Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Prof. Makame Mbarawa (wa pili kulia), akisisitiza jambo kwa Kaimu Meneja wa uwanja wa ndege wa Arusha Bw, Reston Mtafya alipokagua maendeleo ya ujenzi wa uwanja huo.
Kaimu Meneja wa uwanja wa ndege wa Arusha Bw, Reston Mtafya (kulia), akifafanua jambo kwa Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Prof. Makame Mbarawa alipokagua maendeleo ya ujenzi wa uwanja huo.
Muonekano wa barabara ya kuruka na kutua ndege (run way), iliyojengwa kuongeza urefu wa uwanja wa ndege wa Arusha ili kuruhusu ndege kubwa aina ya Q 400 na ATR 72 kutua katika uwanja huo.
Profesa Mbarawa amesema hayo mara baada ya kukagua upanuzi na ukarabati wa miundombinu ya maegesho ya ndege, magari na njia ya kuruka na kutua ndege (run way) katika uwanja huo.
“Nimekagua kazi ni nzuri hongereni, ila nitaleta timu hapa iniambie hizi gharama za ujenzi mnazozitaja kama zinaendana na thamani ya fedha,” amesema Prof. Mbarawa.
Amewataka wafanyakazi wa uwanja wa ndege huo kufahamu umuhimu wao katika kutoa huduma bora kwa watalii na abiria wengine ili kuvutia watu wengi kutumia uwanja huo na hivyo kuongeza mapato.
Amesisitiza kuwa uwanja wa ndege wa Arusha ni wa tatu kwa mapato na wa pili kwa miruko ya ndege na abiria katika biashara ya usafiri wa anga hapa nchini ukitanguliwa na uwanja wa ndege wa Dar es Salaam (JNIA) na Mwanza hivyo Serikali inautazama kikamilifu.
Naye Kaimu Meneja wa uwanja wa ndege huo Bw. Reston Mtafya amesisitiza kuwa watumishi wamejipanga vizuri kimaadili, nidhamu na ubunifu ili kuleta tija katika kazi zao.
“Tumejipanga kuhakikisha uwanja wetu unatumiwa na abiria wengi kwa kutoa huduma za viwango vya juu,” amesisitiza Mtafya.
Katika hatua nyingine Waziri huyo wa Ujenzi na Uchukuzi amekagua karakana ya Wakala wa Ufundi na Umeme nchini TEMESA mkoa wa Arusha na kuwataka kufanyakazi zinazopimika na kumpa ripoti za kazi hizo kila mwezi.
Amewataka kuhakikisha malalamiko ya watumiaji huduma za TEMESA yanafika mwisho kwa kutoa huduma za kisasa, kibingwa na za haraka katika fani ya utengenezaji wa magari, mitambo na umeme .
“Kila mwezi nataka ripoti ioneshe mezalisha kiasi gani cha fedha, mmekusanya shilingi ngapi na mmetoa huduma kwa kiwango gani ili tuwapime na watakaoshindwa watupishe,” amesisitiza Prof. Mbarawa.
Amezungumzia umuhimu wa TEMESA kufanya majukumu yake ya msingi katika kutoa huduma na kuwatumia wahitimu wa VETA na Vyuo vya Ufundi kufanya mazoezi ili kuwajengea uwezo wakati wanatafuta ajira.
Prof. Mbarawa yuko katika ziara ya siku tatu mkoani Arusha kukagua miradi ya maendeleo ya taasisi zilizo chini ya Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi.
IMETOLEWA NA KITENGO CHA HABARI NA MAWASILIANO SERIKALINI WIZARA YA UJENZI NA UCHUKUZI
No comments:
Post a Comment