UTAKATIFU WA NYERERE NA MATOKEO YA SHUFAA - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Thursday 14 October 2021

UTAKATIFU WA NYERERE NA MATOKEO YA SHUFAA

 


Julius Nyerere

Adeladius Makwega, Dodoma.

“Ninakufa kama mtumishi mwadilifu wa mfalme lakini huku nikimtanguliza Mungu kwanza.” Haya yalikuwa maneno ya mwisho ya Mtakatifu Thomas More wakati akinyongwa huku awali akiomba binti yake akabidhiwe mwili wake akauzike baada ya kunyongwa kwa kosa la uhaini.

Kanisa Katoliki lina watakatifu wengi ambao wanatambulika lakini kuna hoja moja juu ya watakatifu wachache ambao walikuwa wanasiasa kuweza kupita katika mchakato wa kumpata mtakatifu, miongo mwa watakatifu waliowahi kufanya siasa na kupenya katika mchakato huo ni huyo niliyemnukuu maneno yake ya buriani, Mtakatifu Tomas More, aliyezaliwa Februari 7, 1478 na kufariki Julai 6 1535.

Thomas More alikuwa Mwingereza akitumika kama kiongozi wa serikali katika ofisi ya mfalme, mwandishi, mwanafalsafa wa kijamii, mwanasheria, jaji, msaidizi wa mfalme na mbunge. 

Oktoba 14, 2021 ni siku ya kumbukumbu ya kifo cha mwalimu Julius Nyerere ambaye na yeye Kanisa Katoliki linampitisha katika mchakato wa kuelekea kutangazwa mtakatifu na kwa sasa ikifikia katika hatua ya pili ya Mtumishi wa Mungu huku tangu afariki dunia sasa anatimiza miaka 22.

Unaposema miaka 22 maana yake ni kuwa wapo Watanzania wengi waliozaliwa baada ya kifo cha Julius Nyerere wakimsoma Mwalimu Nyerere katika maandishi tu kama ilivyo kwa mimi na wengine wenye umri kama wangu tunavyosoma juu ya Chifu Mangungo wa Msowelo, Karl Peters na Edward Twining.

Swali langu la leo ni moja tu lenye pande mbili je, Nyerere kuwa mtakatifu au la kupi kuna faida kwa Watanzania?

Kwa nini Nyerere awe mtakafifu? Hapa kuna hoja kadhaa kwa wanaoliunga mkono hili wanadai kuwa uwezo wa Julius Nyerere wa kuwaunganisha Watanzania na kuwaweka pamoja na kutetea mno maslahi ya wanyonge, hiki ni kigezo kikubwa mno ambacho hakina ubishi. 

Je ni hayo tu? La hasha, katika hili wanataja kuanzishwa kwa vijiji vya ujamaa kupeleka huduma kadhaa kama vile shule, zahanati, maji na kutoa elimu kwa jamii nzima ya Watanzania masikini. Huku akipigania ukombozi wa Bara zima la Afrika.

Lakini wale wanaosema la!, Wanasemaje? Wao wanasimama katika kazi hizo hizo alizofanya mara baada ya uhuru na baada ya muungano. Katika jambo hili wanataja haswa migogoro ya Zanzibar kushindwa kutatuliwa na vifo vilivyotokea katika kipindi chake. Hapa wanatajwa watu kadhaa waliofariki katika mgogoro huo chini ya Zanzibar ya Abeid Karume  na kadhalika hasa kwa kushindwa kumzuia Abeid Karume katika baadhi ya matukio hayo kwa mfano kifo cha Abdalla Kassimu Hanga ambaye alikuwa Waziri Mkuu wa kwanza wa Zanzibar baada ya mapinduzi ya 1964 na majina mengine yakitajwa pia.

Pia wakati wa harakati za kupigania uhuru huku kukiwa na baadhi ya wapigania uhuru  hao kupotea wakiwa ndani ya ardhi ya Tanzania mathalani Makamu wa Rais wa Frelimo Mchungaji Uria Simango na mkewe Celina Simango ambao walikuwa miongoni mwa waanzilishi wa FRELIMO baada ya kifo cha marehemu  Profesa Eduado Mondulane.

Vifo vya baadhi ya watu wakati wa utekelezaji wa zoezi la vijiji vya Ujamaa, kuendelea kutekelezwa kwa hukumu ya kifo katika utawala wake. Kusaini hati za kunyongwa kwa baadhi ya watu waliotiwa hatiani kwa hukumu ya kifo na hata kuziacha sheria hizo mathalani ya hukumu ya kifo kuwa ni sheria halali katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Ndiyo kasema kama akifanikiwa kuwa mtakatifu basi yale ambayo yanatajwa kama mazuri yake yatakuwa yameshinda yale yanayotajwa kama mabaya. Kwa hiyo utakatifu wa Nyerere utakuwa shufaa ya yale yanayotajwa kama makosa yake.

Kwa hiyo Watanzania wanaweza kutambua kuwa kuna umuhimu wa kutenda mema. Kwa kuwa kuna wakati dunia inaweza kutambua hilo miaka kadhaa baada ya mhusika kufariki.

Wengine wakisema kuwa kitendo cha kauli za Nyerere za kuheshimu uhai wa binadamu na kupinga hukumu ya kifo baada ya kutoka madarakani kinaweza kusaidia kubadilisha mtazamo wa Kanisa Katoliki katika kulinda uhai dhidi yake na hiyo kuwa toba kwake.

Lakini kama jina hilo litatupwa na kuishia katika hatua za awali hiyo pia jamii ya Kitanzania na viongozi watatambua yale madhaifu ambayo pengine alikuwa akitajwa kuyafanya iwe kwa mkono wake, kuweka saini au kutoa kauli na maagizo yataonekana kuwa hayafai kwa kuwa hata ulimwengu unaungana na wale waliokuwa  wakiamini kuwa Julius Nyerere alikuwa mtu mwovu.

Naweka kalamu yangu chini kwa siku ya leo kwa kusema kuwa Julius Nyerere kuwa mtakatifu au la kote kote kuna faida kwa Tanzania.

makwadeladaius@gmail.com

0717649257

No comments:

Post a Comment