Sheikh wa Mkoa Singida Issa Nassoro akiwa na viongozi wa kiislamu wakati akiwasili kwenye Maulidi ya kumswalia Mtume Mohammad ( S.A.W) yaliyofanyika Kata ya Kinyeto mkoani hapa jana. |
Diwani wa Kata ya Ilongero, Issa Mwiru ambaye pia ni Mwenyekiti wa Bakwata wilaya hiyo akizungumza kwenye maulidi hayo. |
Wanawake wa Jumuiya ya Wanawake wa Kiislamu ( JUWAKITA) Wilaya ya Singida Vijijini kwenye Maulidi hayo.
Na Dotto Mwaibale, Singida
WAISLAMU Mkoa wa Singida wametakiwa kuhamasishana ili kupata fedha zitakazo saidia kujenga Ofisi za Baraza Kuu la la Waislamu Tanzania (BAKWATA) katika kila Kata.
Ombi hilo limetolewa na Sheikh wa Mkoa wa Singida Issa Nassoro wakati akizungumza na Wanawake wa Jumuiya ya Wanawake wa Kiislamu ( JUWAKITA) Wilaya ya Singida Vijijini kwenye Maulidi ya kumswalia Mtume Mohammad ( S.A.W) yaliyofanyika Kata ya Kinyeto mkoani hapa jana ambayo yalikwenda sambamba na harambe ya upatikanaji wa fedha za ujenzi wa jengo la ofisi ya Juwakita.
" Makatibu wote wa Kata nawaagiza kila kata ianze mikakati ya kujenga ofisi ya Bakwata ya Kata.Mwenyekiti wa Kata, Sheikh wa Kata tafuteni viwanja vya kujenga ofisi ya kata,". alisema Nassoro.
Katika hatua nyingine Nassoro aliagiza viongozi wa misikiti yote iliyopo katika kata hiyo Katibu, kamati, wajumbe ambao ni wasuluhishi kwenye misikiti wahakikishe kila imamu wa misikiti katika kata hiyo ya Kinyeto anapata bima ya afya.
Nassoro pia aliagiza kila Sheikh wa wilaya anataka awe na bima hiyo na alitoa mwezi mmoja ili kukamilika kwa jambo hilo.
Alisema baada ya kukatiwa bima kundi hilo litafuata kundi la walimu wa madrasa ambao siku zote wanaonekana ni watu wenye hali duni na kuwa kila madrasa na wazazi ambao watoto wao wanasoma kwenye madrasa hizo watalazimika kutoa michango kwa ajili ya kufanikisha mpango huo.
Aliwata waislamu kujenga hospitali itakayosimamiwa na Juwakita mkoa kwa ajili ya kustili hali za wanawake wa kiislamu wakati wakijifungua tofauti na sasa ambapo wanazalishwa na madaktari wenye umri mdogo.
Alisema wakiwa na hospitali zao watazalishwa na wauguzi wa kike na madaktari wao wa kiislamu hivyo kutunza stala zao.
Aliwataka wanawake hao kutambua nafasi yao katika uislamu na wakisimama kidete na kuwa kwenye msimamo umma wa kiislamu utanyooka.
Nassoro ameagiza kila wilaya kufanya sensa ili waweze kujua tathmini ya waislamu na kila muislamu wafahamu atachangia kiasi gani na kujua wanayatima na wajane wangapi jambo litakalosaidia kuwapatia msaada.
Katibu wa Juwakita Wilaya ya Singida Vijijini Hawa Shabani alisema jumuiya hiyo imefanikiwa kununua kiwanja cha jengo la mradi wa kiuchumi linalogharimu zaidi ya Sh.70 milioni.
No comments:
Post a Comment