LHRC YATOA WITO KWA SERIKALI MAADHIMISHO YA SIKU YA HAKI ZA BINADAMU AFRIKA - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Friday, 22 October 2021

LHRC YATOA WITO KWA SERIKALI MAADHIMISHO YA SIKU YA HAKI ZA BINADAMU AFRIKA

Mkurugenzi Mtendaji wa kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Anna Henga akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, kuhusu maadhimisho ya siku ya haki za bianadamu Afrika. Kulia ni Afisa Uchechemuzi wa kituo hicho, Raymond Kanegene.

Mkurugenzi Mtendaji wa kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Anna Henga akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, kuhusu maadhimisho ya siku ya haki za bianadamu Afrika. Kulia ni Afisa Uchechemuzi wa kituo hicho, Raymond Kanegene.

KITUO cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kimetumia maadhimisho ya siku ya haki za binadamu katika Bara la Afrika ya mwaka huu kuiomba Serikali ya Tanzania kufikiria upya uamuzi wa kujitoa katika ibara ya 34(6) ya Mkataba wa Nyongeza wa Afrika wa Haki za Binadamu.

Itakumbukwa kwamba mnano tarehe 21 Novemba mwaka 2019 Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ilifanya uamuzi wa kujitoa katika ibara ya 34(6) ya Mkataba wa Nyongeza wa Afrika wa Haki za Binadamu na Watu ambayo ilikuwa inaruhusu mtu au taasisi yoyote kuifikia mahakama ya Afrika pale ambapo kuna uhitaji wa kudai haki yake katika Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu. 

Akizungumza na wanahabari leo jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Bi. Anna Henga alisema uamuzi huo ulishangaza wapenda haki nchini kwa Serikali kujitoa katika kipengele hicho muhimu ambacho kiliweka njia ya kufikia haki. 

“LHRC inapenda kutumia maadhimisho haya kutoa wito kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia upya uamuzi wake wa kujitoa katika mkataba huo kwani itarudisha na kuimarisha heshima ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika uwanda wa kikanda.”

“Tanzania imekuwa nchi ya pili baada ya Rwanda kujitoa katika mkataba huo unaoruhusu mtu au taasis kufungua kesi dhidi ya Serikali pale ambapo kuna malalamiko ya kuvunjiwa haki yake. Ni wazi kwamba, watu pamoja na taasisi walitumia vizuri uwepo wa mkataba huo kwa kufungua kesi mbalimbali dhidi ya Serikali kwa kuhitaji mabadiliko ya sheria, sera pamoja na mienendo kwa nchi ya mahakama,” alisema Wakili Henga.

Aidha alisema tafsiri ya kwamba, watu waliyofungua kesi katika Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu hawana nia nzuri na serikali kwa lengo la kuichafua, si sahihi kwani ni ishara ya kuimarika kwa demokrasia, ufikiaji wa haki, uvumilivu, na uongozi bora unaonyeshwa na Serikali kwa kuruhusu watu au taasisi kufungua kesi dhidi ya serikali. 

“Ndugu wanahabari, LHRC inaona kwaba, bado Tanzania inaweza kurudi katika Mkataba huo na kuruhusu wananchi kufikia mahakama hiyo kwa lengo la kufikia mahakama na kupata mustakabali wa haki zao. LHRC inaamini kwamba muundo wa Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu iliyopo Arusha hapa nchini ni wenye watu wenye kujua misingi  ya kiafrika, tamaduni, taratibu sheria pamoja na mazingira, hivyo kwa vyovyote vile maamuzi yanayotolewa na mahakama hiyo ni maamuzi ya haki na usawa.”

Pamoja na hayo, aliishauri Serikali kuendeleza utamaduni wa kuripoti hali ya haki za binadamu kwa Umoja wa Afrika kupitia mfumo wa Mapitio ya Haki za Binadamu Afrika yaani African Peer Review Mechanism (APRM). Mara ya mwisho, ripoti ya mapitio ya hali ya haki za binadamu ilitolewa mwaka 2013 ambapo utekelezaji wake ulianza rasmi 2014. Hivyo ni vema kuendeleza utamaduni huu kwani unaimarisha na kukuza misingi ya haki za binadamu nchini. 

No comments:

Post a Comment