Sehemu ya washiriki wa mkutano huo wakifuatilia mada anuai. Meneja Programu wa TenMet, Bw. Nicodemus Shauri akiwezesha mjadala kwenye mkutano wa wadau wa elimu uliowakutanisha kuangalia kwa pamoja utekelezwaji wa programu ya Dunia Yangu Bora.
Kaimu Mkurugenzi Elimu ya Msingi, Venance Manori akiwa katika mjadala kwenye mkutano wa wadau wa elimu uliowakutanisha kuangalia kwa pamoja utekelezwaji wa programu ya Dunia Yangu Bora. Kushoto ni Meneja Mwandamizi Usawa wa Kijinsia na Programu za Elimu kwa Mtoto wa Kike kutoka Asasi ya 'Roo to Read', Bi. Zamaradi Islahi.
Washiriki katika mkutano huo wakichangia mada. Mmoja wa wanafunzi wanufaika wa programu hiyo akizungumza na wadau katika mkutano huo.
Na Joachim Mushi, Dar
SERIKALI kupitia Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia imesema inaangalia uwezekano wa kuitumia programu maalum ya Dunia yangu Bora, inayoambatana na stati za maisha kwa wanafunzi inayotekelezwa katika baadhi ya maeneo nchini na Shirika la CAMFED Tanzania kumuwezesha mwanafunzi kufikia malengo yake.
Kauli hyo imetolewa leo jijini Dar es Salaam na Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia, Profesa Caroline Nombo alipokuwa akizungumza na wadau wa elimu waliokutana katika mkutano kuangalia kwa pamoja utekelezwaji wa programu ya Dunia Yangu Bora, mafanikio na changamoto zake hasa kwa watoto wa kike shuleni.
Profesa Caroline Nombo, ambaye alikuwa mgeni rasmi katika mkutano huo alisema programu hiyo inawasaidia vijana kujitambua, kuwasaidia ujuzi mbalimbali wa kuendesha maisha na hata shughuli za biashara hapo baadaye baada ya masomo yao, hivyo kuna umuhimu wa kuangalia namna ya kuiingiza katika mfumo maalum kuweza kuwasaidia vijana zaidi.
"Leo tumekutana hapa wadau mbalimbali na kuona programu hii inayotolewa na Shirika la CAMFED na namna walivyofanikiwa na kutafakari kwa pamoja, pia kuangalia namna ambavyo tunaweza kuboresha programu hii kwa vijana na hata kuiingiza kwenye mfumo wa elimu yetu Tanzania," alisema Profesa Nombo.
Alisema taasisi za Serikali pia zimeshiriki katika kongamano hilo nazo zitaangalia namna zinaweza kuuchukua programu hiyo na kuingiza katika mifumo ya shule kwa lengo la kuwasaidia vijana kwanza wapate elimu stahki na hata stadi za maisha zinazoweza kuwawezesha kukabiliana na changamoto watakapomaliza elimu zao.
"Kwa hili niwahakikishie wadau wa elimu maandalizi yanafanyika na tupo katika hatua nzuri kuweza kuingiza katika mfumo wetu wa shule...naomba kuhamasisha wadau tuendelee kushirikiana kuhakikisha vijana wetu wanapata elimu bora kama ilivyo katika haki ya msingi kwa mtoto," alisisitza Profesa Nombo.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa CAMFED Tanzania, Bi. Lydia Wilbard akizungumza na wadau alisema wataendelea kushirikiana na Serikali kuhakikisha changamoto zinazowakumba watoto kwenye elimu zinapata ufumbuzi, kuanzia wawapo shuleni na hata baada ya kumaliza shule na kurejea katika maisha yao kwenye jamii.
Alisema wamekutana katika mkutano huo na wadau kuwashirikisha kuiangalia programu hiyo kubwa ambayo wamekuwa wakiitekelezwa tangu mwaka 2o13, huku ikijikita kuangalia vijana hawaenguliwi katika mfumo wa elimu kwa changamoto zozote na kuwawezesha pia kukabiliana na changamoto za kiuchumi mara baada ya kumaliza masomo yao hapo baadae.
"...Programu pia imejikita kuangalia kijana anapotoka shuleni na kurejea 'mtaani' anakwendaje na hasa kama ni msichana na anatoka kwenye mazingira magumu, CAMFED katika programu hii inawatumia wasichana wa kujitolea waliosomeshwa shule kupitia shirika letu na wamekuwa wakirudi kwenye shule hizo na kuwafundisha stadi za maisha, kuwatia moyo ili wafikie malengo yao na hapo hapo kushirikiana na walimu kuwafuatilia wanafunzi kwenye utoro," alibainisha Bi. Lydia Wilbard.
"Mafanikio ya programu hii ndio yaliosababisha wadau leo kukutana kwa pamoja kuanzia wale wa serikalini, taasisi binafsi, wadafunzi, wazazi na walimu ili kuangalia programu ya Dunia yangu Bora tunawezaje kushirikiana na kuisambaza nchi nzima, kwani sasa tunaitekeleza kwenye wilaya takribani 27 na kwenye Shule za Sekondari 404, lakini tuna zaidi ya shule za sekondari 5,000...," alieleza Mkurugenzi huyo wa CAMFED Tanzania.
No comments:
Post a Comment