KIWANJA CHA NDEGE CHA MUSOMA KUKAMILIKA MWAKANI - KASEKENYA - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Thursday, 18 November 2021

KIWANJA CHA NDEGE CHA MUSOMA KUKAMILIKA MWAKANI - KASEKENYA

Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Eng. Gofrey Kasekenya (katikati), akisisitiza jambo alipokagua ujenzi wa  kiwanja cha ndege cha Musoma ambacho ujenzi wake unaendelea (kulia), ni Mkuu wa wilaya ya Musoma Dkt. Khalfan Haule na kushoto ni Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS), mkoa wa Mara Eng. Vedastus Maribe.

Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS), mkoa wa Mara Eng. Vedastus Maribe akimuonesha Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Eng. Gofrey Kasekenya (katikati), eneo la kiwanja cha ndege cha Musoma ambacho ujenzi wake unaendelea alipokagua maendeleo ya ujenzi huo (kulia), ni Mkuu wa wilaya ya Musoma Dkt. Khalfan Haule.

Muonekano wa kiwanja cha ndege cha Musoma ambacho upanuzi wake wa kukiwezesha kuwa na urefu wa mita 1,705 na upana wa mita 30 unaendelea.

Muonekano wa barabara ya Bulamba-Kisorya (KM 51), ambayo ujenzi wake kwa kiwango cha lami umekamilika barabara hiyo ni sehemu ya barabara ya Nyamuswa-Bunda-Kisorya-Nansio (KM 121.9), ambayo ujenzi wake kwa kiwango cha lami unaendelea mkoani Mara.



Meneja wa wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA), mkoa wa Mara Eng. Vitalis Bilaul akifafanua jambo kwa Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Eng. Gofrey Kasekenya alipokagua kivuko cha MV. Musoma kinachotoa huduma kati ya Mwigobero na Kinesi mkoani Mara.

Meneja wa wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA), mkoa wa Mara Eng. Vitalis Bilaul akifafanua jambo kwa Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Eng. Gofrey Kasekenya alipokagua kivuko cha MV. Musoma kinachotoa huduma kati ya Mwigobero na Kinesi mkoani Mara.

NAIBU Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Eng. Godfrey Kasekenya amesema ujenzi wa kiwanja cha ndege cha Musoma utakamilika mwakani hivyo wakazi wa mkoa wa Mara wajipange vizuri kunufaika na fursa zote za ujenzi na matumizi ya kiwanja hicho.

Akikagua upanuzi na ujenzi wa kiwanja hicho kwa kiwango cha lami Eng. Kasekenya amesema lengo la Serikali kurefusha kiwanja hicho na kukijenga kwa viwango vya kisasa ni kuwezesha ndege kubwa  kutua na hivyo kuufungua mkoa wa Mara kwa kuongeza tija katika utalii wa hifadhi ya taifa ya Serengeti.

“Kiwanja hiki kitakapokamilika kitakuwa na urefu wa mita 1,705 na upana wa mita 30 na hivyo kuwezesha ndege nyingi kukitumia na hivyo kuvutia watalii wanaokwenda Serengeti”, amesema Eng. Kasekenya.

Naibu Waziri huyo amemtaka mkandarasi anayejenga kiwanja hicho Beijing Construction Engineering Group (BCEG), kuzingatia ubora na kukamilisha kazi kwa wakati.

Naye Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS), mkoa wa Mara Eng. Vedastus Maribe amesema zaidi ya shilingi bilioni 3, za fidia zimeshalipwa na hivyo watahakikisha ujenzi unakuwa wa viwango na unakamilika kama ilivyopangwa.

“Tumejipanga vizuri kupitia msimamizi wa maradi huu (TECU),kuhakikisha mradi unakamilika mapema na kwa viwango vya kimkataba hivyo tunawaomba wananchi watupe ushirikiano”, amesisitiza Eng. Maribe.

Katika hatua nyingine Naibu Waziri Kasekenya ametoa siku saba kwa Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA), mkoa wa Mara kukutana na Mtendaji mkuu wa Wakala huo ili kupitia upya gharama za ujenzi wa jengo la kupumzikia abiria katika eneo la Mwigobero-Musoma ambazo ameelezea kutokuridhishwa nazo.

Amesema hakubaliani na kiasi cha shilingi milioni 86, zilizopangwa kutumika kwani ni kubwa kuliko matarajio ya jengo na eneo husika.

Aidha, amemwagiza Meneja wa TEMESA mkoa wa Mara Eng. Vitalis Bilaul kuhakikisha changamoto za kivuko cha MV. Musoma kinachotoa huduma kati ya Mwigobero na Kinesi zinapatiwa ufumbuzi haraka ili kupunguza adha za usafiri kwa wananchi hususan kipindi cha mvua.

Naibu Waziri Kasekenya yuko katika ziara ya siku mbili kukagua miradi ya ujenzi katika mkoa wa Mara.

IMETOLEWA NA KITENGO CHA HABARI NA MAWASILIANO SERIKALINI WIZARA YA UJENZI NA UCHUKUZI


No comments:

Post a Comment