SHIRIKA LA NYUMBA SINGIDA LAJIVUNIA MAFANIKIO YA MIAKA 60 YA UHURU - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Thursday, 9 December 2021

SHIRIKA LA NYUMBA SINGIDA LAJIVUNIA MAFANIKIO YA MIAKA 60 YA UHURU

Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt. Binilith Mahenge (kushoto) akizungumza na wafanyakazi wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) wakati wa maadhimisho ya miaka 60 ya Uhuru yalioadhimishwa jana kimkoa wilayani Manyoni. Kulia ni  Afisa Miliki Israel Ngapona.

Wafanyakazi wa shirika hilo Mkoa wa Singida wakiwa kwenye banda lao wakati wa maadhimisho hayo. Kutoka kulia ni Mhandisi wa Mkoa wa Shirika hilo Albert Guruyedi, Mhasibu wa shirika hilo Mkoa wa Singida,  Renalda Mlambo  na Afisa Miliki Israel Ngapona, 

Na Dotto Mwaibale,Singida.

SHIRIKA la Nyumba la Taifa (NHC) Mkoa wa Singida limejivunia mafanikio yake ya miaka 60 ya Uhuru kutokana na shughuli mbalimbali ilizozifanya katika kipindi hicho.

Hayo yalibainika katika sherehe za maadhimisho ya miaka 60 ya u

Uhuru wa Tanzania Bara na miaka 59 ya muungano yaliyofanyika jana kimkoa katika Wilaya ya Manyoni.

Akielezea mafanikio hayo Mhandisi wa Mkoa wa Shirika hilo Albert Guruyedi alisema Shirika hilo limejenga nyumba za makazi katika maeneo mbalimbali ya mkoa huo pamoja na nyumba za biashara kwa lengo la kuhakikisha wananchi wanapata huduma za Nyumba kwa bei nafuu.

"Tunawakaribisha wananchi mje mpange kwenye nyumba za Shirika la nyumba,zipo za makazi na za kibiashara karibuni sana." alisema Mhandisi Guruyedi.

Alisema wakati wa maadhimisho hayo NHC linajivunia mafanikio makubwa mengi ambayo pia yanaendelea kupatikana kwa maslahi sio tu ya shirika la nyumba bali na kwa ajili ya wananchi wa Mkoa wa Singida.

Alisema shirika hilo wametumia fursa ya maadhisho hayo  kutangaza nafasi walizonazo za majengo ya biashara mawili ya ambayo yamebaki na nafasi chache. 

Alitaja majengo hayo kuwa ni la Singida Shops ambalo ni kwa ajili ya maduka na ofisi ambalo lipo Mtaa wa Lumumba jirani na Soko Kuu la Mkoa wa Singida na jengo la pili kuwa ni la Singida Complex lililopo Mtaa wa Boma jirani na Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Singida ambalo ni kwa ajili ya maofisi na biashara.

Aidha Guruyedi alisema kupitia maadhimisho hayo wamewezakutangaza mradi wa nyumba 1000 uliopo Dodoma ambao kwa awamu ya kwanza wameanza kujenga nyumba 400 za kuishi ambapo nyumba 300 zimejengwa eneo la Iyumbu jirani kabisa na Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM).

Alisema nyumba hizo zote ni kwa ajili ya kuuzwa na tayari zimeanza kununuliwa na malipo yakiendelea kufanyika huku nyumba 100 za makazi zikiwa zimejengwa kwa ajili ya kupangishwa ambazo zipo eneo la Chamwino.

Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt.Binilith Mahenge alilipongeza Shirika hilo kwa mafanikio hayo na kulitaka kuendelea kutoa huduma kwa wananchi kama ilivyokuwa inakusudiwa na Serikali wakati inaanzisha shirika hilo hapa nchini.

Alisema shirika la nyumba limechangia mafanikio makubwa yaliyopatikana ndani ya Miaka 60 ya Uhuru katika sekta mbalimbali ikiwemo kurahisisha upatikanaji wa nyumba za kupangisha kwa bei nafuu.

Mkoa wa Singida umeadhimisha siku ya miaka 60 ya uhuru kwa takribani siku nne kwa kutembelea maeneo mbalimbali ya kihistoria,kufanya kongamano,michezo na baadaye kuhitimishwa kwa hutuba mbalimbali za viongozi.

No comments:

Post a Comment