Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo (WUSM), Mhe. Innocent Bashungwa.
Katibu Mkuu, Dkt. Hassan Abbasi. |
Na Adeladius Makwega, Dodoma-WUSM.
WAZIRI wa Utamaduni, Sanaa na Michezo (WUSM) Mhe. Innocent Bashungwa amewataka watumishi wa umma kufanya kazi kwa bidii ili kuhakikisha wanatimiza malengo ya Serikali inayosimamiwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan katika kuijenga Tanzania Mpya.
Mhe. Bashungwa ametoa kauli hiyo leo, Novemba 19, 2021 kwenye kikao kazi na watumishi kikiwa ni kikao cha kwanza tangu Wizara mpya ya Utamaduni, Sanaa na Michezo kuundwa rasmi hivi karibuni na Mhe. Rais ambapo kimejadili utekelezaji wa majukumu ya Wizara akiwa na Naibu wake, Mhe. Pauline Gekul, Katibu Mkuu, Dkt. Hassan Abbasi jijini Dodoma.
Amempongeza Katibu Mkuu wa Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa kuwa mbunifu ambapo amesema tayari uongozi wa Wizara umekaa pamoja na kujipanga ili kufanya kazi vizuri.
Waziri Bashungwa ametumia fursa hiyo kumshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhui Hassan kwa kutoa fedha takriban bilioni 22 kwa ajili ya ujenzi wa jengo la Wizara katika Mji wa Serikali Mtumba na kumuagiza Katibu Mkuu Dkt. Hassan Abbasi kuhakikisha jengo hilo limajengwa kwa ubora ambao utasaidia watumishi kuleta tija katika utendaji wao wa kila siku wa kuwahudumia watanzania kupitia sekta za Utamaduni, Sanaa na Michezo.
“Tuendelee kubuni vitu mbalimbali na tujiratibu vizuri ili tuweze kuwaratibu vizuri wadau wetu, tushirikiane kwa pamoja watumishi na viongozi hatua inayosaidia kufikia malengo ya Serikali” amesema Mhe. Bashungwa.
Mhe. Bashungwa ameongeza kuwa Wizara yake ipo mstari wa mbele na imefanikiwa kupiga hatua kwa kuzingatia msukumo wa kiasia ambao Serikali ya Awamu ya Sita inatoa kwa Wizara hiyo kwa kuzingatia umoja na mshikamano wa watumishi ambao unaifanya Wizara hiyo kusonga mbele.
Baadhi ya mafanikio hayo ni kuanzishwa kwa Mfuko wa Utamaduni na Sanaa, Mfuko wa Maendeleo ya Michezo, kupunguzwa kodi ya VAT kwa nyasi bandia kwenye viwanja vya Michezo, kurejeshwa kwa Taifa Cup pamoja na kurejeshwa kwa michezo ya Shule za Msingi (UMITASHUMTA) na Sekondari (UMISETA).
Aidha, amesema Wizara yake itaendelea kushirikiana na wizara nyingine kama TAMISEMI, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia ili kuhakikisha kuwa sekta za Utamaduni, Sanaa na Michezo zinafanikiwa.
Akizungumza katika kikao hicho, Naibu Waziri. Mhe, Pauline Gekul amesema kwa sasa nguvu ya Wizara zinaelekezwa katika sekta tatu zilizosalia baada ya kuondolewa kwa Sekta ya Habari ili ziweze kufanya vizuri zaidi.
“Mimi kama Naibu Waziri nitaendelea kushirikiana na Waziri wangu Mhe. Bashungwa, Katibu Mkuu na Watumishi wote ili kutekeleza Ilani ya CCM, kwa kuwa Wizara hii inagusa vipaji vingi vya Watanzania kazi yetu ni kuviunganishwa ili kupata fursa mbalimbali ndani na nje ya Tanzania yetu.” Amefafanua Mhe. Gekul
Awali Katibu wa Wizara hiyo, Dkt. Hassan Abbasi ametoa taarifa ya utekelezaji wa shughuli zote hususani kupandishwa madaraja, kulipa malimbizo ya madai, ununuzi wa vifaa mbalimbali ikiwamo magari ambayo yatawawezesha watumishi zaidi 182 kufanya kazi vizuri.
“Tumefanikisha watumishi 66 kulipwa malimbikizo ya sehemu ya madai yao na watumishi waliosalia wanaodai zaidi ya milioni 90 watalipwa stahiki zao, pia watumishi watapandishwa madaraja ambapo mpaka sasa watumishi 74 tayari wameshapandishwa madaraja na kulipwa nyongeza za mishahara yao.”
Katika kikao hicho watumishi kadhaa walipata nafasi ya kutoa ushauri, maoni na kuuliza maswali mbalimbali ambayo yalipokelewa na kupatiwa majibu ambayo yanafanya utekelezaji wa majukumu ya Wizara ipasavyolijibiwa.
No comments:
Post a Comment