MHE. MARY MASANJA AKUTANA NA VIONGOZI WA VYAMA VYA WAFANYABIASHARA ZA UTALII RWANDA - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Wednesday 24 November 2021

MHE. MARY MASANJA AKUTANA NA VIONGOZI WA VYAMA VYA WAFANYABIASHARA ZA UTALII RWANDA

Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mary Masanja (Mb)(kushoto) akimsikiliza Mkurugenzi Mkuu, Idara ya Utalii ya Rwanda, Frank Mugisha (wa pili kutoka kulia) akitoa ufafanuzi wa namna Rwanda imekuwa ikishirikiana na Tanzania kuboresha sekta ya utalii katika kikao kilichofanyika Hoteli ya Kigali Serena nchini Rwanda. Kulia ni Kaimu Mkurugenzi, Idara ya Utalii kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii, Philip Chitaunga na Msaidizi wa Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Sikujua Mfangavo (wa pili  kutoka kushoto)

Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mary Masanja (Mb) (kulia) akimsikiliza Mwenyekiti wa Jumuiya ya Utalii na Usafiri ya Rwanda, Bonita Mutoni (katikati) akielezea kuhusu umuhimu wa nchi za Tanzania na Rwanda kujitathmini zinaposhiriki maonesho kutangaza utalii,katika kikao kilichofanyika Hoteli ya Kigali Serena nchini Rwanda. Kushoto ni Afisa Masoko Mkuu kutoka Bodi ya Utalii Tanzania, Bernard Mtatiro akifuatilia mazungumzo.

Na Happiness Shayo - Rwanda

NAIBU Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mary Masanja (Mb) amefanya kikao na viongozi wa vyama vya wafanyabiashara za utalii nchini Rwanda kwa lengo la kujadili namna bora ya kuboresha, kukuza na kuendeleza sekta ya utalii nchini Tanzania.

Kikao hicho kimefanyika katika hoteli ya Kigali Serena nchini Rwanda mapema leo.

Akizungumza katika kikao hicho, Mhe. Mary Masanja amekubaliana na viongozi wa vyama vya wafanyabiashara za utalii nchini Rwanda kutafuta namna bora ya kuwaunganisha wadau wa utalii wa Rwanda na wa Tanzania ili kukuza utalii wa nchi zote mbili.

Katika majadiliano hayo, Mhe. Mary Masanja amepata ufafanuzi kutoka kwa viongozi hao kuhusu namna ambavyo Serikali ya Rwanda inashirikiana na sekta binafsi katika kuendeleza utalii na mbinu ambazo Serikali hiyo inatumia kupata wawekezaji hasa katika utalii wa mikutano. 

Naye Mwenyekiti wa Jumuiya ya Utalii na Usafiri ya Rwanda, Bonita Mutoni amezishauri Serikali za Tanzania na Rwanda kujitathmini kama ushiriki wao katika maonyesho mbalimbali unaleta manufaa kwa mataifa hayo ili kujua maeneo ya kuyaboresha ili kukuza utalii.

“Tunahitaji kushiriki katika mikutano na maonesho mbalimbali lakini ni lazima tujiulize wapi tunakosea ili tujirekebishe” Bi. Mutoni amesisitiza.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu, Idara ya Utalii ya Rwanda, Frank Mugisha amesema kuwa ofisi yake imekuwa ikifanya kazi na Tanzania kupitia Chama cha Mawakala wa Utalii Tanzania (Tanzania Association of Tour Operators) ambacho hushirikiana na Serikali ya Ujerumani katika utunzaji wa Hifadhi za wanyamapori hasa kwenye  Hifadhi ya Taifa ya Serengeti.

Wafanyabiashara hao wamependekeza kwamba mwaka 2022 Serikali ya Tanzania na Rwanda iandae maonesho ya road shows kwa pamoja katika nchi za Ulaya ambako kuna wanunuzi wakubwa wa vivutio vya utalii lengo ikiwa ili kutangaza vivutio vya utalii vya nchi zote mbili kwa kauli mbiu ya “Visit Tanzania and Rwanda” .

Aidha, wafanyabiashara hao wameahidi kuitembelea Tanzania mwezi Desemba mwaka huu kwa lengo la  kujifunza zaidi kuhusu vivutio vya utalii na maeneo ya uwekezaji yaliyopo nchini Tanzania ili waweze kuwekeza, kuviuza  vivutio hivyo na pia  kuvisemea kwenye biashara zao.

Kikao hicho kimehudhuriwa na watumishi kutoka Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA), Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), Hifadhi za Taifa Tanzania  (TANAPA), Mamlaka ya Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro.

No comments:

Post a Comment