MIFUMO YA KIDIGITALI TAHAFIFU KWA WADAU-WAZIRI BASHUNGWA - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Tuesday 23 November 2021

MIFUMO YA KIDIGITALI TAHAFIFU KWA WADAU-WAZIRI BASHUNGWA

Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Innocent Bashungwa.

Na Adeladius Makwega

WAZIRI wa Utamaduni, Sanaa na Michezo mheshimiwa Innocent Bashungwa amesema kuwa Uzinduzi wa mifumo wa Kidigitali wa BASATA, Bodi ya Filamu na COSOTA itasaidia sana upatikanaji wa huduma kama vile vibali vya Uhakiki wa filamu, Leseni za uendeshaji wa Kazi za Filamu, Vitambulisho na Vibali vya kurekodi filamu kwa haraka kwa wadau wa filamu sehemu yoyote yenye mtandao wa intanet hivyo kupunguza kero na usumbufu kwa wadau hao kusafiri hadi Dar es Salaam kufuata huduma hizo.

Kauli hiyo ya Mheshimiwa Bashungwa imetolewa Novemba 22, 2021 katika hafla ya uzinduzi wa mifumo hiyo, Uzinduzi wa Bodi ya Mfuko wa Utamaduni na Sanaa na  Uzinduzi wa Samia Taifa CUP uliwahusisha wadau utamaduni, sanaa na michezo mkoani Dar es Salaam.

“Waombaji wa vibali vya kuandaa filamu iliwachukua siku thelathini kupata kibali; lakini kupitia mfumo huu waombaji wa vibali vya nje watapata vibali ndani ya siku mbili na wale wa ndani watapata vibali ndani ya saa tatu (3), Kupitia mfumo huu, wadau wanaoomba kuhakiki kazi zao watapata huduma hii ndani ya siku mbili (3) lakini iliwachukua hadi siku thelathini kupata huduma hii.” Mheshimiwa Bashungwa alikumbusha.

Aliongeza kuwa Mfumo utatoa fursa ya kupata vibali kwa wasanii wanaofanya shughuli za sanaa nje ya nchi na kutowalazimu kurudi nchini pale inapobidi kuongeza muda wa vibali vyao au pale wanapokuwa wamepata fursa nyingine wakiwa hukohuko nje ya Nchi.


“Mfumo huu utasaidia upatikanaji na utunzaji wa takwimu za sekta ya filamu ambapo takwimu hizi zitasaidia katika kupanga mipango ya kuendeleza sekta kwa upande wa nyanja mbalimbali kama vile; mafunzo na uwezeshwaji”


Pia mfumo huu utapunguza gharama za uendeshaji kwa serikali zikiwemo gharama za uchapaji vyeti vya usajili na vibali vya uendeshaji wa shughuli za filamu na Michezo ya Kuigiza kwani vibali husika vitapatikani kupitia mfumo.

Akizungumza katika hafla hiyo Waziri wa Habari, Utamaduni, Vijana na Michezo wa Zanzibar Bi Tabia Mwita amesema kuwa anapongeza ushirikiano uliopo baina ya serikali hizi mbili.“Zanzibar itaendelea kutoa ushirikiana katika mambo haya kama la usajili kwa kutumia mfumo wa kidigitali na kuanza rasmi kwa Samia Taifa CUP kuwa yanaonesha umoja wetu kwa vitendo.” 


Awali akitoa neno la kumkaribisha Waziri Bashungwa, Katibu Mkuu wa WUSM Dkt Hassan Abbasi alisema kuwa Bodi ya Mfuko wa Utamaduni na Sanaa itawapa nafasi wasanii kupeleka maombi yao huko na yatapatiwa majibu.


“Uzinduzi wa Bodi hii leo unatoa nafasi ya mfuko huu kufanya kazi yake vizuri na upya ambao kwa hakika utawezesha wadau kupata mikopo na mafunzo na kusahau yaliyopita.”


Katika Hafla hiyo ilibainika kuwa Taifa Cup hapo awali ilikuwa inashirikisha mchezo wa soka tu na hata timu ya taifa ilikuwa na wachezaji kutoka  kila mkoa na sasa Taifa CUP itajumuisha kwa michezo zaidi ya mmoja yaani soka, mpira wa pete na riadha. Mashindano haya yatakusanya washiriki wa bara na Visiwani, kuanzia tarehe 10 hadi 21 Disemba 2021.  Huku nafasi ya kuongezeka kwa michezo zaidi ipo wazi na kamati kushauri juu ya michezo mipya zaidi.


Shughuli hii ni kwanza kufanyika tangu WUSM kuundwa rasmi ambapo imewakutanisha wadau zaidi ya mia mbili na ushehee wa sekta za utamaduni, sanaa na michezo.Huku Naibu Waziri wa WUSM Bi Pauline Gekul, Naibu Katibu Mkuu Dkt Ali Possi, Wakurugenizi, wakuu wa taasisi zilizo chini ya wizara hii, machifu na wadau kadhaa wakishiriki pia.


No comments:

Post a Comment