Mkurugenzi Mtendaji wa Kimimbi Herbal Clinic inayojishughulisha na utengenezaji wa dawa za asili, Kafana Mussa akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake Kiwalani jijini Dar es Salaam jana.
Na Dotto Mwaibale
KIMIMBI Herbal Clinic inayojishughulisha na utengenezaji wa dawa za asili imeiomba Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR) kuruhusu dawa ya Kafana 20 inayotibu ugonjwa wa Corona ili iwasaidie wananchi.
Ombi hilo limetolewa na Mkurugenzi Mtendaji wa Clinic hiyo Kafana Mussa wakati akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake Kiwalani jijini Dar es Salaam jana.
"Ombi letu kubwa kwa NIMR ni kuruhusu dawa yetu hii ili kuwasaidia wananchi katika kipindi hiki cha ugonjwa wa Covid-19" alisema Kafana.
Alisema mara baada ya kugundulika kwa ugonjwa huo nchini China wao kama watafiti walichukua jukumu la kufanya utafiti na kutengeneza dawa yao ya kwanza ya kutibu ugonjwa huo ambayo waliipa jina la Kafana 20.
Alisema walianza kuifanyia majaribio yasio rasmi kwa watu waliokuwa na viashiria vya ugonjwa huo na kuonesha mafanikio makubwa.
Mussa alisema April 10, 2020 waliandika barua kwenda Wizara ya Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto ili kupata kibali ambapo waliambiwa waende NIMR.
Alisema baada ya kufika NIMR walitakiwa kueleza namna walivyotengeneza dawa hiyo ambayo ilitumia sampuri ya miti aina tano.
" Baada ya kutoa maelezo hayo na kuifanyia utafiti wao walituambia dawa hiyo hawataweza kuitoa kwa sababu miti iliyotumika kutengeneza ni mingi hivyo itawawia vigumu kuipata na kutengeneza dawa nyingi vinginevyo wamtafute mwekezaji mkubwa ambaye atapanda aina ya miti hiyo kwa wingi ili waingie naye ubia wa kutengeneza dawa hiyo." alisema Mussa.
Mussa alisema jambo lingine waliloelezwa ni kuwa licha ya wao kuitengeneza wanao paswa kuitoa dawa hiyo ni NIMR kwa maana Serikali ambayo itachukua asilimia 90 ya fedha za mauzo na wao watachukua asilimia 10 tu.
Mkurugenzi huyo Kafana Mussa ameiomba Serikali kuruhusu dawa hiyo ili kusaidia wananchi katika kipindi hiki cha Covid-19 kama ambavyo Rais Dkt.John Magufuli amekuwa akihimiza kufanya maombI pamoja na kutumia dawa za asili na kujifukiza ikiwa na kuchukua hatua zote za kujikinga na ugonjwa huo.
Mussa alitumia nafasi hiyo kuwataka wananchi ambao watakuwa na viashiria vya ugonjwa huo kuwasiliana na Clinic hiyo kwa namba za simu 0743068792 na 0674456789 kwa msaada wa kitabibu.
No comments:
Post a Comment