NAIBU WAZIRI, MHANDISI KASEKENYA AIPA KONGOLE TMA - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Sunday 17 October 2021

NAIBU WAZIRI, MHANDISI KASEKENYA AIPA KONGOLE TMA

Mkurugenzi wa Tehama na huduma za ufundi, Dr. Pascal Waniha (kulia) akimmwelezea Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya namna TMA inavyofanya kazi na sekta za uchukuzi na kusaidia miradi ya maendeleo alipotembelea Banda la TMA kwenye Mkutano wa 14 wa sekta ya Uchukuzi uliokuwa na lengo la kupima utendaji wa sekta mbalimbali za uchukuzi.



Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya (kulia) akipata maelezo ndani ya Banda la Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) kwenye Mkutano wa 14 wa sekta ya Uchukuzi uliokuwa na lengo la kupima utendaji wa sekta mbalimbali za uchukuzi.


Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania, Dk. Agnes Kijazi akitembelea mabanda ya taasisi wadau walioshiriki mkutano huo, kujua namna wanavyonufaika na huduma za TMA.

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania, Dk. Agnes Kijazi akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) waliotembelea banda la TMA kwenye mkutano huo.

NAIBU Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya ameipongeza Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) kwa kuendelea kutoa taarifa za Hali ya Hewa , ambazo zinasaidia katika sekta mbalimbali nchini ikiwemo ya usafirishaji wa ardhini na majini na uboreshaji wa miundombinu ya kimaendeleo.

Naibu Waziri Kasekenya aliyasema hayo jijini Dar es salaam alipokuwa akizungumza kwenye Mkutano wa 14 wa sekta ya Uchukuzi uliokuwa na lengo la kupima utendaji kazi wa sekta mbalimbali za uchukuzi.

Mhandisi Kasekenya alisema TMA ni muhimu kwani inasaidia sekta zote katika utekelezaji wa miradi ya kimkakati hususani ya barabara kufahamu taarifa za hali ya hewa ambazo ni muhimu katika utekelezaji wa miradi hiyo.

Aidha Mhandisi Kasekenya amesema ni vyema katika ujenzi wa miradi yeyote kuhakikisha unafuatwa utaratibu wa kitaalamu wa kufahamu mazingira hayo ili kuweza kuepukana na madhara yanayoweza kujitokeza.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania, Dk. Agnes Kijazi alisema wamefurahi kupata nafasi ya kuonesha shughuli zao kwa taasisi washiriki wa mkutano huo ambao wengi ni wanufaika wa huduma za TMA.

Alisema shughuli za  uchukuzi zinaendana na masuala ya hali ya hewa hivyo wamekuja kuonesha huduma zao wanazozitoa katika miradi ya maendeleo kwenye sekta nzima ya uchukuzi. 

"...Hapa tukitembelea banda letu utaona tunatoa utabiri wa hali ya hewa na tunaonesha unavyotumika kwenye sekta mbalimbali ambazo zote zinashiriki katika mkutano huo, mfano sekta ya anga, sekta ya reli, masuala ya barabara na kwenye miradi mbalimbali mikubwa ya ujenzi," alisema Dk. Kijazi.

Aliongeza kuwa huduma za hali ya hewa katika kipindi hiki cha mabadiliko makubwa ya hali ya hewa kutokana na mabadiliko ya tabia nchi ni muhimu sana kwenye miradi mikubwa ya maendeleo, kwani zisipo zingatiwa mradi unaweza kuangamizwa na majanga yanayotokana na mabadiliko ya hali ya hewa na kujikuta taifa linaingia katika hasara kubwa.

"...Hapa sisi tupo ili kuonesha umuhimu wa kutumia huduma za hali ya hewa katika shughuli mbalimbali za maendeleo, na ni mahali ambapo ni pa muhimu kwa sababu wawekezaji wenyewe wapo hapa taasisi mbalimbali ambazo zinatumia huduma zetu zipo hapa kwa hiyo banda hili lipo kwa ajili ya kupata huduma. Na tunawaeleza namna ambavyo wanaweza kuzitumia katika shughuli zao kwa hiyo kwetu tumeona ni fursa muhimu sana ya kuelezea huduma zetu," alisema.

No comments:

Post a Comment