Zanzibar, 18 Novemba, 2021 – Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Dkt. Hussein Ali Mwinyi ameipongeza Benki ya CRDB kwa kuanzisha huduma za kibenki zinazozingatia misingi ya kiislam “CRDB Al Barakah Banking,” akibainisha kuwa kupatikana kwa huduma hizo kupitia matawi ya Benki ya CRDB kutasaidia kuongeza ujumuishi wa kifedha visiwani humo na Tanzania kwa ujumla.
Rais Mwinyi amesema hayo katika hafla ya uzinduzi wa huduma hiyo uliofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Michenzani Mall na kuhudhuriwa na viongozi wa juu wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Benki Kuu ya Tanzania, Benki ya CRDB, pamoja na wateja wa benki hiyo na wananchi.
“Nafahamu wapo watu ambao walikuwa hawajajiunga na mfumo rasmi wa kibenki kutokana na kutokuwepo au kutopatikana kwa urahisi kwa huduma zinazoendana na imani yao ya kiislam. Huduma hii ya CRDB Al Barakah itakwenda kuwa jibu kwa changamoto zao na kuwawezesha kunufaika na huduma za kibenki,” alisema Rais Mwinyi.
Aidha aliwahimiza wananchi kutumia fursa zinazotolewa na Benki hiyo kupitia CRDB Al Barakah akisema zitawawezesha kunufaika na fursa za kiuchumi zilizopo nchini. Alisema kwa kiasi kikubwa maendeleo yanahitaji fedha ambazo zinaweza kupatikana aidha kwa kujiwekea akiba benki au kupitia uwezeshaji wa mikopo, hivyo ni vema wananchi wakitambua fursa hizo na kuzitumia vizuri kujipatia maendeleo.
“Jambo zuri ni kuwa kupitia huduma hii itawapa amani wale wote wanaotaka fedha zao walizohifadhi Benki zisitumike kwenye mambo ambayo yanakinzana na misingi ya dini ya kiislamu. Lakini pia kama tulivyosikia hapa uwezeshaji utakuwa ukifanyika kupitia mfumo usioambatana na riba wa kununua na kuuza kwa faida, kitaalamu inajulikana kama Murabaha,” aliongezea Rais Mwinyi akionyesha faida za huduma hiyo.
Naye Waziri wa Fedha na Mipango wa Serikali ya Mipinduzi ya Zanzibar, Jamal Kassim Ali alisema huduma za CRDB Al Barakah zitakwenda kuchochea utekelezaji wa mpango mkuu wa maendeleo ya sekta ya fedha uliozinduliwa mwaka jana 2020 ambao pamoja na mambo mengine umesisitiza katika upatikanaji wa huduma jumuishi za fedha.
“Kuanzishwa kwa huduma hii inayozingatia misingi ya dini ya kiislamu kutavutia watu wengi zaidi kujiunga, jambo ambalo litatoa msukumo mkubwa katika ujumuishi wa kifedha na kuongeza kasi ya mikopo kwa sekta binafsi, hivyo kuchochea kasi ya ukuaji wa uchumi,” alisema.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela alisema kuanzishwa kwa huduma ni matokeo ya kufanyia kazi maoni ambayo yamekuwa yakiwasilishwa na wateja na jamii. “Tukiongozwa na kaulimbiu yetu ya Benki inayomsikiliza mteja, tumekuwa tukipokea maoni kutoka kwa wateja na jamii moja wapo ikiwa ni hili la kuanzisha huduma zinazozingatia misingi ya dini ya kiislamu,” alisema Nsekela.
Nsekela alisema Benki hiyo inajivunia kuendelea kufanikisha mahitaji halisi ya wateja kupitia huduma hiyo ya CRDB Al Barakah ambapo alibainisha kuwa huduma hiyo sio tu kwa waislamu pekee kwani pia inatolewa kwa watu wengine ambao wanapenda kupata huduma zinazofuata misingi ya dini ya kislaamu.
Akielezea upatikanaji wa huduma hiyo, Nsekela alisema CRDB Al Barakah itakuwa ikipatikana katika matawi yote 268 ya Benki ya CRDB yaliyosambaa nchi nzima. “Ukiwa popote pale Tanzania huduma za CRDB Al Barakah zipo katika kukuwezesha kufanikisha malengo yako. Najua sote sisi niwachakarikaji hivyo hata katika mihangaiko yetu ya kutafuta riziki popote pale, hauhitaji kusubiria kupata huduma mpaka urudi wilay au mkoa fulani kupata huduma,” aliongezea.
Akitoa mada kuhusu huduma zinazopatikana kupitia CRDB Al Barakah, Mkuu wa Kitengo cha Islamic Banking Benki ya CRDB, Rashid Rashid alibainisha kuwa huduma zitakazotolewa ni pamoja na utunzaji wa amana ambapo kuna akaunti zaidi ya kumi na tano zinazogusa makundi mbalimbali ya wateja ikiwamo watoto, wanafunzi, wakinamama, wajasiriamali, wafanyabiashara na taasisi.
“Vilevile tutakuwa tukitoa huduma za uwezeshaji wa mikopo ya biashara, utekelezaji wa miradi, mikopo binafsi kwa wafanyakazi wa Serikali na sekta binafsi, pamoja na mikopo ya ujenzi wa nyumba kupitia mfumo usiombatana na riba, wa kununua na kuuza kwa faida, kitaalamu inajulikana kama Murabaha,” alisema Rashid.
Aliongezea kuwa ili kuhakikisha misingi inafuatwa Benki hiyo pia imeunda Bodi ya Ushauri na Usimamizi wa CRDB Al Barakah ambayo imejaa wataalamu na wabobezi wa huduma za kibenki zinazozingatia misingi ya dini ya kiislamu kutoka ndani ya nchi, ukanda wa Afrika Mashariki na duniani.
Katika hafla hiyo, Rais Mwinyi pia alipongeza jitihada zinazofanywa na Benki ya CRDB katika kusaidia mikakati ya maendeleo inayotekelezwa na Serikali yake ili kutimiza malengo ya uchumi wa buluu. Katika kipindi cha mwaka huu pekee, Benki ya CRDB imetoa zaidi ya shilingi bilioni 150 katika sekta mbalimbali za maendeleo visiwani humo ikiwamo sekta za utalii, kilimo, uvuvi, nishati, mawasiliano, miundombinu, elimu na afya.
Hivi karibuni Benki ya CRDB pia ilianzisha mpango wa kilimo unaotumia teknolojia kusaidia kukabiliana na mabadiliko ya hali ya tabianchi (TACATDP) na kufanikiwa kupata fedha kiasi cha dola za kimarekani milioni 100 kutoka Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Mabadiliko ya Tabianchi (GCF).
Rais Mwinyi alisema Benki hiyo imeonyesha uzalendo wa hali juu katika kubuni na kutekeleza mpango huo ambapo mbali na fedha zinazotolewa na GCF yenyewe pia imetenga dola za kimarekani milioni 100 na hivyo kufanya jumla ya fedha kufikia dola za kimarekani milioni 200 sawa na shilingi bilioni 460.
“Katika mpango huu sisi tutajikita zaidi kwenye malengo ya uchumi wa buluu ikiwamo usafiri wa uhakika baharini, uvuvi wa kisasa hasa kwenye bahari kuu ili kufaidi zaidi matunda ya bahari yetu inayotuzunguka pamoja na shughuli zetu mbalimbali tunazozifanya baharini,” alisema.
Rais wa Zanzibar, Dkt. Hussein Mwinyi na Mwenyekiti wa Baraza la
Mapinduzi, akipokea zawadi maalum ya ufunguzi kutoka kwa Mkurugenzi
Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela baada ya uzinduzi wa
huduma ya Benki ya CRDB inayozingatia misingi ya kiislamu ‘CRDB Al
Brakah,’ iliyofanyika katika ukumbi wa Michenzani Mall. Wengine pichani
kutoka kushoto ni Waziri wa Fedha Zanzibar, Jamali Kassim, Mkurugenzi
Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela, Mwenyekiti wa Bodi ya
Wakurugenzi Benki hiyo, Dkt. Ally Laay na Naibu Gavana wa Benki Kuu ya
Tanzania, Bernard Kibesse.
Rais wa Zanzibar, Dkt. Hussein Mwinyi na Mwenyekiti wa Baraza la
Mapinduzi, akipokea zawadi ya mafanikio ya mwaka wake mmoja madarakani
kutoka kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela
wakati uzinduzi wa huduma ya Benki ya CRDB inayozingatia misingi ya
kiislamu ‘CRDB Al Brakah,’ iliyofanyika katika ukumbi wa Michenzani
Mall. Wengine pichani kutoka kushoto ni ni Waziri wa Fedha Zanzibar,
katikati ni Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi Benki hiyo, Dkt. Ally
Laay.
No comments:
Post a Comment