FAMILIA YA RIADHA YAMMWAGIA SIFA RAIS SAMIA - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Monday 11 October 2021

FAMILIA YA RIADHA YAMMWAGIA SIFA RAIS SAMIA

Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Michezo nchini (katikati) Yusufu Omary Singo akiongoza kikao cha wadau wa mchezo wa Riadha kujadili maendeleo ya Riadha  kulia ni Kaimu Katibu mtendaji wa Baraza la Michezo la Taifa, kushoto Rais wa Shirikisho la Riadha, Silasi Lukas.

Na John Mapepele, Arusha

WADAU wa mchezo wa Riadha nchini wamempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Mhe, Samia Suluhu Hassan kwa kuwekeza katika michezo ambayo imeanza kuleta matokeo makubwa kwa timu za Taifa za mpira wa miguu kwa wanawake kufanya vizuri kwenye mashindano ya kimataifa na kuiingiza Tanzania kwenye ramani za kimataifa.

 

Wakizungumza kwenye kikao cha kitaifa cha wadau wa mchezo wa Riadha kujadili maendeleo ya mchezo wa riadha kilichoratibiwa na Wizara ya Sanaa, Utamaduni na Michezo jijini Arusha Oktoba 10, 2021 wamesema Timu ya Taifa ya Wanawake ya Mpira wa Miguu (Twiga Stars) imechukua Kombe la COSAFA jana kutokana mikakati Madhubuti inayofanywa na Serikali.

 

Mkimbiaji wa kimataifa Suleimani Nyambui akichangia katika kikao hicho amesema maelekezo ya Rais Samia ya hivi karibuni ya kuitaka Wizara ya Sanaa, Utamaduni na Michezo, kwa kushirikiana na Baraza la Michezo la Majeshi Tanzania (BAMMATA) na Baraza la Michezo la Taifa (BMT) kujadili mikakati ya pamoja ya jinsi ya kuendeleza michezo nchini kutasaidia kuboresha michezo ya kimkakati ikiwa ni pamoja mchezo wa riadha.

 

“Tunafurahi kusikia kuwa Serikali imeandaa Mpango Mkakati wa michezo ambao umeanisha michezo ya kipaumbele tunaomba sasa serikali ianze kuwaweka kambini wachezaji ili waweze kufanya vizuri kwenye mashindano ya jumuiya ya madola yanayokuja”. Ameongeza Nyambui

 

Kocha wa riadha nchini   Robert Kalihaye ameomba Serikali kuangalia  namna ya Serikali kuwapa kipaumbele cha kuwapa ajira  wanariadha  kwenye majeshi bila kuangalia viwango vya elimu zao  ili waweze kuendeleza vipaji vyao kikamilifu.

 

Aliyekuwa Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Riadha iliyomaliza muda wake Meta Petro kutoka Karatu ameipongeza Serikali kurudisha mashindano ya michezo kwenye shule msingi na Sekondari ambapo ameomba vipaji vinavyopatikana kwenye mashindano kuviendeleza.

 

Mwanariadha Mkongwe nchini Steven Akwali amewataka wadau wa riadha kuacha  kutoa visingizio kwa Serikali na  badala yake waanze kufanya  mazoezi  kuanzia kwenye ngazi ya Kijiji  ili kuibua vipaji katika  ngazi ya kitaifa.

 

“Ndugu zangu hata kama Serikali ikitoa fedha kiasi gani haitaweza kutengeneza  vipaji kwa kuwa fedha hazichezi jambo la muhimu ni sisi kuwa wazalendo na kuanza kucheza, sisi miaka ya hamsini tulicheza kama wazalendo bila kujali chochote na tulililetea taifa medali”. Ameongeza Akwali.

 

Rais wa Shirikisho la Riadha nchini Silas Lukasi amewataka makocha wa riadha  kuwa wazalendo ili kuendeleza michezo ambapo amewataka makocha wote nchini  kabla ya mwezi Novemba mwaka huu kuleta vyeti vyao ili kuwa na uratibu mzuri kwenye mchezo huu. 

 

Mratibu wa Michezo kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Riziki Luoga ameiomba Serikali kusimamia na kutenga muda wa michezo ili kuimarisha michezo nchini.

 

Naye Mshindi wa kwanza wa mbio ndefu za mita 10000 kwa upande wa wasichana Failuna Matanga kwenye mashindano ya kitaifa ya Riadha yaliyomalizika jana Oktoba 9, 2021jijini Arusha amewataka wasichana kujitokeza kushiriki kwenye mchezo wa Riadha ili mchezo huu uwe na hamasa kama mchezo wa soka kwa wanawake hatimaye pia kufanya vizuri kimataifa. 

 

Akifungua kikao hicho kwa niaba ya Katibu Mkuu, Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Michezo nchini Yusufu Omary amesema ili kuinua maendeleo ya michezo nchini Serikali imeandaa Mpango Mkakati wa michezo ambao umeainisha michezo ya mkakati ili kufanya vizuri zaidi.

 

Amesema tayari Serikali kupitia Jeshi la Polisi wameshaajiri wanamichezo mia moja ambao watasaidia kuboresha michezo nchini. 

 

Amewataka wadau wa mchezo wa riadha kuacha kufanya siasa badala yake waendeleze  vipaji. 


“Ili kufanikiwa katika michezo lazima kuwe na nidhamu namwagiza tena leo Rais wa Shirikisho na BMT simamieni hili la nidhamu kama wachezaji na viongozi wanakosea wachukuliwe hatua,” amesisitiza  Omary.

 

Kaimu Katibu Mtendaji wa Baraza la Michezo la taifa (BMT) amewaomba kila mdau kuzingatia wajibu wake ili kuendeleza mchezo wa riadha badala ya kuweka maslahi binafsi.

 

“Nadhani umefika wakati wa kila mmoja kuangalia na kujihoji mimi kama kocha, mchezaji au Maliki nimeifanyia nkuitakaji yangu,” amefafanua Msitha.


No comments:

Post a Comment