Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere. |
Na Judith Mhina -Maelezo
Dhamira ya Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, Rais wa Kwanza wa Jamhuri ya Tanganyika na baadaye Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ya kuwaunganisha Watanzania na kuwa kitu kimoja bila ubaguzi wa kabila, dini, rangi, na eneo analotoka imeendelea kutekelezwa na Awamu zote za uongozi hapa Tanzania.
Dhamira hiyo ni mkakati wa muda mrefu na ndoto ya Baba wa Taifa kuwa mara Tanganyika ipatapo Uhuru atahakikisha anajenga Taifa lenye Umoja, Upendo, Mshikamano na lisilobaguana kwa namna yeyote ile, ikiwa ni kimbiilio la wale wote waliokosa amani na utulivu katika nchi zao za asili.
Akithibitisha utekelezaji wa azma hiyo, Mzee Juma Ismail (90) mwenyeji wa Masasi, ambaye ni mmoja wa vijana wa TANU Youth Legue (TYL), ambao walishiriki katika harakati za kugombania Uhuru wa Tanganyika akihudumu kama mlinzi wa mikutano mbalimbali ya Mwalimu Nyerere na mhamasishaji wa wananchi kujiunga na chama cha Tanganyika African National Union (TANU) na kuhakikisha nchi inapata Uhuru, ambaye kwa sasa ni mkazi wa kijiji cha Kerege Wilaya ya Bagamoyo.
Amemuelezea Mwalimu Nyerere katika mahojiano yaliyofanywa na Idara ya Habari Maelezo tarehe 09 Novemba 2021 katika kijiji cha Kerege Wilaya ya Bagamoyo Mzee Juma Ismail ametoa simulizi ifuatavyo:
Nyerere aliulizwa swali na vijana wa TYL, huku wakimshangaa Mwalimu na kutaka kujua ni kwa nini unachanganya makabila mbalimbali pamoja hujui kama watagombana? Amesema Juma Ismail.
Mwalimu alicheka na kujibu “Hapana hawawezi kugombana ndio watapatana na kuelewana kwa kuwa wakichanganyika Wasukuma, Wanyasa, Wamakonde, Wandengereko, Wamakuwa na wengine wote kwa sababu ninajenga Taifa moja la Tanganyika”.
Mzee Juma aliongeza simulizi kwa kusema kuwa, Mwalimu alisimulia “Unaposafiri wewe Mtanganyika kwenda nje ya nchi huwezi kusema natoka Masasi, bali unasema natoka Tanganyika. Lazima muelewe ili tuwe na nguvu na umoja yapasa tujenge Taifa imara la Tanganyika”.
Swali hilo lilitokana na Mwalimu Nyerere kuchukua vijana kutoka maeneo mbalimbali ya Tanganyika kwa ajili ya kuhamasisha kujiunga na chama cha TANU ili kuhakikisha nchi inapata Uhuru. Aidha, mara baada ya kupata uhuru chama cha TANU kiliandaa maeneo ya kuhamasisha uzalishaji wa mazao ya chakula na biashara, ikiwemo kijiji cha Gezaulole Mbwamaji Kigamboni Mkoa wa Dar-es-salaam na Kerege Wilaya ya Bagamoyo Mkoa wa Pwani, kwa lengo la kujenga siasa ya Ujamaa na Kujitegemea.
Kijiji cha Kerege kilianzishwa rasmi mwishoni mwa mwaka 1964 na kupewa hati mwaka 1965 kutokana na sera ya Serikali ya kuanzishwa kwa Settlement Scheme na kupokea vikundi vitatu vya wahamiaji kutoka maeneo matatu ambao ni ya vijana wa TYL ambao ni familia 105 kutoka Kitonga (Ruvu) na kuwasili Kerege tarehe 15 Desemba 1964.
Kikundi cha pili kilikuwa cha watu 50 kutoka kijiji cha Mapinga, ambao walitoka Ilala Boma Dar-es-salaam na kuwasili Mapinga tarehe 01 Julai mwaka 1964 mpakani mwa Wilaya ya Kinondoni na Bagamoyo, Kundi hili lilihamia kijiji cha Kerege tarehe 01 Februari 1965, na kundi la tatu lilitoka Nachingwea na kuwasili Kerege tarehe 13 Oktoba mwaka 1965.
Akielezea historia ya makundi hayo ya vijana wa TANU Youth Legue Mwenyekiti wa Kijiji cha Kerege Bernet Mauma Mujaga “Amesema mwaka 1962 vijana wa TYL kutoka Wilaya ya Bagamoyo vijiji vya Zinga, Pande, Mlinotini, Kiromo Yombo na Bagamoyo waliitikia wito wa viongozi wa Wilaya wa kuanzisha ushirika unaojulikana kama Bagamoyo Farming and Marketing Agricultural Association ( BFMAA) vijana hao walikwenda Kitonga Ruvu, na kufungua mashamba ya Mpunga na miwa a,mbapo vijana 600 walijitokeza na kufumgua mashamba yenye ukubwa wa ekari 700.”
Hivyo mwaka 1964 mmiliki wa shamba la Kerege mwenye asili ya Ugiriki Pania Topras aliliuza shamba lake kwa chama cha TANU na Serikali ya Tanganyika na kuwawezesha wana Ushirika wa BFMAA, ambapo Mwalimu Nyerere aliwashauri wana Ushirika hao kuhamia Kerege. Ambapo aliwaomba viongozi wao kwenda kuliangalia shamba hilo ambalo lilikuwa na ukubwa wa ekari 15,000 ambalo ndani yake mna mazao ya Minazi, Mikorosho, Maembe, na Michungwa.
Shamba hilo pia lilikuwa na Ng’ombe wa maziwa na nyama na Serikali iliwamiikisha shamba na kuagiza viongozi wao kutembelea shamba hilo ili kuridhia au la. Ambapo viongozi waliridhia na Jumla ya familia 105 kuhamia rasmi Kerege tarehe 15 Desemba 1964.
Utaratibu huu wa Mwalimu Nyerere ndio chanzo cha Taifa la Tanzania kuwa na umoja, mshikamano na amani ambapo alichanganya wanafunzi wa makabila mbalimbali. Mfano watoto wa shule za sekondari wa eneo la Kaskazini walipelekwa kusoma Kusini na Kusini walipelekwa kusoma shule za Magharibi na Magharibi kusoma shuke za Kaskazini kwa lengo la kuwawaandaa kujiona wote ni wamoja ni Watanzania, kujua jiografia ya Tanzania, kuelewa mila na desturi za maeneo mbalimbali kwa lengo la kuleta maelewano, umoja, amani na mshikamano.
Akizingatia azma yake ya Amani, Umoja, Mshikamano na kujenga Taifa moja la Tanzania Serikali ilianzisha Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) ambapo vijana wote wanaomaliza kidato cha Sita na wale waliohitimu mafunzo ya vyuo vya kati waliweza kushiriki mafunzo ya mwaka mmoja kwa mujibu wa sheria kwa lengo hilo hilo la kujenga Taifa moja.
JKT, ni kiungo kkubwa sana cha kuwajumuisha vijana kwa pamoja na kuwafanya wajione wako sawa wote na kujenga uzalendo wa hali ya juu wa kuipenda na kuilinda nchi yao kwa gharama yeyote ile kwa manufaa ya Taifa la Tanzania.
JKT, chimbuko lake limetokana na vijana wa TYL, walioshiriki harakati za Uhuru, Uhamasishaji wa kujiunga na chama, ulinzi wa mikutano mbalimbali ya TANU na kutekeleza siasa ya Ujamaa na Kujitegemea kwa vitendo. Wazee waliopo hadi tunafanya mahojiano haya tarehe 09 Novemba 2021 ni pamoja na Mzee Fransis Khalid (96) Juma Ismail (90) Bi Kashindye Mohamed Kikwande (69) ambaye mume wake Marehemu Ibrahim Nassoro alikuwa mwanachama wa TYL alizaliwa mwaka 1923 na kufariki mwaka 2020 ambaye ni Mwenyekiti wa kwanza wa kijiji cha Kerege.
Wito wa Wazee hao wa TANU na baadaye Chama Cha Mapinduzi ni kuendeleza salsafa ya Mwalimu Nyerere ya kuhakikisha viongozi wa sasa na wajao watafakari kwa undani falsafa hii ya Mwalimu na kuhakikisha wanawarithisha watoto wa sasa na vizazi vijavyo waweke Taifa lao la Tanzania mbele kuliko mambo mengine yoyote, hapo watakuwa wamemuenzi Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere.
No comments:
Post a Comment