WAZIRI WA KILIMO PROFESA ADOLF MKENDA ATEMBELEA SHAMBA LA MICHIKICHI NCHINI UGANDA - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Friday, 26 November 2021

WAZIRI WA KILIMO PROFESA ADOLF MKENDA ATEMBELEA SHAMBA LA MICHIKICHI NCHINI UGANDA

Waziri wa Kilimo Prof. Adolf Mkenda alipotembelea kitalu cha kuoteshea miche ya michikichi katika shamba la Oil Palm Uganda Limited, katika ziara ya kikazi nchini Uganda. Kushoto ni Mkurugenzi wa maendeleo ya mazao wizara ya kilimo, Bw. Nyasebwa Chimagu,

Baadhi ya wafanyakazi wakipanda miche kwenye shamba la michikichi katika shamba la Oil Palm Uganda Limited nchini Uganda ambako Waziri wa Kilimo Profesa Adolf Mkenda alitembelea jana.

Miche iliyooteshwa katika shamba la Oil Palm Uganda Limited nchini Uganda.

Waziri wa Kilimo Prof. Adolf Mkenda akiangalia mbegu za mchikichi alipotembelea kitalu cha kuoteshea miche ya michikichi katika shamba la Oil Palm Uganda Limited, katika ziara ya kikazi nchini Uganda. Kushoto ni Mkurugenzi wa maendeleo ya mazao wizara ya kilimo, Bw. Nyasebwa Chimagu,

Na Mwandishi Wetu, KAMPALA

WAZIRI wa Kilimo, Prof. Adolf Mkenda, amezuru kikazi Uganda na kufanya mazungumzo na Waziri wa Kilimo, Mifugo, Viwanda na Uvuvi, Frank Tumwebaze pamoja na timu ya wataalamu kutoka Tanzania na Uganda. Katika ziara hiyo, Waziri Mkenda ameambatana na Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Kamishna wa Polisi Thobias Andengenye na wataalamu wa kilimo kutoka Wizara ya Kilimo na Mkoa wa Kigoma. Mkoa wa Kigoma ni miongoni mwa mikoa ya kimkakati katika uzalishaji wa zao la mchikichi nchini. Ziara hiyo imelenga kuimarisha uhusiano wa Uganda na Tanzania katika sekta ya kilimo ili kukuza tija ya uzalishaji wa mazao kwa kutumia mbinu bora za kilimo, ikiwa ni pamoja na kuimarisha utafiti wa kilimo na upatikanaji wa mbegu bora. Katika mazungumzo yao hayo jana Waziri Mkenda alieleza jitihada zinazofanywa na Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan za kukuza uchumi kwa kuimarisha uhusiano chanya na nchi jirani kama Uganda. “Tumekuja Uganda kwa kuwa tunafahamu sisi ni ndugu na uhusiano wetu una historia ndefu. Marais wetu wote wawili, Rais Yoweli Museven na Rais Samia Suluhu Hassan wanafanya kazi nzuri ya kuimarisha uhusiano uliopo na kukuza uchumi wa nchi zote mbili," alisema. Waziri Mkenda alisisitizia Wizara ya Kilimo ipo katika mkakati kabambe wa kuhakikisha nchi inaondokana na dosari ya uhaba wa mafuta ya kula na kutumia fursa ya ziara hiyo kujifunza namna ambavyo Uganda imepiga hatua kubwa ya kilimo cha michikichi. Alisema hatua hiyo itaongeza hamasa kwa uwekezaji mkubwa wa kilimo hicho nchini na kulimwa kwa tija na kupunguza uhaba wa mafuta ya kula kwa kiwango kikubwa na kushusha bei kwa mtumiaji. “Katika ziara hii nimeongozana na Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Kamishna wa Polisi Thobias Andengenye kwa kuwa Kigoma ni mkoa mmojawapo wa kimkakati kwa kilimo cha michikichi. "Kuja kwake huku kutawezesha kujionea na kujifunza ili kwenda kuwahamasisha wakulima wetu kulima kwa tija," Prof. Mkenda alisema. Ziara hiyo pia ilihusisha kutembelea mashamba makubwa ya mchikichi, viwanda vya uchakataji wa mafuta ya mawese na kujifunza mfumo mzima wa ulimaji na utunzaji wa mchikichi na hadi kupata mafuta ya mawese. Kampuni ya Wilmer yenye matawi katika nchi zaidi ya 25, ina nia ya kuongeza uzalishaji Tanzania katika kuzalisha mafuta yatokanayo na michikichi, alizeti na mazao mengine. Kampuni hiyo imejenga kiwanda cha mchele mjini Morogoro chenye uwezo wa kukoboa mpunga tani 200 kwa siku, kilichofunguliwa rasmi na aliyekuwa Rais wa Tanzania, Hayati Dk. John Pombe Magufuli mapema mwaka huu. Waziri wa kilimo, Mifugo, Viwanda na Uvuvi wa Uganda, Tumwebaze, alimshukuru Waziri Mkenda na timu yake kwa kuamua kutembelea Uganda na kuonyesha undugu na urafiki wa nchi hizo mbili. Aliongeza kuwa Uganda iko tayari kuendelea kuimarisha uhusiano na Tanzania katika sekta ya kilimo na kutaka wataalamu wa kilimo wa nchi zote mbili kuharakisha uundwaji kamati ya pamoja ya kilimo ili kutekeleza makubaliano ya ushirikiano wa pamoja katika kilimo yaliyotiwa saini Septemba 6, 2019 jijini Dar es Salaam. “Tumekubaliana nchi zetu kushirikiana katika mambo mbalimbali kwenye sekta ya kilimo ikiwa ni pamoja na uzalishaji wa mbegu bora, masoko, utafiti na mengineyo. "Tumefurahi sana kwa ujio huu wa Waziri wa Kilimo wa Tanzania kwa kuwa ni sehemu ya utekelezaji wa makubaliano hayo," alisema Waziri Tumwebaze. Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Wilmar anayesimamia Afrika, Santhosh Pilai, alisema kampuni hiyo iko tayari kuongeza uwekezaji mkubwa zaidi Tanzania ili kumhakikishia mkulima soko pamoja na kuondoa vikwazo vya uhaba wa mafuta ya kula Tanzania. “Tumefanya uwekezaji katika nchi zaidi ya 20 Afrika, Asia na Marekani na kwa Tanzania tuwekeza kiwanda kikubwa pale Morogoro na tunataka kuwekeza zaidi Tanzania. Zaidi ya vijana 400 wameajiriwa katika uwekezaji huo," alisema Pilai

No comments:

Post a Comment