Wanafunzi wa Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini, wakimuonesha Naibu Katibu Mkuu Fedha na Mipango, Dkt. Khatibu Kazungu, bidhaa walizobuni, wakati wa hafla ya kutoa vyeti kwa wanafunzi waliofanya vizuri kitaaluma, ubunifu na michezo, jijini Dodoma.
Mwanafunzi Rashid Sudi, akiwa amebeba kifaa cha kutambua iwapo gesi imepungua katika vifaa vya kuhifadhia, wa pili kulia ni Naibu Katibu Mkuu Fedha na Mipango, Dkt. Khatibu Kazungu akishuhudia.
Na Peter Haule, WFM, Dodoma
WAHITIMU wa vyuo mbalimbali nchini hususani wa Chuo cha Mipango ya Maendeleo vijijini, wametakiwa kuhakikisha wanatumia ubunifu na maarifa waliyoyapata ili kujikwamua kimaisha na kuchangia maendeleo ya nchi badala ya kujihusisha na ubadhilifu wa mali za umma na uzembe.
Rai hiyo imetolewa na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Dkt. Khatibu Kazungu, wakati wa mkutano wa 14 wa kitaaluma wa chuo hicho ambao ulienda sambamba na kutoa vyeti kwa wanafunzi waliofanya vizuri katika suala la taaluma, michezo na ubunifu.
Dkt. Kazungu alisema kuwa wahitimu wanatakiwa kufanya kazi kwa bidii, ubunifu, uadilifu na kujiepusha na vitendo vya rushwa ili kuweza kukidhi mahitaji ya Soko la ajira katika sekta binafsi na umma.
“Nawaasa vijana ambao wanatarajia kuhitimu katika ngazi mbalimbali chuoni hapa, watambue kuwa kuna changamoto za ajira hasa katika sekta ya umma ukilinganisha na idadi ya wahitimu kila mwaka, hivyo ni vema kutumia fursa zilizopo katika maeneo mbalimbali zikiwemo halmashauri kujikwamua kimaisha”, alieleza Dkt. Kazungu.
Alisema kuwa jambo ambalo ni muhimu vijana kulitambua hususani ambao wanaenda kujiunga kwenye soko la ajira ni kuwa Serikali kupitia Halmashauri zake imetenga fedha asilimia 10 kutoka katika mapato yake ya ndani kwa ajili ya kusaidia vikundi vya akina mama, vijana pamoja na watu wenye ulemavu. Ni wakati mwafaka kwa vijana ambao wanahitimu katika ngazi tofauti hususani katika Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini (IRDP) wakajiunga katika vikundi ili waweze kutumia asilimia nne kati ya 10 iliyotengwa ili kujikwamua kiuchumi.
“Nitoe wito kwa vijana kuhakikisha kuwa wanatumia fedha hizo kuendesha miradi yao kwa manufaa yao kwa kujikimu na kuliletea maendeleo taifa”, alisisitiza Dkt. Kazungu.
Aidha Dkt. Kazungu amewapongeza wahadhiri na wanajumuiya ya Chuo hicho kwa jitihada za kuwezesha wanafunzi kujiajiri kutokana na mafunzo yanayotolewa chuoni hapo hivyo kupunguza tatizo la ajira nchini.
Kwa upande wake Mkuu wa Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijiji, Prof. Hozen Mayaya, alisema kuwa miongoni mwa mambo ambayo chuo hicho kinajivunia ni kuanzishwa kwa kituo cha ubunifu ambapo vijana wanakuja na ubunifu wa aina mbalimbali ambao unalelewa na chuo na hatimaye kuweza kuutumia kujiajiri na kuajiri wengine.
Alisema chuo kinapitia mitaala iliyopo ili kuiboresha na kuweza kuifungamanisha na mahitaji ya soko hivyo kuwa na wataalamu wanaoweza kuisaidia Serikali kufikia malengo yake ya maendeleo.
Naye mwanafunzi mbunifu wa kifaa cha kutambua upungufu wa gesi katika vifaa vya kuhifadhia kutoka Chuo hicho Bw. Rashid Sudi, amekipongeza chuo hicho kwa kumpatia maarifa yaliyomuwezesha kuwa mbunifu na pia amewataka wanafunzi wenzake kuzitumia fursa zilizopo chuoni hapo kubuni vitu vitakavyosaidia kuchochea maendeleo na kupunguza changamoto ya ajira.
Jumla ya wanafunzi 77 wamepata zawadi mbalimbali, katika maeneo ya taaluma, michezo na ubunifu na kati ya hao wanafunzi 42 ni wanaume na 35 ni wanawake.
Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini Kampasi Kuu ya Dodoma, Desemba 3 mwaka huu kinatarajia kuwa na mahafali ya wahitimu wa ngazi tofauti za elimu takribani 8500 kuanzia ngazi ya Cheti, Diploma, Shahada ya kwanza na Shahada ya udhamili.
No comments:
Post a Comment