Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mheshimiwa Othman Masoud Othman akiwa katika ziara yake. |
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mheshimiwa Othman Masoud Othman akiwa katika ziara yake. |
MAKAMU wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mheshimiwa Othman Masoud Othman, amesema suala la athari za mazingira na mabadiliko ya tabianchi ni la kidunia, ambapo nchi za visiwa zinabaki kuwa waathirika wakubwa, bali la msingi ni kuweka sera na mipango makini ya kuyalinda.
Mheshimiwa Othman ameyasema hayo leo katika ziara yake ya Wilaya mbili za Mkoa wa Kaskazini Unguja, akiangalia athari za kimazingira zinazotokana na mabadiliko ya tabianchi.
Amesema pamoja na juhudi mbali mbali zinazosimamiwa na serikali, asasi za kiraia, vikundi vya ushirika na watu binafsi, bado kuna haja ya kufuata mbinu za kitaalamu na njia mbadala za kuyalinda na kuyatunza maeneo, ikizingatiwa kuwa mazingira ni uhai na njia ya maisha ya kila siku, kwa watu kujitafutia riziki.
Mheshimiwa Othman ameeleza azma ya Serikali ya Awamu ya Nane ya Zanzibar, ya kufanya mapitio na marekebisho makubwa ya sera na sheria, yatakayopelekea kuandaa mipango imara ya kuwawezesha wananchi kiuchumi ili kuyaokoa mazingira, ambayo kwa sasa yanakabiliwa na tishio kubwa la uharibifu sambamba na athari za mabadiliko ya tabianchi.
Mheshimiwa Othman, katika ziara yake hiyo aliweza kuyatembelea maeneo mbali mbali yakiwemo ya utunzaji wa misitu chini ya Jumuiya ya Mazingia ya Fujoni (JUMAFU), Shimo la Mchanga la Donge Mchangani, Eneo la Waanika Madagaa la Fungu-Refu, Uendeshaji wa Hoteli unaozingatia utunzaji wa mazingira Kijiji cha Kendwa, Majengo yaliyobomolewa na bahari kutokana na athari za mabadiliko ya tabianchi jirani na Soko la Samaki la Nungwi, na Machimbo ya Mawe na Kokoto ya Kandwi, yote katika Mkoa wa Kaskazini Unguja.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Unguja, Bw. Ayoub Mohamed Mahmoud, amesema licha ya changamoto katika utunzaji wa mazingira, zikiwemo za ukosefu wa vifaa, nyenzo na ufinyu wa miundombinu, ni vyema kwa wadau kujiunga pamoja ili kunufaika na fursa ambazo serikali imekusudia kuzitoa katika misaada na mipango yake ya maendeleo.
Naye, Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Misitu, Bw. Said Juma Ali, amesema juhudi za utunzaji wa mazingira kwa sasa zinakabiliwa na tishio kubwa, kutokana na mabadiliko ya tabia ya baadhi ya watu kugeukia vivutio vya utalii, vikiwemo komba na kima-punju kuwa kitoweleo.
Katika ziara hiyo, Mheshimiwa Othman, aliongozana na viongozi mbali mbali wa Kiserikali na wa kijamii akiwemo Katibu Mkuu, Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Dokta Omar Dadi Shajak, Wakuu wa Wilaya za Kaskazini A na B, Ndugu Sadifa Juma Khamis na Ndugu Said Seif, na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi na Uendeshaji wa Mazingira, Bw. Sheha Mjaja.
No comments:
Post a Comment