Muonekano wa sehemu ya Barabara ya Katoro–Kyamulalile–Kashaba yenye urefu wa kilomita 15.7 kwa kiwango cha changarawe inayounganisha Kata ya Katoro na Kyamulalile katika Halmashauri ya Wilaya ya Bukoba mkoani Kagera ili kutatua kero ya muda mrefu na kuwezesha wananchi kusafiri kwa urahisi.
Muonekano wa Daraja la Nyikonga lenye urefu wa mita 32 katika Barabara ya Kasemo-Nyamalulu-Mbogwe linalounganisha Kata ya Magenge na Lulembela katika Halmashauri ya Wilaya ya Geita mkoani Geita likiwa limekamilika.
Na Geofrey Kazaula na Bebi Kapenya
WAKALA wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) umeendelea kufungua barabara katika maeneo mbalimbali nchini ili kuwezesha wananchi kufika sehemu mbalimbali ambazo hapo awali zilikuwa hazifikiki.
Katika Wilaya ya Mbogwe mkoani Geita, pamoja na miradi mingine TARURA inaendelea na ujenzi wa barabara ya Mzambarauni–Budoda kwa kukarabati eneo korofi lenye urefu wa mita 800 kwa kiwango cha changarawe ili iweze kupitika katika kipindi chote cha mwaka.
Kwa mujibu wa Meneja wa TARURA Wilaya ya Mbogwe, Mhandisi Justin Lukaga barabara hiyo ya Mzambarauni-Budoda itasaidia wananchi kutoa mazao yao mashambani na kusafiri kwa urahisi kutoka Ushetu kwenda Masumbwe, na pia itawasaidia katika kuendesha shughuli za uchimbaji wa madini.
’’Barabara hii itakapokamilika hasa kwa kipande hiki korofi itarahisisha shughuli za kiuchumi kwa wananchi maana kuna shughuli za kilimo na uchimbaji wa madini”, alisema Mhandisi Justin.
Katika Wilaya ya Geita, TARURA imekamilisha ujenzi wa daraja la Nyikonga lenye urefu wa mita 32 katika barabara ya Kasemo-Nyamalulu-Mbogwe linalounganisha Kata ya Magenge na Lulembela ambapo hapo awali wananchi walitegemea kuvushwa kwa kulipa fedha na sasa wanavuka bila shida.
Meneja wa TARURA Wilaya ya Geita, Mhandisi Bahati Mtumwa amesema kuna shughuli za uchimbaji wa madini na kilimo zinazotegemea uwepo wa barabara hiyo na kwamba kwa sasa wananchi wanaendelea na shughuli zao za biashara bila shida.
Maeneo mengine yaliyofunguliwa na TARURA ni pamoja na barabara ya Kimeya- Kyamiyorwa yenye urefu wa kilomita 9.8 kwa kiwango cha changarawe katika Halmashauri ya Wilaya ya Muleba Mkoani Kagera ambapo kwa mujibu wa Meneja wa TARURA Wilaya ya Muleba, Mhandisi Dativa Telesphory barabara hiyo imefunguliwa ili kuwasaidia wananchi kuzifikia huduma za kijamii kwa urahisi.
Diwani wa Kata ya Kasharunga Wilaya ya Muleba Mkoani Kagera, Mhe. Theobard Michael amesema kuwa hapo awali wananchi walilazimika kutumia Shillingi 5,000 hadi 10,000 kukifikia kituo cha Afya Kimeya lakini baada ya kufungua barabara sasa wanatumia 1,000 hadi 2,000 ambapo pia barabara hiyo inategemewa kwa shughuli za kilimo na biashara.
’’Mwendo ulikua mrefu kwa sababu kabla ya kufungua barabara hii, wananchi walilazimika kutembea hadi kilomita 20 lakini sasa kufunguliwa kwa barabara hii tumepata njia ya mkato suala linalorahisisha shughuli za kiuchumi na kijamii kwa wananchi’’ amesema Mhe Theobard.
Maeneo mengine yaliyofunguliwa kwa Mkoa wa Kagera ni pamoja na barabara ya Katoro–Kyamulalile–Kashaba yenye urefu wa kilomita 15.7 kwa kiwango cha changarawe iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Bukoba ambapo katika barabara hiyo kuna eneo korofi lenye urefu wa kilomita 3.7 linaloendelea kujengwa na TARURA ili kuwezesha wananchi kusafiri kwa urahisi.
Ili kuwezesha shughuli za uvuvi kufanyika kwa urahisi, TARURA Manispaa ya Bukoba imefungua barabara ya Bunena-Kalobela yenye urefu wa mita 400 kwa kiwango cha ambayo hapo awali haikuwepo hivyo itarahisisha shughuli za uvuvi na biashara.
Kaulimbiu ya Kufungua Barabara Kufika Kusiko Fikika imewafikia pia wananchi wa Kata za Rwamishenyi na Nshambya Bukoba mjini baada ya kuanza ujenzi wa daraja la Kyebitembe lenye urefu wa mita 18 litakalounganisha Kata hizo kwa lengo la kufungua mji na kusaidia huduma za kijamii kama shule na zahanati.
Katika Halmashauri ya Wilaya ya Kyerwa TARURA inaendelea na ujenzi wa barabara ya Nyaruzumbura–Kishanda B yenye urefu wa mita 240 kwa kiwango cha changarawe ili kurahisisha usafiri kwa wananchi.
Mbunge wa Jimbo la Kyerwa, Mhe. Innocent Bilakwate ameipongeza TARURA kwa kuendelea kufungua barabara na kuwafikia wananchi.
’’ TARURA inafanya kazi nzuri, katika Jimbo la Kyerwa maeneo mengi yalikuwa hayapitiki lakini kwa sasa yanapitika na kazi inaendelea katika maeneo mbalimbali”, amesema Mhe. Bilakwate.
Kwaupande wake Meneja wa TARURA Mkoa wa Kagera, Mhandisi Avith Theodory amesema kuwa lengo la Wakala katika Mkoa huo ni kuhakikisha maeneo yenye changamoto yanafanyiwa kazi ili kuhakikisha wananchi wanazifikia huduma za kijamii kwa urahisi.
No comments:
Post a Comment