WAPIGA KURA, TEMA NIMCHAPE..! - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Monday 15 June 2020

WAPIGA KURA, TEMA NIMCHAPE..!

Joseph Kasheku.

Na Tata Gordon Kalulunga

NAVUTIWA sana siasa za Wabunge Kama Msukuma (Joseph Kasheku) na wenzake akina Mwakajoka bila kumsahau Naibu Waziri Hessein Bashe na wenzao, hasa katika kusema ukweli mchungu.
TUNAELEKEA katika mchakato wa kuwapata wapeperusha bendera za vyama vya siasa katika nafasi ya Rais, Wabunge na Madiwani/wawakilishi Mwaka huu 2020.

Huu ni wakati sahihi wa kuchagua viongozi sahihi ili kupunguza malalamiko ya kwamba huyu ametutelekeza na wala hana mawazo mapya.

Wananchi katika Kata na Majimbo kadhaa wamekuwa wakinung'unika baada ya kutoona ufanisi chanya wa viongozi wao waliokuwa wamewachagua mwaka 2015.

Wakati wananung'unika baadhi yao mioyo inawasuta kwasababu walijihusisha kwa namna moja au nyingine kuwachagua viongozi kwa mkumbo na baadhi kupata tufedha twa chumvi kutoka kwa wagombea.

Sauti kutoka Nyikani inawataka wananchi na viongozi walio kwenye Mamlaka za uteuzi waache kujichezea wenyewe kwa kuona mgombea anayetoa chochote ni mwema kwao kwa kigezo kuwa atarahisisha pia kampeni kutokana na ukwasi wake wa fedha, wakati tafsiri ni kwamba analipa mishahara kabla hajapata kazi na akipata kazi hawezi kurudi.

Wanasiasa wengi wanaotoa chochote, wengi wao wanaandika hizo gharama hata kama katembeza viberiti kila nyumba, hivyo anapopata uongozi lazima arejeshe kwanza fedha zake maana baadhi yao wanadiliki kuununua uongozi.

Aisha ni vema wananchi wakawa na uelewa sahihi katika utoaji taarifa katika vyombo vinavyosimamia maadili na taasisi ya kupambana na kuzuia Rushwa (TAKUKURU) ili wahusika waweze kushughulikiwa au kuonywa hadharani.

Hofu kwa jamii imekuwa kikwazo katika utoaji wa taarifa.

Ni vema Mamlaka zinazohusika, kama Mheshimiwa Rais wetu mpendwa, Dr. John Pombe Magufuli alivyoutangazia umma kuwa wananchi waondoe hofu katika kukabiliana na Ugonjwa wa Corona, vivyo hivyo wananchi waondolewe hofu katika utoaji wa taarifa za uhalifu mbalimbali ikiwemo suala la rushwa na hofu za hisia za watu waitwao wasiojulikana na hofu za wasema ukweli kutafsiriwa kama ni wachochezi au kiitwacho kuichafua serikali.

Na hapa nakiomba chama kinachounda Serikali, Chama Cha Mapinduzi (CCM), kuendelea kuwa watetezi wa waitwao wanyonge kama misingi yake ilivyo ya kujali utu wa wanyonge badala ya baadhi ya viongozi wa chama kujigeuza kuwa Serikali.

Kila mzazi anafahamu namna faraja isiyo ya kweli ampayo anapewa mtoto anapolia.

Mtoto anaulizwa nani mkorofi? Akisema dada, mtoto anaambiwa tema mate tumchape.

Mtoto anatema mate na kulaghaiwa kuwa aliyemtendea jambo ambalo limemsababishia kulia amepigwa kisha anaambiwa nyamaza.

Mheshimiwa Rais wetu Dr. Magufuli aliwaondoa hofu wananchi kuwa uchaguzi Mkuu 2020 utakuwa wa haki na kuwaachia wananchi wachague kiongozi wamtakaye, na kwasababu Rais wetu anaishi katika uhalisia bila ubaguzi, hili litafanyika kama alivyoahidi na jambo hili wananchi wasiwe na hofu kabisa kama michapo ya mtaani inavyoendelea.

Sauti kutoka Nyikani inasema kuwa, kwasababu Maendeleo yanaenda kasi, ni vema wananchi wakaondoa hofu mioyoni mwao ikiwemo wale wanaosema hawataweza kwenda kupiga kura kwasababu hofu yao ni kwamba mazingira yamebadilika na kwamba wakisema maoni yao wanaweza kuguswa. Yaani mlango ukigongwa hawana uhakika kama wanaogonga ni watu salama.

Nitumie nafasi hii kuwahamasisha wananchi kujitokeza kupiga kura wakati utakapofika na kuwachagua viongozi watenda haki na warejee kauli za Mheshimiwa Rais Dr. Magufuli kuwa Maendeleo hayana chama na ndiyo maana hata katika teuzi zake anateua hata kutoka vyama vya upinzani.

Na kwa wale wanaotumia majina ya viongozi kufanya fujo zenye manufaa" majimboni pia ni vema Mamlaka zinazohusika zikawatendea haki wananchi bila upendeleo.

Kama kuna viongozi katika Kata na Majimbo yao walikuwa wanaimba korasi za Maendeleo bila kuwa na ubunifu na mawazo mapya, ni vema majina yao yakakatwa.

Wananchi wengi Wana hofu mioyoni na kwa Mambo mengi wanadhani wanafarijiwa kama watoto kwa kauli ile ya kuwaambia, tema tumchape.

Huu ni wakati Kama Taifa kusimama kwa Umoja wetu na kushikamana maana nyakati za uchaguzi kuna watu wanatumia mianya isiyo mizuri kuwagawa wananchi.

Sisi ni Watanzania huru katika nchi huru.

Ndiyo maana nasema kuwa, wapiga kura, tema nimchape.

0765 615858

No comments:

Post a Comment