SERIKALI imewapongeza Wadau mbalimbali wa maendeleo waliojitokeza katika kikao kazi cha Sekta ya Afya Mkoani Singida na kujitolea viwezeshi mbalimbali vitakavyosaidia kuendesha zoezi la utoaji wa hamasa, elimu na chanjo kwa jamii .
Baadhi ya wadau hao wameahidi kusaidia upatikanaji wa magari ya matangazo, mafuta kwa ajili ya safari za vijijini huku wengine wakiwa tayari kusaidia kupeleka elimu waliyoipata kuhamasisha jamii juu ya zoezi la uchanjaji lengo likiwa na kufanikisha kwa kiwango kikubwa.
Pongezi hizo zimetolewa leo kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Singida na Mganga Mkuu wa Mkoa Victorina Ludovick wakati wa mkutano huo uliofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Hoteli ya KBH na kubainisha kwamba jitihada zinazooneshwa na wadu hao zitasaidia katika kuwafikia watu wengi vijijini na kutoa elimu ya chanjo.
Mganga Mkuu wa Mkoa Singida Victorina Ludovick akieleza jambo wakati wa mkutano huo.
Pamoja na hayo Mganga mkuu amesema kwamba Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbalia itaendela kusambaza huduma ya chanjo dhidi ya ugonjwa wa UVIKO 19 katika maeneo mbalimbali Mkoani Singida kama hatua muhimu ya kupambana na kudhibiti ugonjwa huo.
Amesema Chanjo zinaendelea kusambazwa kwenye vituo vya kutolea huduma ambapo awali vilikuwa vituo 21 vilivyoanishwa na Serikali lakini kupitia Mkakati Shirikishi na Harakishi, Serikali itawafikia wananchi kupitia vituo 219 vinavyotoa huduma za Chanjo.
“Chanjo tayari zipo katika vituo vya kutolea huduma, lakini tunayo changamoto kubwa ya kufikisha elimu na hamasa ili wananchi wakubali kuzitumia” Alikaririrwa Mganga Mkuu
Aidha amebainisha kwamba jamii imekuwa na mwitikio mdogo katika kupokea chanjo sababu kubwa ikiwa ni hofu iliyojengeka licha ya jamii kushuhudia wananchi wengine wakiendelea kunufaika bila kuwepo kwa madhara yoyote.
Kutokana na muingiliano mkubwa uliopo hasa kibiashara na kijamii kati ya Mkoa wa Singida, Mikoa mbalimbali na Nchi nyingine, ni muhimu kuchukua tahadhari za kutosha ili kuukabili ugonjwa, Alibainisha Dkt Ludovick.
Aidha Dkt Ludovick. amesisitiza kwamaba Chanjo zilizoruhusiwa kutumika hapa nchini ni salama hivyo kila mtanzania ana hiari ya kupata chanjo hiyo na kuwataka kutokuwa na hofu .
Aidha amewataka Wadau wote na viongozi wa Dini kusaidia jithada za Serikali ili Chanjo ziweze kuwafikia wananchi wote wenye uhiari wa kupatiwa Chanjo ili kuiweka jamii salama.
Alimalizia kwa kusema kwamba Jukumu la kinga dhidi ya ugonjwa huu ni la kila mtanzania hivyo kutoa wito kwa jamii kuendelea kuzingatia afua za kinga.
Hivyo, Wizara ya Afya inawataka Viongozi wote wa serikali, sekta binafsi, Viongozi wa Kijamii na madhehebu ya dini kuwajulisha wananchi wote kuchukua tahadhari zote muhimu, kuelimisha, na kutekeleza afua za kujikinga .
Awali mratibu wa Malaria mkoani Singida Dkt. Abdallah Balla alieleza lengo la mkutano huo kwamba ni kutoa taarifa kuhusu hali ya UVIKO-19 na udhibiti wake katika Mkoa wa huo na kubadilishana uzoefu pamoja na kuyatambua maeneo Serikali iliyofanya vizuri.
Dkt. Abdallah aliendelea kusema mkutano huo utasaidia kuongeza ufanisi na ubora unaohitajika katika utoaji wa huduma za afya kwa kuzingatia viwango vilivyowekwa na Serikali na kuwepo kwa mfumo mmoja wa utoaji huduma unaoshirikisha wadau wote ( mfumo wa rufaa – “Vertical and Horizontal referrals”)
Mwenyekiti wa dini mbalimbali Mkoa wa Singida Sheikh Hamisi Mohamedi Kisuke akizungumza wakati wa mkutano
Naye Mwenyekiti wa dini mbalimbali Mkoa wa Singida Sheikh Hamisi Kisuke ameiomba serikali kuendelea kutoa elimu juu ya chanjo hasa kwa vijana kwa kuwa katika kipindi hiki wameonekana kutokujali ugonjwa huku wengi wao wakiwa hawajapata chanjo.
Ameihakikishia serikali kwamba kwa upande wa dini wanazo simamia wanaunga mkono na watashiriki kikamilifu katika utoaji wa elimu ya chanjo kwa jamii kwa kuwa vitabu vya mwenyezimungu vinataka jamii kujikinga na mambo yenye kuangamiza. Alifafanua sheikh Kisuke.
Askofu wa Kanisa la Tanzania assemblies of God (TAG) Jimbo la Singida Kati Rev.Gasper Mdimi amesema wamejipanga kuhakikisha wanashirikiana na Serikali kutoa elimu na hamasa juu ya chanjo ili kuwaepusha watanzania juu ya madhara makubwa yanayoweza kutokana na ugonjwa wa KOVID 19.
Mratibu wa Malaria Mkoa wa Singida Dkt. AbdallaH Balla akieleza lengo la mkutano huo
No comments:
Post a Comment