WANAWAKE NI MUHIMU KATIKA MAENDELEO YA TAIFA : RAIS PUTIN - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Friday, 15 October 2021

WANAWAKE NI MUHIMU KATIKA MAENDELEO YA TAIFA : RAIS PUTIN

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Dorothy Gwajima akizungumza na wataalam wake mara baada ya ufunguzi wa Kongamano la Wanawake nchini Urusi ambapo Rais wa nchi hiyo Vladimir Putin alihutubia Kongamano hilo.

Na WAMJW-St. Petersburg, Urusi

RAIS wa Urusi Vladimir Putin ameonesha kuwa wanawake ni muhimu katika maendeleo ya taifa lolote kulingana na asili ya majukumu yao wanayoyafanya hasa katika malezi kwa mtoto. Hayo yamebainishwa na Waziri wa Afya, Maendelo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Dorothy Gwajima mara baada ya kushiriki kwenye Kongamano la tatu la Wanawake lililofunguliwa na Rais huyo na kuhudhuriwa viongozi wa mataifa mbalimbali nchini hapa.

Dkt. Gwajima amesema kuwa Rais huyo  amebainisha kwamba ni namna gani wanawake ni muhimu katika hatua za awali za malezi na makuzi ya mtoto ambapo mambo mengi ya msingi ambayo mtoto anapaswa kupatiwa katika msingi wa makuzi yake mwanamke anahusika moja kwa moja kwani muda mwingi anakuwa na mtoto katika malezi yake.

“Rais Putin amerejea mfano wa taifa la Urusi ambalo linafanya vizuri katika kuwapa nafasi  Wanawake waweze kushiriki kwenye maendeleo ya nchi na jinsi gani Wanawake wanapewa fursa katika nyanja zote za maendeleo la taifa kwa sekta zote.

“Tumeweza kujifunza kwamba hata sisi nyumbani muelekeo anaochukua Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan wa kuwajenga na kuwawezesha wanawake katika nyanja zote wasiachwe nyuma ni muelekeo sahihi kwani imejionesha katika nchi kubwa kimaendeleo duniani ziliweza kuona msingi mzima wa nafasi ya mwanamke katika kuchangia maendeleo ya jamii”.

Dkt. Gwajima ameongeza kuwa wanawake ndio wanaoleta Taifa kuwa na sura fulani na  tabia nyingi wanazorithi watoto wetu wakiwa wadogo zinabaki katika kumbukumbu zao na ndizo zinazojenga taifa mbele ya safari.

Waziri Dkt. Gwajima amesema kuwa Rais Putin amewapa changamoto hivyo wanaporudi Tanzania lazima wakafanyie kazi kwa nguvu ili dhamira ya Mhe. Rais Samia ya kuwatoa wanawake wengi ambao wapo nyuma na hawana nafasi nzuri kimaendeleo  wapande juu na wachangie maendeleo ya taifa.

Hata hivyo Dkt. Gwajima ameahidi kutokana na Kongamano hilo Serikali ya Tanzania itajipanga kuwa na kongamano la Wanawake kupitia Majukuwaa  ya Uwezeshaji Wanawake Kiuchumi ambayo yapo kwenye ngazi za halmashauri hadi Mikoa ili kuweza kujiandaa kwa miaka inayokuja kuwasilisha yatokanayo na kongamano hili na hata kuwaalika mwanawake wa mataifa mengine wafike Tanzania na kuona mafanikio yatakayofikiwa na wanawake wa Tanzania.

Wakati huo huo akizungumza na Kituo cha Runinga cha Serikali cha “Russia One” Dkt. Gwajima alibainisha kuwa Tanzania ipo salama kutokana na ugonjwa wa UVIKO-19 na kwamba idadi ya maambukizi yamepungua huku akitolea mfano kati ya  tarehe 2  hadi 8 mwezi Oktoba Tanzania iliandikisha kesi mpya  77 na wagonjwa 171 ndio waliokuwa wamelazwa ukilinganisha na idadi ya watu waliopo na hivyo kuwaondoa hofu wananchi wa Urusi na kuwathibitishia mipaka ya Tanzania ipo wazi hivyo hamna haja ya kufungia ndege zao kuruka Tanzania na za Tanzania kuruka Urusi.

Kwa upande wa utalii Waziri huyo aliwathibitishia Urusi kuwa Tanzania inapokea idadi kubwa ya watalii  kutoka mataifa mbalimbani na kwamba idadi ya watalii kuanzia Mwezi Agosti hadi Februari, 2021 zaidi ya watalii laki moja (100,000) waliweza kuingia Tanzania na waliondoka wakiwa salama.

Akielezea kuhusu Madini Dkt. Gwajima alisema Tanzania ndio nchi Pekee duniani kuwa na  madini ya Tanzanite na ni moja ya vito adimu na yenye thamani ambayo huchimbwa  kaskazini mwa nchi katika eneo la Mirerani wilayani Simanjiro mkoani Manyara hivyo kuwaalika wawekezaji kutoka nchini Urusi kuwekeza katika Sekta hiyo.

No comments:

Post a Comment