wa Uendeshaji UTT AMIS, Daniel Mbaga, Mada ya Gawio kwa Wanahisa iliyowasilishwa na Katibu wa Benki ya CRDB, John Rugambo, Mada ya Uwekezaji Endelevu wa Mali iliyowasilishwa na Mkurugenzi wa Joachiam and Jacob Attorneys, Waki Grace Joachim, Mada ya Uwekezaji kupitia Huduma na Bidhaa za Benki na Bidhaa iliyowasilishwa na  Meneja wa Idara ya Hiiazina Benki ya CRDB, Hemed Masumai, na Mada juu ya Huduma za Benki ya CRDB Kufanikisha Uwekezaji iliyowasilishwa na Mkurugenzi wa Wateja Wadogo na Wakati wa Benki ya CRDB, Boma Raballa.

Washiriki wa Semina hiyo waliipongeza Benki ya CRDB kwa kuandaa semina hiyo huku wakisema imesaidia sana kuongeza uelewa juu ya masuala ya uwekezaji na huduma za kifedha. Baadhi ya washiriki walipendekeza semina hiyo kufanyika hata mara tano kwa mwaka kwani bado uelewa wa masuala ya uwekezaji katika jamii ni mdogo.
Akitoa shukrani kwaniaba ya washiriki, Waziri Mkuu Mstaafu Fredrick Sumaye ambaye pia ni Mwanahisa wa Benki ya CRDB aliishuru Bodi na Menejimenti ya benki hiyo kwa kuendelea kutekeleza programu za elimu ya uwekezaji na fedha kwa Watanzania. Sumaye pia alitumia nafasi hiyo kuwakaribisha Watanzania wengine kuwekeza katika Benki yao ya CRDB. “Faida ya kuwekeza huku ni kubwa mno, niwakaribishe mjionee wenyewe,” alisisitiza Sumaye.

Waziri wa Uwekezaji Geoffrey Mwambe (katikati) akiwasalimia washiriki wa Semina ya Uwekezaji iliyoandaliwa na Benki ya CRDB katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere. Wengine pichani ni Mwenyekiti wa Bodi ya Benki ya CRDB, Dkt. Ally Laay (wapili kulia), Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Benki ya CRDB, Prof. Neema Mori (wakwanza kushoto), Mkurugenzi Mtendaji Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela (wapili kushoto) na Katibu wa Benki ya CRDB, John Rugambo. Semina hiyo pia ilifanyika kupitia mtandao na kuhudhuriwa na washiriki zaidi ya 3,000.


Waziri wa Uwekezaji Geoffrey Mwambe akiwa katika picha ya pamoja na Wajumbe wa Bodi ya Benki ya CRDB wakionGozwa na Mwenyekiti, Dkt. Ally Laay, Mkurugenzi Mtendaji Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela (wanne kushoto) na Katibu wa Benki ya CRDB, John Rugambo (wapili kushoto) wakati wa Semina ya Uwekezaji iliyoandaliwa na Benki ya CRDB. Semina hiyo pia ilifanyika kupitia mtandao na kuhudhuriwa na washiriki zaidi ya 3,000.

Waziri wa Uwekezaji Geoffrey Mwambe akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya wanahisa wa Benki ya CRDB wakati wa Semina ya Uwekezaji iliyoandaliwa na Benki ya CRDB. Semina hiyo pia ilifanyika kupitia mtandao na kuhudhuriwa na washiriki zaidi ya 3,000.

Waziri wa Uwekezaji Geoffrey Mwambe akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya wanahisa wa Benki ya CRDB wakati wa Semina ya Uwekezaji iliyoandaliwa na Benki ya CRDB. 
Waziri wa Uwekezaji Geoffrey Mwambe akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya Mameneja wa Matawi ya Benki ya CRDB wakati wa Semina ya Uwekezaji iliyoandaliwa na Benki ya CRDB. S

Waziri wa Uwekezaji Geoffrey Mwambe akiwasili katika Ukumbi wa Selous katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere katika Semina ya Uwekezaji iliyoandaliwa na Benki ya CRDB. Alioambatana nao ni Mwenyekiti wa Bodi ya Benki ya CRDB, Dkt. Ally Laay (kushoto) na Mkurugenzi Mtendaji Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela (kulia).Semina hiyo pia ilifanyika kupitia mtandao na kuhudhuriwa na washiriki zaidi ya 3,000.


















No comments:

Post a Comment