Na Mwandishi Wetu, Mwanza
MKUU wa Mkoa wa Mwanza, Mhe. John Mongela anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika uzinduzi wa michezo ya Kombe la Mei Mosi inayofanyika kwenye uwanja wa CCM Kirumba jijini hapa. Uzinduzi huo utatanguliwa na maandamano ya wachezaji zaidi ya 700 wanaoshiriki kwenye michezo ya soka, netiboli, kuvuta Kamba, baiskeli, riadha, karata, bao na draft.
Katika michezo ya netiboli iliyofanyika leo timu ya Wizara ya Mambo ya Ndani imeiadhibu bila huruma Wizara ya Mambo ya Nje kwa kuwafunga magoli 80-4, Hadi Mapumziko washindi walikuwa mbele kwa magoli 41-2, yaliyofungwa na Mwanaisha Ally magoli 61 na Mery Mangi magoli 19, huku magoli pekee ya Mambo ya Nje yalifungwa na Juneck Mbisse huku Patricia Kiswaga hakufunga.
Katika mchezo mwingine timu ya Ikulu iliwafunga Shirika la Maendeleo ya Petrol nchini (TPDC) kwa magoli 40-8, ambapo wafungaji Anna Msulwa alifunga magoli 31 huku Sophia Komba magoli manne na Irene Kanije magoli matano, huku magoli ya TPDC yalifungwa na Elizabeth Luanda magoli sita na Rehema Said magoli mawili. Hadi mapumziko Ikulu walikuwa mbele kwa magoli 23-6.
Timu ya Tanesco iliwafunga wenyeji Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mwanza (MWAUWASA) kwa magoli 48-0, magoli ya washindi yaliyofungwa na Celestine Mbassa 45 na Agnes Ryoba matatu. Hadi mapumziko mshindi alikuwa na magoli 25-0.
Katika mchezo wa soka timu ya Ukaguzi waliwafunga MWAUWASA, kwa magoli 2-1, yaliyofungwa na Nyanda Mabuga na Cassian Luoga na goli pekee la MWAUWASA lilifungwa na Telesifori Mwajemu.
Mchezo mwingine uliokuwa mkali timu ya Wizara ya Kilimo iliwafunga Mambo ya Nje kwa magoli 4-3, yaliyofungwa na Johnson Tamba magoli matatu na Ahmed Kinyunyu goli moja, huku ya Mambo ya Nje yalifungwa na Habibu Soud, Elly Chuma na Mikidadi Magole.
Katika michezo ya kuvuta kamba wanaume timu ya Wizara ya Mambo ya Nje waliwavuta Wizara ya Kilimo kwa mivuto 2-0; huku Tanesco wakiwashinda TPDC kwa mivuto 2-0; wakati Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) wakiwashinda MWAUWASA kwa mivuto 2-0; nayo timu ya Uchukuzi ilipata ushindi wa chee wa mivuto 2-0 baada Ulinzi kushindwa kuonekana uwanjani.
Kwa mechi za wanawake timu ya Uchukuzi iliwavuta Tanesco 2-0; nayo TPDC iliwavuta MWAUWASA kwa 2-0.
Michuano hiyo inaendelea kesho kwa upande wa soka timu ya Uchukuzi itakutana na TPDC; huku Tanesco watawakaribisha NCAA; wakati katika netiboli timu ya Uchukuzi watakutana na Ulinzi; nayo Wizara ya Kilimo itacheza na TPDC; na Tanesco na Wizara ya Mambo ya Ndani.
Katika michezo ya kuvuta kamba timju ya TPDC watacheza na Wizara ya Kilimo; huku Tanesco kukutana na Wizara ya Mambo ya Nje; Uchukuzi kuumana na Ukaguzi zote zikiwa ni mechi za wanaume; wakati kwa upande wa wanawake timu ya NCAA kucheza na MWAUWASA; nayo Taasisi ya Saratani Ocean Road wakutana na Uchukuzi.
No comments:
Post a Comment