*Kuwatunuku zawadi wateja wake kupitia promosheni ya Muda wa maongezi
KAMPUNI ya simu ya Viettel au maarufu kama Halotel, inayojikita kupeleka mawasiliano vijijini, leo inatimiza miaka sita ya kutoa huduma hapa nchini huku ikidhamiria kufikia idadi ya wateja milioni 10 kufikia mwaka 2023.
Mkurugenzi Wa Biashara – Halotel, Abdallah Salum, amesema hayo leo wakati wa mkutano na waandishi wa habari kuhusu mafanikio yaliyopatikana kwa kipindi hiki cha miaka sita.
Mkurugenzi Wa Biashara amesema kuwa katika kipindi hicho kampuni imekuwa ikisajili wateja zaidi ya milioni moja kwa mwaka.
Kwa mujibu wa ripoti ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), hadi kufikia robo ya tatu ya mwaka 2021 kampuni imeweza kusajili wateja milioni 7.
“Kwa kipindi cha miaka miwili ijayo tunapanga kuwekeza zaidi kwenye miundombinu ya mtandao kwa kuiboresha zaidi, kuongeza ubora wa huduma na kupanua wigo wa mtandao wetu ili kukidhi mahitaji ya wa jamii kwa vile dunia inahitaji sana huduma za kidijitali. Eneo lingine tutakalowekea mkazo ni kuongeza wateja wa Halopesa kufikia milioni tano,” Salum alisema huku akianisha kuwa kwa sasa kuna idadi ya wateja zaidi ya milioni 2.3.
Alibainisha kuwa Halotel tayari imezindua huduma ya 4G katika maeneo mengi hapa nchini na imejenga vituo vya kusambazia huduma hiyo katika maeneo mengi ambapo idadi ya vituo hivyo kwa sasa ni mara mbili zaidi ya idadi iliyokuwa awali. Wateja wanaotumia laini za 3G kwa sasa wanaweza kubadili laini zao kutoka 3G kuwa za 4G bila malipo.
“Kwa huduma ya 4G, wateja wa Halotel ambao wanatumia huduma ya 3G wanaweza kubadili laini zao za 3G kuwa za 4G bila malipo na watapata ofa ya intaneti ya GB4 bure za kutumia kwa muda wa siku tatu,” Bw Salum alifafanua.
Akiwashukuru wateja kwa kuendelea kuunga mkono kwa kuchagua mtandao wa kampuni ya Halotel, Mkurugenzi Wa Biashara huyo alisema kuwa kampuni ina mipango madhubuti ya kuendelea kutoa huduma bora kwa wateja wake hapa nchini.
“Katika kusherehekea miaka sita na kuhakikisha kuwa huduma inawafikia watu wengi, tungependa kuwashukuru wateja wetu kwa kuendelea kuchagua mtandao wa Halotel kwa kipindi chote hicho na kwa hiyo leo tunawazawadia wateja wetu wote kupitia kampeni maalumu ijulikanayo kama ‘Recharge promotion’. Kupitia kampeni hii mteja atapata asilimia 20 zaidi ya salio atakaloliongeza, kwa mfano Mteja akiongeza salio la shilingi 1000 atapata sh.200 ya ziada. Promosheni hii ni maalum kuanzia tarehe 15 hadi 16 mwezi huu,” amesema.
Aidha HaloPesa chini ya Halotel inasheherekea miaka mitano ya kutoa huduma bora za kifedha. Na katika kusheherekea HaloPesa inapenda kutoa shukrani kwa kuwapa wateja promosheni ya kurudisha asilimia 100 ya makato mteja atakayokatwa na Halopesa akituma pesa kwenda Halotel na anapo nunua Luku kuanzia tarehe 15 Oct, 2021 na promosheni hii itaisha tarehe 16 Oct, 2021.
“Mpango wetu mwingine ni kuwekeza zaidi katika kutoa huduma ya teknolojia ya habari na mawasiliano (Tehama) ili kuwafanya watumiaji wa simu janja kuweza kuperuzi kwenye mitandao ipasavyo,na kuweza kunufaika kutokana na mahitajiyao mbalimbali katika kuwapa maendeleo ya kiuchumi na kijamii” ameeleza.
Kampuni ya Halotel ni tawi la kampuni ya kivietnam Viettel Group ya nchini Vietnam ambayo ilianza kutoa huduma zake hapa nchini mnamo Octoba mwaka 2015 kwa kujikita zaidi kupeleka huduma za mawasiliano watu waishio vijijini, na hivyo kufanya kampuni hiyo kufikia asilimia 95 ya Watanzania.
No comments:
Post a Comment